Pages

Monday, September 5, 2022

UHEHENI ILIKUWA MARUFUKU KUMWAGA DAMU YA NDUGU WA MUTWA


 Nchi ambayo sasa inaitwa Uhehe, awali ilikuwa na Vatwa wengi, (mmoja;Mutwa). Nisingependa kutumia neno Chief maana halitoshelezi kutafsiri neno Mutwa.
Kuanzia zama za Mihwela, wale Vatwa wa vikabila mbalimbali vilivyotekwa au vilivyokubali kutawaliwa na Mutwa, wakawa sasa wanaitwa Vansagila. Hii iliendelea mpaka hatimae Mutwa wa Uhehe akaja kuwa mmoja tu Mutwa Mukwava, lakini tufwatilie simulizi hii ili kujua Mkwava alifikiaje nafasi hiyo.

Vatwa waliheshimika mno Uheheni, mtoto wa kiume wa Mutwa aliitwa Mwaluka, wengi waliitwa Valuka. Mtoto wa kike wa Mutwa aliitwa Munumwehe. Mkwe wa Mutwa hasa yule aliyeoa binti wa Mutwa alitambulika kama  Mwanamutwa.

Mutwa alikuwa na salamu yake maalumu, alisalimiwa 'Ase Senga' nae alijibu 'Asee'.
Mwiko mkubwa wa ukoo wa Mutwa ni kumwaga damu ya ndugu. Kuna hadithi za ajabu sana kuhusu imani hii ambayo iliheshimiwa sana. Kuna hadithi moja ilimuhusu Mabohola mtoto wa Munsagila Ngawonalupembe aliyekuwa kiongozi wa jeshi la Vanyamwani kutoka Ubena,  wakati fulani Mkwawa na Mabohola walikuwa wakipigana na Wangoni, Mutwa Mukwawa akaona kuwa vita imekuwa kali mno bora akimbie  atoroke wakati wa usiku. Mabohola akamsihi asifanye hivyo, akamwambia akikimbia usiku, Wangoni wataelewa kuwa kaelemewa na watamfuata, lakini akifanya kama anarudi nyuma wakati wa mchana, adui wangejua anaenda kujipanga mahala pazuri zaidi hivyo adui angesita kumfuata. Wazo lile lilifanikiwa na Mkwava akaweza kurudi Kalenga salama. Lakini Mkwava alianza kuona kuwa Mabohola ana akili mno anaweza kuja kumpindua, na kuna wazee wengine husema kuwa kiutaratibu Mabohola alikuwa na haki sawa kiukoo kuweza kutawala Uheheni kama alivyokuwa nayo Mkwava wakati huo. Mkwava akaona Mabohola ni tishio na hakutakiwa aishi zaidi. Siku moja akamkaribisha Mabohola kwenye Ivaha yake Kalenga, askari wa Mabohola walimuonya kuwa ni hatari kwenda Kalenga.  Mabohola aliamua kwenda, na alipofika kalenga watu wanne waliokuwa wamepangwa wakamkamata na kumnyonga, hawakutumia mkuki ili wakwepe kipengele cha kumwaga damu ya ndugu wa Mutwa. Inasemekana Mkwava alipokuwa akiangalia ndugu yake akinyongwa alisema, 'Wutema wutalamu' yaani 'Ukuu ni mgumu'.

Wakati ule Mwamubambe alipoamua kumuua Muhalwike, aliyepewa Wutwa baada ya kifo cha Munyigumba, askari aliyepewa kazi ya kumchoma mkuki alikataa na kuamua kujiua kwa kujichoma mkuki mwenyewe kuliko kumwaga damu ya Mutwa. 

Hadithi nyingine ilihusu Mpangile , mdogo wake Mukwava, kwa sababu moja au nyingine aliwahi kuchoma mkuki na kuuwa ng'ombe 40 wa kaka yake , Mkwava alikasirika sana lakini hakuweza kumwaga damu ya ndugu yake, badala yake akamchukua mke wa Mpangile aliyekuwa mzuri kuliko wote na kumchuna ngozi ya uso.

Damu ya hawa ndugu wa Mutwa ilikuwa inathaminiwa kiasi cha kwamba hata vitani hawakuruhusiwa kuwa mstari wa mbele.
Hadithi nyingine ilihusu Merere. Munyigumba aliwahi kumuoza Mutwa Merere binti yake mmoja mzuri sana katika makubaliano yao ya kupata amani, bahati mbaya binti yule akapata ugonjwa wa ndui, na kupofoka macho. Merere akamrudisha yule binti Uheheni kwa Muyigumba, jambo hilo lilimuudhi sana Mutwa Muyigumba, akatuma jeshi lake kwenda kumpiga Merere, lakini pamoja na yote akatoa amri, 'Mugonage si senga, sa mulagela mutose migoha, uyo mwanangu' Yaani, tekeni ng'ombe lakini msijaribu kumtupia mikuki huyo ni mwanangu, kwani Merere alikwisha kuwa Mwanamutwa kwa kumuoa binti ya Muyigumba. Hivyo ndivyo ilivyothaminiwa damu ya Vatwa na ndugu zao.

