![]() |
Migagi |
Leo tunaendelea na sehemu ya 11 ya simulizi ya historia ya
Wahehe. Nitashukuru sana kama ukiwa mmoja wa atakae kuwa anafuatilia maandiko haya kwa kuwa mmoja wa followers na ikiwezekana kutoa maoni yako kuhusu unachojua kuhusu historia ya Wahehe ili tuboreshe historia hii.
Katika maelezo niliyoyatoa katika awali nilielezea mkasa
wa Kindole na nduguye Chota kugombania kutawala Rugemba na hatimae Chota
kuhamia Iwawa ambako pamoja na kukaribishwa kwa ukarimu mwingi aliishia
kumchoma mkuki na kumuua mwenyeji wake ambaye alikuwa tayari kumuachia utawala.
Sehemu iliyokuja kutawaliwa na Chota iliitwa Udongwe. Jina la Udongwe
lilitokana na jina la babu yake Mnyaluwaho, akiyefahamika kama Mkilwa Mudongwe. Munyaluwaho ndie
aliyekuwa mtawala aliyeuwawa na Chota, sasa kutokana na jina la babu yake, ni
wazi asili yao ilikuwa Kilwa. Wajukuu wa Wadongwe wamekuwa wakijitapa kuwa wao
ndio Wahehe wa asili, lakini hili lina utata kwani wengi wao walikuwa wa asili
ya Wahumya (Wahamitic) ambao hawakuwa
Wabantu. Kuna wadongwe wengine asili yao Vakilwa yaani waliotoka Kilwa, wengine
asili yao Vanyalyagi, wengine Vanyamahuvi, kuna Vanyandembwe ( hawa walikuwa
wakidai kuwa asili ya ukoo wao ni Tembo- Ndembwe).
Lakini ni ukweli kuwa Wadongwe walistahili kuitwa kiini
cha kuanzishwa kwa kabila la Wahehe. Mtu wa awali kabisa katika kujenga misingi
ya Uheheni aliitwa Mihwela alikuwa mjukuu wa Chota. Miwhela alikuwa
akijulikana kwa majina tofauti matatu. Aliitwa Mihwela kwakuwa alipokuwa mtoto mchanga nchi ya
Udongwe ilibarikia kuwa na mvua nyingi za usiku kucha, jina lake la pili lilikuwa la Lwangwi lwa ndembwe,hii ilikuwa kwa sababu ya sauti yake kubwa iliyofika
mbali alipocheka au kuongea,hivyo tafsiri ya jina lake ni kicheko cha tembo, na mwisho alijulikana kwa jina la Gingilifwili, alikuwa anafuga nywele zake nyingi na
kuzifunga kisogoni!!!.
Mihwela ndie alikuwa kiongozi wa kwanza kuanza kuwakusanya
askari na kuwafundisha maarifa na ujanja wa vita, jambo lililofanya Udongwe isihinde vita
nyingi.
Hebu tuangalie mambo mengine makubwa aliyoyafanya Miwhela. Wahafiwa na
Vanyamahuvi walikuwa wakiishi katika sehemu ya makutano ya mito Lyambangali
na Luvaha, hawakuwa na amani kwa kuwa jirani zao Wahuma walikuwa mara kwa mara
wanawashambulia. Watu hawa wakamuomba Mihwela aje kuwasaidia kumukomesha adui
yao huyu. Jeshi la Mihwela lilikuja na
kuwashambulia Wahuma na kuwafukuza mpaka ng’ambo ya mto Kizigo, na pia wakanyang’anywa mifugo yao
yote, tangu wakati ule Wahumma hawakuvuka tena Kizigo na Lyambangali kusumbua
Uheheni. Koo mbalimbali zilikubali kumkaribisha Mihwela awatawale kwani hilo
lilihakikisha amani na usalama wao toka kwa maadui.
Kuna wakati Wasangu waliingia na kuanza kuenea sehemu za
Uhehe, waliingia kupitia Ilongo na kukaribishwa na Wasawila ambao walikuwa na
ndoto za kumpinga Miwhela. Mihwela alishuku kuwa Wasangu wataingiliwa Uhafiwa
ili kufika Udongwe kumshambulia. Kwanza akakusanya mifugo yote, ilia dui
watakapofika wakose chakula, na kweli kama alivyotabiri Wasangu walipoingia uheheni wakaweka
kambi mahala palipoitwa Ipagala, katikati ya Tosamaganga na Kalenga, mahala
hapo palikuwa na majani ya matete mengi, njaa zilipowazidia Wasangu walianza kuyatafuna matete
kama miwa. Mihwela aliizunguka kambi ya Wasangu na kuwavamia, Wasangu wengi
walikufa pale, waliotekwa wakafanywa watumwa na wachache sana waliweza kutoroka
na kukimbia. Tangu ushindi ule bwawa la Kipagala likapewa jina la Idete
kukumbusha jinsi Wasangu walivyofyonza matete kwa njaa.
Nzuri xana
ReplyDelete