Pages

Sunday, August 7, 2022

MAELEZO YA ZIADA KUTOKA KWA MZEE MKOCHA KUHUSU MUFWIMI

 



Simulizi kuhusu Mufwimi ni simulizi nzuri na ina uhalisia fulani. Kwa mujibu wa akina Mwamuyinga wa Image, Avanyidaha wote walikuwa wawindaji; tofauti kubwa aliyoleta Mfwimi ilikuwa ushujaa wake wa kuua mnyama mkubwa, nyati, kwa mara ya kwanza na umaarufu wa Mfwimi wa pili, alikuja na chumvi, ambayo haikuwepo. Chumvi iliwawezesha jamii ile kula nyama nyingi. Na hasa ndiyo ilikuwa kivutio cha Mfwimi kwa Mwamduda na kwa muda mfupi watu hawa wakanawiri wakawa na nguvu. Hata huyu kijana aliyezaliwa na Se Mduda licha ya uwindaji, alikuwa mtundu na jeuri kupindukia.
Wakati wa utoto wangu mwanzoni mwa miaka ya 1950, kule kwetu Image kulikuwa na utaratibu wa kupimana nguvu kwa kupigana. Kila Kijiji kulikuwa na kijogoo wa ngumi, na kulikuwa na utaratibu wa kijogoo mmoja kutawala sehemu kubwa.
Wanaume walikuwa wanapigana bila kuwa wamegombana ila tu kuonyeshana ubabe. Mwamba mmoja alikuwa anasimama mbele ya watu kwenye mkusanyika hata kama ni kilabuni au hata kusanyiko la msibani, na kujitangaza kuwa anaeona kuwa ni kijogoo ajitokeze atetee heshima yake. Na kweli ilikuwa inatokea vurugu hapo mpaka kijogoo mmoja anapatikana.
Mimi nimeanza kwenda shule 1957, kijogoo wa Image wakati huo alikuwa Mwamadate. Akikasirika mishipa ya damu ya mikononi inatokeza mithili ya mkono wa mtoto mchanga. Ngumi yake ni kifo ikimpata mpinzani kichwani. Mwamba wa kujengea nyumba ya liking'a ya vyumba 3,  anatoka nao milimani amebeba kama unyasi wakati wenzie hata kuusimamisha huo mwamba, wanasaidiana watu kadhaa!
Kwa hiyo hata majeshi ya watu hawa walioshiba nyama, maziwa na ugali wa ulezi yalikuwa na afya kweli kweli. W
aandishi wengi wa historia ya Waafrika wanasahau kuelezea jinsi lishe bora ilivyowafanya watu wa zamani wawe wakakamavu walioweza kufanya mambo mengi ya ajabu.

No comments:

Post a Comment

STAT COUNTER