Monday, August 29, 2022

MKWAVA APOKELEWA NA MUYOVELA UGOGONI

 


Mukwava inasemekana alizaliwa Luhota kwenye mwaka 1855. Alipokuwa mdogo aliitwa Ntasalatsi, yaani mtu mwenye kupapasa kwa mikono na vidole anapotafuta kitu. Mkwava aliishi kwenye nyumba iliyokuwa haikosi simulizi za ushujaa wa baba yake na askari wake. Akiwa bado mdogo baba yake, Mutwa Munyigumba, alikwenda kuwa kuwapiga Wasangu na kupanua utawala wake mpaka Ng’uluhe.
Mutwa Mihwela alipokufa, mtawala ambaye alikuwa mjomba wa Muyingumba na aliwahi kumlea kwa muda mrefu,   Muyigumba alifanya kila hila mpaka binamu yake Myovela akalazimika kukimbia himaya yake na kwenda kujificha Ugogoni, na Munyigumba aliweza kuiteka kirahisi himaya hiyo na ikawa chini yake, na baadae akaweza kumnyan'ganya himaya binamu yake mwingine Mwengamagoha, mdogo wake Myovela, ambaye naye alilazimika kukimbilia alikokuwa kaka yake. Munyigumba akaweza kuunganisha koo ndogondogo nyingi kuwa chini yake na hakika alikuwa ni muhimili mwingine katika ujenzi wa kabila la Wahehe.

Munyigumba akaweka  Ivaha(ikulu) yake Muhana  sehemu iliyoka jirani na Luhota, na huko ndiko kulikuwa na kambi ya kuwazoesha vijana wa jeshi lake mbinu za vita. Kwa vile utawala wake ulipanuka sana, Munyigumba akaweka watu wake waaminifu kuwa viongozi kwenye sehemu mbalimbali alizokuwa akizitawala. Viongozi hawa waliitwa Vanzagila. Hawa pia walikuwa viongozi wa jeshi lililokuwa chini yao ambalo Mutwa angeweza kuwaita wakati wowote.

Kati ya mateka wa vita za Muyigumba alikuweko mateka mmoja wa Kinyamwezi, mateka huyu alikuwa mtoto. Mateka huyu alianza kutumiwa kwa kutumwa kubeba dawa za zilizoaminika kuwa ndizo zilikuwa za kulinda ukubwa, akaanza kuaminika na kupendwa sana na Munyigumba. Pamoja na ushauri aliopewa na wazee kuhusu kujihadhari na mapendo na madaraka makubwa aliyokuwa akimpa mtu huyu, Munyigumba aliongeza tena kwa kumwozesha mtu huyu binti yake. Mtu huyu aliitwa Mwanakimamule, ila jina lake lililokuja kuwa maarufu lilikuwa Mwamubambe au Mwambambe.

Mwambambe alikuwa jitu la miraba minne lenye nguvu sana, inadaiwa vitani alikuwa akitangulia mbele na yeye alikuwa anawakamata adui kwa mikono yake na kuwavunja kisha kuwatupa nyuma yake wamalizwe na askari waliokuwa wakimfuata.  Inasemekana katika kuwa mtumwa wa kubeba madawa ya Munyigumba na yeye alitumia madawa hayo ya mizimu hivyo ikawa si rahisi kumuua.  Katika ile vita ambapo Wangoni walimzingira Muyugumba na jeshi lake katika mapango ya Nyamulenge, Mwamubambe na Mkwawa walikuwa bega kwa bega walipoenda kumuokoa Munyigumba. Kiasi cha mwaka mmoja baada ya kuokolewa kutoka kwa Wangoni, Mutwa Muyigumba akafariki.
Na bada ya muda kukatakiwa kuchaguliwe mtu wa kumrithi.  Wazee wa ukoo wa  Muyinga wakaingia katika wakati mgumu wa kuchagua mtu sahihi kwani walijua wazi kuwa Mwamubambe angewasumbua, hivyo wakawa wanatafakari nani angeweza kutawala na kuweza kumdhibiti Mwamubambe ambae alikuwa na nguvu nyingi pamoja ya kuwa hakuwa mwenyeji. Hatimae wakamteua Muhalwike arithi kiti cha Munyigumba,  haikuchukua muda  Mwamubambe alimuua Muhalwike, na wengine husema alishawishiwa na mkewe mtoto wa Munyigumba. Mwamubambe akamtawaza ndugu yake mmoja aliyeitwa Muhenga kutawala himaya ya Muyigumba, huyu Muhenga alikuwa mtawala jina tu kwani Mwamubambe ndie aliyetawala haswa. Watoto wengine kadhaa wa Muyigumba waliendelea kuuwawa na Mwamubambe, kwa usalama wake Mkwava akalazimika kuimbia himaya iliyokuwa ya baba yake.
Kitu cha ajabu akalazimika kukimbilia  Nondwa Ugogoni kwa mjomba Muyovela. Ikumbukwe kuwa Muyovela alikimbilia Nondwa kwa kufukuzwa na Muyigumba baba yake Mkwava. Ila ni wazi Mkwava alijua kuwa Myovela hakuwa mtu wa visasi, kwani hata mdogo wake Mwengamagoha aliwahi kumsaliti na kujiunga na Muyigumba lakini mambo yalipomuharibikia alikimbilia kwa kaka yake Myovela na akapokelewa bila kinyongo.
Ilikuwa katika wakati wa msafara huu wa kukimbilia Ugogo ambapo inadaiwa mama yake Mukwava, Sengimba, alijitupa kwenye mto sehemu iliyoitwa Kikongoma. Katika sehemu hii mto unapita chini ya ardhi, wenyeji hupaita hapo Daraja la Mungu.
Kuna hadithi mbalimbali kuhusu tukio hilo. Kuna wanaosema mama huyo alikuwa kwenye msafara wa Mwanawe wakielekea Ugogoni ndipo alipoamua kujitosa  kwani hakutaka kuendelea na safari na hakutaka kutekwa na Mwamubambe. Kuna hadithi nyingine za wazee wanasema mama huyo alitekwa na Mwamubambe akawa anadaiwa akaonyeshe zilipo dawa zilizokuwa zikimfanya mumewe Muyingumba kuweza kutawala, hivyo aliwaelekeza kuwa zipo hapo Kikongoma, lakini walipofika aliwaambia kuwa dawa hizo hazitakiwi kuonekana na wanaume hivyo apewe wanawake wa kumsindikiza kuzifuata, na ndipo alipofika kwenye daraja hilo akajitosa mtoni na kujiua.

Msafara wa Mkwava ulipofika jirani na Nondwa, ujumbe ulitumwa kwenda kuomba hifadhi, Muyovela hakuwa na kipingamizi lakini mtoto wake,  Mubogamasoli, hakutaka kabisa kusikia habari za Mkwava, kwanza alikumbusha jinsi baba yake Mkwava alivyowanyang’anya nchi, pili Mubogamasoli alikuwa na uchungu wa kunyang’anywa mpenzi wake na Mkwava. Kabla ya kukimbilia Nondwa, Mubogamasoli alikuwa kamchumbia Semsilamugunda, lakini alipoondoka huku nyuma Mkwava akamuoa Semsilamugunda, ambaye ndiye alikuja kuwa mama  wa mwanae wa kwanza Sapi, baba ya Mutwa Adam Sapi.

Ili kumtuliza mwanawe, Muyovela akamuahidi kuwa Mkwava hataletwa Nondwa, akatuma watu wakamchukua Mukwava na kumpeleka Nzuguni, Muboga masoli akatulia.
Nae  Mkwava alipofika Nzuguni akaanza kupanga namna ya kurudi kwao kwenda kuchukua himaya ya baba yake

   

 

Sunday, August 21, 2022

MKWAVA ALIPOIKIMBIA NCHI YA BABA YAKE

 


Baada ya Shaka ka Senzangakhona, au kwa jina maarufu Shaka Zulu,kurithi utawala wa Wazulu baada ya kifo cha baba yake, kati ya  mwaka 1818 na 1828 alianzisha utawala wa kikatili wa kuua na kuteka tawala zilizokuwa jirani yake. Kipindi hiki kigumu kwa Wazulu kilipewa jina Mfecane, viongozi wa makabila makubwa kama Zwangendaba, Mzilikazi, na  Shoshangane wakaanza kuhamisha watu wao na kuelekea kaskazini mwa nchi yao ya awali ili kukimbia vita hizo za Shaka Zulu, nao katika kusafiri kwao wakapiga na kuteka mali za makabila walioyakuta njiani mwao bila huruma. 
Wavamizi hawa wengine wakaingia eneo sasa linaloitwa Tanzania kupitia iliko Malawi, wengine wakabaki sehemu ulipo mkoa wa Ruvuma hawa wakaja julikana kwa jina la Wangoni, jina lililokuwa kwa asili  la ujumla wa makabila mengi yaliyokuwa jirani na Wazulu.  Baada ya kutujila na kujijenga sehemu hii, mwaka 1878 jeshi la Wangoni lilipenya Ubena toka kusini mpaka kaskazini bila upinzani wowote na hatimae kuingia katika himaya ya Munyigumba.
Askari wa jeshi hili la Wangoni, walikuwa hodari wasioogopa kifo. Walitumia bangi kuondoa hofu yoyote, hivyo walifanya walichotaka katika nchi ya Ubena.
Munyigumba alikuwa hajapata nafasi ya kutayarisha majeshi yake kwa uvamizi wa watu hawa kutoka kusini,  hivyo alipojaribu kuwazuia  kazi ilikuwa ngumu sana, majeshi ya Munyigumba yalianza kusukumwa nyuma kwa urahisi kabisa. Munyigumba alirudishwa nyuma hadi karibu na Image na akalazimika kukimbilia kwenye mapango ya Nyamulenge na kujificha humo. Wangoni walipomgundua walimzingira na hakika ilionekana kuwa ndio mwisho wa Mutwa huyo.

Bahati nzuri sana  mwanae Munyigumba, Mukwava aliyekuwa na umri wa miaka 23 wakati huo alikuwa tayari askari jemadari aliyekamilika, hivyo alikusanya askari na kutengeneza jeshi imara na kuelekea Image. Alijipanga vizuri na kuwazunguka Wangoni, kisha kuwashambulia kutoka mgongoni, Wangoni hawakuwa na namna ila kujiokoa, wakakimbia wakirudi kwao kupitia Lulanga, kule wakashambuliwa tena na Mutengela aliyekuwa mutwa wa Wakinamanga, tena yeye akawafukuza mpaka ndani ya nchi yao.  Wangoni hawakuamini kipigo hicho kwani katika vita zao zote walikuwa na kawaida moja tu kushinda vita. Walirudi kwao na kutulia kwa muda mrefu.

Kiasi cha mwaka mmoja baada ya mapambano hayo na Wangoni, Mutwa Munyigumba akafariki.

Kikaanza kipindi chenye mashaka sana, kwani wakati wa uhai wake Munyigumba alikuwa na msaidizi wake ambaye alikuwa pia mkwewe. Mtu huyu aliyekuwa pande la mtu na ambaye Munyigumba alimpa mamlaka makubwa, hivyo  alikuwa akihofiwa sana. Huyu bwana alikuwa wa ukoo wa Lunyungu, kwa majina alikuwa akiitwa Mwanakimamule au Pokavilonga. Mwenyewe alijiita wa ukoo wa Mwamubambe au wengine huita Mwambambe, jina alilolitoa kutoka jina la baba yake Mubambe.
Wakina pia Muyinga walimhofu sana mtu huyu na hofu yao haikuwa bure hakuwa mtu wa kawaida. Kutokana na hofu hiyo akina Muyinga wakaacha kumtawaza Mkwava kwa vile waliona bado kijana mdogo ambaye walihisi asingeweza kushindana na hila za Mwamubambe. Hivyo wakamteua ndugu yake aliyeitwa Mhalwike awe Mutwa.  Haikuchukua muda mrefu woga wa kina Muyinga ukadhihirika,  Mwamubambe alimuua Muhalwike na kumtawaza ndugu yake aliyeitwa Mwamuhenga. Huyu alikuwa mtawala jina tu kwani mtawala rasmi alikuwa Mwamubambe.
Hapo ikalazimika Mkwawa aikimbie nchi yake mwenyewe.

Tuesday, August 16, 2022

KISA CHA MUYOVELA KUKIMBILIA UGOGONI


Mihwela alipofariki, wale watoto wake  wawili wa kiume, Muyoviligombo au Myovela na Mwengamagoha, wakaamua kugawana nchi ya baba yao na kumpa binamu yao Munyigumba mali. Munyigumba akakataa na kudai apewe eneo la kutawala. Ndugu zake wakampuuza, na yeye akajifanya kama pia hana shida kumbe alianza kupanga mipango ya chinichini ya kupata alichokuwa anakitaka. Kwanza akaanza kuonyesha ukaribu mkubwa na  Mwengamagoha, kwa kuwa huyu alikuwa na hasira za harakaharaka akawa anamtumia kumchokoza kaka yake kwa hila moja au nyingine. Alipoona hila zake hazimtii hasira Myovela akaona abadili utaratibu, siku moja akamualika Myovela amtembelee Ng’uluhe, baadhi ya Wadongwe mashuhuri waliompenda Myovela akina Luvanga, Mulala, Nyakunga, wakamkataza asiende, tena wakamshauri kuwa ni heri aondoke na watu wake na mifugo yake na kuhamia nchi nyingine, kwani ni lazima Munyigumba takuja kupiga. Myovela na watu wake wakaondoka na kutembea mpaka Izazi wakataka kuweka masikani pale, lakini wakapata habari kuwa Munyigumba na jeshi lake wanawasaka, wakalazimika kuondoka na kuvuka mto Lyambangali mpaka Ilolo, kule kulikuwa na mtawala aliyeitwa Msane, Msane aliwakaribisha Myovela na watu wake, lakini Myovela hakukaa sana hakutaka wenyeji wake aliyemkaribisha vizuri aje apewe adhabu na Munyigumba kwa ajili yake. Aliendelea na safri hadi Nyamasitu, akapumzika na watu wake pale, lakini tena akaambiwa kuwa adui bado anamfuata. Myovela aliendelea na msafara mpaka jirani na ulipo mji wa Kibakwe siku hizi, eneo hilo lilikuwa likitawaliwa na Mdemu mtoto wa Manyile, huyu aliposikia jeshi la Wadongwe lililoongozwa na Myovela linamkaribia hakungoja, aliondoka na watu wake na kukimbilia Ugogo. Wanyandewela wa Mudemu walikuwa wana haki ya kuliogopa jeshi la Myovela maana habari za ukali wa Wadongwe zilifahamika sana.  Lakini  bahati haikuwa ya Mudemu, jeshi lake  lilipofika karibu na ilipo Mvumi,  likashambuliwa na Wagogo na Wamasai na kuangamizwa karibu lote, mahala pale pakaitwa Makang’wa, na wajukuu wa waliosalimika katika maangamizi yale mpaka leo hutumia kiapo cha Kumakang’wa kukumbuka ilikolala mizimu yao.
Muyovela alitulia kwa miaka kadhaa katika makao yake mapya, watu wake wakaanza kusambaa na kuishi bila woga kwani wenyeji waliwaogopa sana hawa wageni, waliendelea kuishi na hadi leo wakazi wa maeneo ya Wota waliotokana na msafara huo wa Myovela hujitambua kuwa ni Wahehe na hufuata mila zote za Kihehe.

Myovela aliondoka tena na watu wake wengine na kuelekea  Nondwa iliyokuwa katika himaya ya Ugogo, kwenye tambarare  kusini mwa bwawa la Kinyambwa, aliafikiana na wenyeji kule na akaishi kwa raha ukiachia mapigano ya hapa na pale na Wamasai aidha kwa kuwaibia ng’ombe au walipokuwa wakiibiwa ng’ombe.

Huku nyuma Mnyigumba na Mwengamagoha wakaamua kugawana nchi. Munyigumba akamshauri Mwengamagoha akajenge ikulu yake Nzihi, wakati yeye akaendaa kujenga ikulu yake Lungemba. Myovela alipopata habari ya kinachoendelea akatuma ujumbe kwa nduguye na kumsihi  akajenge ikulu yake Luhota kwani ndiko ilikokuwa chanzo cha himaya ya baba yake, angekuwa kati ya watu wake,  Nzihi ilikuwa ni kama ugenini. Mwengamagoha  akampuuza kaka yake. Na kuanza kujenga ikulu yake Nzihi. Munyigumba akatuma kikosi cha siri kikaenda kushambulia Nzihi, mke na watoto wote wa Mwengamagoha waliuwawa, na yeye alinusurika tu  kwa kujificha kwenye shimo lililokuwa linachimbwa udongo wa kujengea ikulu yake.

Mwengamagoha alipopata nafasi akatoroka na kuelekea alikokuwa kaka yake Ugogoni. Alipofika kaka yake alimpokea vizuri lakini alimkaripia sana kwa upumbavu wake wa kutokutambua kuwa Munyigumba alikuwa adui yao wote. Mwengamagoha aliyapokea makaripio ya kaka yake vizuri lakini wake na watoto wa Muyovela waliendelea kumtania na hata kumtungia nyimbo za kejeli, hakuweza kuvumilia akahama na kuelekea Usangu na baadae Ukosikamba  hatimae akafia Udonya akiwa hana nchi,

 

 

 

 

 

 

Friday, August 12, 2022

UNAJUA JINSI MUNYIGUMBA ALIVYOPATA JINA LAKE?

 


Mtoto wa kwanza wa Kilonge na Sekindole aliitwa Mugavanalupembe. Huyu ndie aliyerithi utawala wa Ng’uluhe, lakini hakutawala muda mrefu kwani aliuwawa na Muhingile Mwangwenga kwenye ugomvi wakati wa kunywa pombe. Muhingile alitoroka na kujificha kwa muda mrefu lakini alipojitokeza kitu cha ajabu, hakuna aliyemkamata au kumhukumu.
Mtoto wa pili wa Kilonge na Sekindole aliitwa Binini. Jina hili halikupendwa sana na  kwani lilikuwa likitambulisha umbo la mtoto huyu kuwa alikuwa na aina ya kibyongo. Alikuja kujulikana zaidi kwa jina la Munyigumba au Mugohang’amwa yaani Mkuki unakamulika, kwani kwa kutumia mikuki alipata mali kama mtu mwenye ng’ombe anavyokamua maziwa.

Wakati kaka yake Mugavanalupembe alipokuwa akitawala Ng’uluhe, Binini alipelekwa kukulia kwa mjomba wake shujaa Mihwela. Mihwela alikuwa binamu ya Sekindole mama wa Binini hivyo alikuwa mjomba wake. Huko akajifunza mbinu za vita na utawala. Akaanza nae kuwa na hamu ya kutawala.

Mihwela alikuwa na watoto wa kiume wawili, Muyoveligombo na Mwengamagoha. Huyu Muyoveligombo alikuwa mwanamuziki  aliyependa kupiga ‘ligombo’, aina ya gitaa la asili ya Uheheni, na pia kuimba. Na ndivyo alivyopata jina la Muyoveligombo ambalo baadae likafupishwa na kuwa Muyovela. 

Huyu Mwengamagoha alikuwa mtu wa kukasirika kasirika na  mwenye jeuri. Mihwela aliwahi kumkemea mara kadhaa mwanae huyu kutokana kuwa na jeuri. Kuna wakati aliwateka watu wawili, Mwisaka mmoja na Mwachusi mmoja, akawatesa sana na hatimae akamuua yule Mwisaka, Mihwela alikasirika sana na kumwambia mwanae kuwa anafumua misingi ya kuunganisha  koo mbalimbali na hivyo kuwa na nguvu za pamoja na pia kwa kuwa watu hawa walikuwa mashujaa katika mapambano kadhaa aliyofanya Mihwela. Lakini Mihwela alifahamu pia kuwa Binini ndie aliyekuwa akichochea hayo ili apunguze nguvu za kumpinga wakati atakapoanza mbinu zake za kuchukua utawala.
Mihwela alimwambia mwanae Myovela kuwa apigane na Mwengamagoha na Binini wakati akiwa bado na uwezo kwani alikuwa ameota ndoto kuwa  Muyovela alikimbilia nchi ya mbali, kavu na yenye joto nje ya Uhehe. Lakini wajukuu zake watarudi Uhehe ila wakati huo watu weupe watakuwa wamefika na kuchimba ardhi na kujenga vichuguu vikubwa vyeupe. Myovela alikuwa mtu wa amani hakutaka kupigana na ndugu zake, hivyo akapuuza maagizo ya baba yake, lakini miaka mingi baadae ndoto ya baba yake ilitokea kama alivyoiota, kama tutakavyoona hapo baadae.

Wakati Binini yupo Luhota akaoa mke kutoka ukoo wa mwa Ngimba wa Ilole. Akina NGimba asili yao ni Hamitiki hivyo mpaka leo hutokeza wajukuu warefu wenye vidole virefu, masalia ya DNA ya Wahamitiki..
Binini alipoitwa kweda kwenye msiba wa kaka yake Mugavanalupembe alikataa na kusema kuwa angetaka kwanza aende kuwapiga Wasangu, kwani aliamini baada ya hapo angerudi na mali nyingi na utukufu hivyo kuchukua kirahisi himaya iliyokuwa ya kaka yake. Alikusanya vikosi vya Wadongwe wa Luhota na akapata vikosi vingine kutoka kwao Ng’uluhe, na askari wote walitakiwa kukutana Lungemba, Binini mwenyewe alipofika Lungemba,  ndugu zake akina Kindole wakamuongezea askari, akawa na jeshi kubwa. Aliingia Usangu na kuwashambulia ghafla Wasangu na kuteka mali nyingi na wanawake. Binini mwenyewe akamuua kiongozi wa Wasangu aliyeitwa Munyigumba na akatwaa jina lake kama kumbukumbu ya vita hiyo. Baada ya ushindi huo akaanza kurudi Ng’uluhe akapitia Mufindi iliyokuwa chini ya binamu yake Musambila Mwamdemu mtoto wa Chawala. Huyu alitawala Ifwagi, Mufindi na hata sehemu za Malangali. Munyigumba alipokelewa kwa shangwe na ngoma, lakini katikati ya sherehe akamchoma mkuki mwenyeji wake na kumuua na kujitangaza mtawala.  Na nia yake ya kupitia Mufindi ikadhihirika kwani alikuwa kapita ili kulipa kisasi kwani Musambila hakumpa askari wakati anaenda kupigana na Wasangu, na pia kuanza kutimiza ndoto yake ya kutawala eneo kubwa.

 

Thursday, August 11, 2022

MIHWELA MUHEHE ANASTAHILI KUITWA SHUJAA WA TAIFA

Mihwela azuia utumwa

Katika mfululizo wa historia hii nimeongelea mambo makubwa aliyofanya Mihwela mjukuu wa Chota. Lakini  mtu huyu bahati mbaya jina lake huwa halitajwi sana katika watu muhimu Uheheni, licha ya makubwa aliyowafanyia watu wa Uheheni. Tuliona jinsi alivyokuwa wa kwanza kuanza kuanzisha mpangilio wa mafunzo ya kijeshi kwa askari na alivyoweza kushinda vita kadhaa kiasi cha koo na kabila ndogondogo mbalimbali kuanza kumuita awatawale ili wapate ulinzi wa askari wake. Leo tutazungumzia jambo moja kubwa sana alilolifanywa Mihwela.

Kati ya mwaka 1820 na 1830, Waarabu walianza kuingia bara kutoka pwani na kuanza kuteka watu ili wakauzwe na kuwa watumwa kwenye mashamba ya Karafuu huko Unguja.
Kikosi kimoja cha waarabu kikaingia sehemu za Pawaga na kuteka watu wengi na kuwaweka katika makambi tayari kwa safari ya kwenda pwani kuuzwa Pwani, baadhi ya watu walioweza kutoroka walikimbia na kwenda kumtaarifu Mihwela ambaye alikusanya jeshi lake na kuweza kusafiri na hatimae kufika usiku karibu na kambi hiyo ya Waarabu. Jeshi la Mihwela lilijipanga na kuizunguka kambi ile, mapema alfajiri jeshi lile lilifanya mashambulizi na kuteketeza Waarabu wote, wakamuachia mmoja tu aliambiwa akatoe taarifa kuwa Wadongwe wamepiga marufuku biashara ya utumwa eneo lile.
Na tangu wakati ule biashara ya utumwa uheheni ilikufa, Wahehe wachache walioingia utumwani ni wale waliorubuniwa kuondoka mipaka ya Uheheni na huko kujikuta wakitekwa na kuuzwa. Wanyamwezi wanasemekana  walikuwa maarufu kwa ujanja huu wa kuwa rubuni Wahehe kuondoka katika usalama wa nchi yao.
 Waarabu walikuja baadae kufanya biashara Uheheni lakini si biashara ya utumwa, Ila ieleweke kuwa Wahehe wenyewe walikuwa na watumwa waliofanya kazi mashambani, majumbani na kwenye shughuli za uchungaji.
Kiukweli kwa hili Mihwela alistahili kuwa shujaa si wa Uheheh tu bali wa nchi yetu ya Tanzania.
Kama mnakumbuka babu yake Mihwela, Chota,  alimuua Mnyaluhwao siku ya kwanza ya kukutana nae hivyo kuzuia kuja kupingwa baadae, na Mihwela alitumia akili hiyohiyo kuzuia upinzani pale alipohisi unaweza kuja kutokea, himaya yake ikaanza kukua.
Kama tulivyoona awali alimaliza uasi wa Wasawila kwa kuwapiga wasaidizi wao Wasangu, akawaweka chini ya utawala wake Vanyandevelwa waliokuwa chini ya mtawala wao Mdemu mtoto wa Manyile ambaye baada ya mapigano kadhaa alikimbilia Wota.

Wahehe 

Jeshi la Mihwela lilikuwa na vikosi

Jeshi la Mihwela lilikuwa na vikosi vyenye watu 200 kila kikosi. Taratibu hii ya kuwa na askari 200 kila kikosi inaonekana ilikuwa ya kawaida katika Afrika, kwani miaka mingi kabla ya hapo Vanyangologo walipoingia Uheheni walikuwa wakitembea kwa vikosi vya watu mia mbili mia mbili, hata Shaka wa Wazulu jeshi lake pia lilikuwa na mfumo huo, na hata Mkwawa baadae alikuwa na jeshi lenye vikosi vya idadi hiyohiyo.

Wadongwe walipenda sana mtindo wa kuwazunguka adui usiku na kisha kuwashambulia alfajiri mapema, kila askari wa Wadongwe alikuwa na ngao iliyotengenezwa kwa ngozi ya ng’ombe iliyokuwa na urefu wa kwenda juu kimo cha askari na upana wake kiasi cha upana wa binadamu. Pia kila askari alikuwa na mikuki miwili, mmoja mwembamba alioutupa na mwingine wenye bapa nene, ulioitwa lisala, ulitumika kuchoma adui na kuchomoa kama kisu.
Mdongwe alikuwa akipigana na adui mwenye mkuki alisimamisha ngao yake, na kama ni adui waliotumia visu na mapanga kama Wahuma ngao aliishika kwa kuilaza upande kusudi kisu kisichane ngao ile kutoka juu mpaka chini. Kuna hadithi kuwa Wahehe walianza kutumia ngao baada ya kupigana na Wangoni, hii si kweli Wategeta walianza kutumia ngao baada ya mapigano yao na Wahumma na kuona Wahumma walivyofaidika na kinga hiyo

Tuesday, August 9, 2022

KABLA YA KUWA KABILA MOJA, UHEHE ILIKUWA NA VIKABILA MBALIMBALI KARIBU THELATHINI

 

Wahehe

Kabla ya Wahehe kuwa kabila moja kama linavyojulikana sasa kulikuwa na vikabila vidogovidogo karibu 30, na kila kimoja kikiwa chini ya ukoo kama ndio watawala. Tuanze na ukoo ulioitwa VaMudemu, .hawa walitawala katikati ya Ubena na Ulanga, maeneo kama  Ifwagi mpaka ilipo Malangali leo yalikuwa maeneo chini ya ya VaMudemu.  Ukoo huu unasemekana ulianzishwa na muwindaji  aliyeitwa Bugoma aliyetoka Ndweve iliyoko kwenye bonde la Ulanga. Mtiririko  wa watawala hao ulianza na Bugoma, akafuata Silonga, akafuata Nolelo, akafuata Mudemu, akaja Msambila, akafuata Mtamile na kumalizikia na Jumbe Hassan.
Kulikuwa na ukoo mwingione wenye jina la VaMudemu hawa ni wa Ndevelwa maeneo ya Isimani, hawa walikuwa ni ukoo tofauti na nilioutaja hapo awali.
Utawala mwingine Uheheni ulikuwa ni wa Ukalinga, huu ulikuweko kwenye milima ya Udzungwa. Kuna hadithi za mapokeo kuwa machifu hawa  wa Kalinga walitoka Unyakyusa, na ndio maana kuna Wanyakyusa wengi tu ni wa ukoo wa Mwakalinga, lakini pia kuna ile historia kuwa Wanyakyusa walitokana na ukoo wa Chusi  kama nilivyoeleza katika makala moja hapo nyuma.
Kuna akina Mwakalinga wengine wanasema chanzo cha ukoo wao ni Mufwimi Mwakalinga,  aliyefika Kisanga katika nchi ya Ukalinga na akampa mimba Sekikungile, na akakimbia na kumuacha binti huyo mja mzito. Sekikungile akamzaa Mupogole aliyekuja kutawala eneo la Ukalinga lililokuwa likikaliwa na Vadzungwa ambao hawakuwa na mtawala.
Mlolongo wa utawala huo ulikuwa hivi, kulikuwa na Mpogole aliemuoa Sekatefu, akafuata Lubida aliyemuoa Sepulamu, akaja  Mumehwa aliyeoa  Sekindole, akafuata Makanya aliyemuoa Semugele, akarithi Mugabe aliyemuoa  SeKindole, akarithi Mwanasindava aliyemuoa Semudalingwa, akafuatia Chotisamba aliyekuja kumzaa Hamisi aliyekuja kuwa sub chief wa mwisho  Ukalinga. Kuna kitu hapa cha kujihadhari, hadithi ya muwindaji kufika mahali  na kumpa mimba mtoto wa Chifu huwa inajirudia rudia katika simulizi nyingi za Uheheni, hivyo ni ya kuichukua kwa tahadhari kwa vile ni mapokeo. Lakini ukweli ni kuwa na kulikuwa na Wakalinga wengi katika eneo lililoitwa Ukalinga. Hii ilikuwa ni eneo mashariki mwa Mdabulo. Hivyo nyakati za mwanzo za utawala wa Muyugumba, Vakalinga nao walikuwa na utawala wao, na walikuwa wanaheshimika kiasi hata cha kufika Lugemba na kuoa akina Sekindole waliokuwa wa koo za kitawala.
Kulikuwa na kabila la Vategeta, hawa walikuwa na kiongozi aliyeitwa Nyembe au Nyembeke, Vategeta wanasemekana waliishi maeneo jirani na Ilula. Uzazi wao ni pamoja na wakina  Kihwaganise.

Ngoja nizitaje baadhi ya tawala ndogo ndogo na viongozi wao zilizokuweko kabla ya Uhehe kuwa moja;

 

1.       Igavilo, mtawala Kindole

 

2.       Savila mtawala Mandili

 

3.       Hafiwa mtawala Lyelu

 

4.       Nyandevelwa mtawala Mudemu

 

5.       Dongwe mtawala Mudung’u

 

6.       Nyimage mtawala Maginga

 

7.       Nyilambo mtawala Kitalika

 

8.       Nyilole mtawala Kihwaganise

 

9.       Tegeta mtawala Nyembe

 

10.   Fwagi mtawala Mudemu

 

11.   Ukalinga mtwala Kalinga

 

12.   Chalamila mtawala Chalamila

 

13.   Sagala mtawala Mukwando

 

14.   Sagala mtawala Mwigombe

 

15.   Nyaganilwa mtawala Mugovano

 

16.   Dzungwa mtawala Kahemela

 

17.   Dzungwa mtawala Njole

 

18.   Sagala mtawala Lwafu

 

19.   Sagala mtawala Mulandali

 

20.   Sagala mtawala Wutalo

 

21.   Dekwa mtawala Muhanga

 

22.   Dene mtawala Mulefi

 

23.   Nyamudenye mtawala  Mandongo

 

24.   Nyamugovelo (Sagala) mtawala Mutalula

 

25.   Nyang’uluhe mtawala Mududa

 

26.   Ilongo mtawala Mduda

 

27.   Ilongo mtawala Lukungu

 

28.   Kinamuyinga mtawala Muyinga


STAT COUNTER