Wawindaji walithaminiwa sana Uheheni kwani walikuwa chanzo
cha mlo safi kwa jamii, hivyo sifa za Mufwimi zilitangulia kabla hajaingia
Ng’uluhe. Alipofika Nguluhe akapokelewa vizuri na Mduda aliyekuwa mtawala wa
eneo lile na kuwa mgeni rasmi wa Mutwa. Kila baada ya siku chache alikuwa akienda
kuwinda na kurudi na nyama nyingi, Wahehe huita nyama hizi za porini 'mbelembo'. Kuna wakati alikuwa akipotea
kwa siku kadhaa lakini hatimae akarudi tena, wenyeji wakampa jina la utani wakampa jina la Kayinguye.
Siku alizokuwa
ametulia aliwafurahisha wenyeji kwa kupiga chombo chake cha muziki unachoweza kulinganisha na gitaa kilichokuwa
kinaitwa Kimandinda, kilikuwa ni chombo cha muziki maarufu katika nchi ya Usagala wakati huo, nacho kama lilivyo gitaa kilikuwa na nyuzi sita.
Binti mkubwa wa Mduda alianza kumpenda Mufwimi, walianza
kushinda pamoja jioni mpaka usiku mzito wakati watu wengine wamekwenda kulala,
Mufwimi akimhadithia binti yule habari
zake mbalimbali za kusisimua za maisha
yake ya uwindaji. Haikuchukua muda mrefu ukaribu huo ukaanzisha mapenzi, siku moja Semduda,
yaani binti ya Mduda akamwambia Muyinga kuwa anajihisi ana mimba. Mufwimi
alijua kabisa kuwa kutakuwa na janga kubwa litakalomkumba pale Mtemi Mduda
atakapopata taarifa za mimba ya binti yake, hivyo Mufwimi akamwambia mpenzi wake kuwa kama atazaa mtoto
wa kiume amfundishe kuwa mwiko wa ukoo wa Mombe ni Funo. Kisha akatoroka
kuelekea kwao Ikombagulu.
Hakuna habari tena zinazosimuliwa kuhusu Mufwimi baada ya hapo, japo
kuna habari zingine husema akina Mduda walimtafuta na kumuua Mufwimi kwa kosa la kumpa mimba
dada yao bila ndoa,pengine hii ni hadithi tu kwani haijulikani kulikuwa na taratibu gani za kuishi mtu na mzazi mwenzie zama hizo,
Mduda alimpa mjukuu wake jina la Mwamuyinga, yaani mtoto wa yule
anayetangatanga. Mwamuyinga nae alikuwa na kuja kuwa muwindaji hodari kama baba
yake, na pia alikuwa na busara sana, inaonekana alikuja kuwa kipenzi cha babu yake, hivyo alikuja kurithi sehemu ya utawala wa
Babu yake, baada ya kifo cha Mduda.
Kuna hadithi za mapokeo kuhusu watawala waliokuja kumrithi
Muyinga huyu wa kwanza, lakini nyingine ni wazi ni za kubuni, na pengine nyingine
zimebadilika kutoka na kuwa zimekuwa zikirithiwa kwa kuhadithiana. Kilicho wazi
ni kuwa kwa vyovyote Muyinga hakuweko kabla ya mwaka 1760, hivyo kutaja majina
mengi ya warithi wa Muyinga wa kwanza na kudai kuwa wengine walitawala mpaka
uzee sana kunakosa mashiko kutokana ma muda.
Huwa majina kama Kitova, Lalika, Mdegela, Kilonge hutajwa katika
orodha ya watawala warithi wa Muyinga, lakini kuna wenye kudhani kuwa Kitowa ni jina
jingine tu la Muyinga wa kwanza, na Lalika ni jina la mdogo wake Mdegela
aliyekuwa babu mzazi wa Mkwava. Kuna wanaosema Kitoa na Mdegela ni jina lamtu
huyohuyo mmoja, wengine husema Mdegela alikuwa mtoto wa Kilonge, na wengine
husema Kilonge alikuwa mtoto wa Mdegela, na huo ndio mchanganyiko wenyewe. Kwa
kuendeleza historia tukubali kuwa Kilonge alikuwa mtoto wa Mdegela.
Inasemekana kuwa akina Muyinga walikuwa wakioa katika ukoo
wa Mveyange, Kindole na Vanyamahuvi.
Mpango huu ulikuwa tofali moja katika ujenzi wa kabila moja la Wahehe..
Kilonge alimuoa binti mmoja wa Kindole, ukumbuke kuwa
Kindole alikuwa mtawala wa Lungemba baada ya msuguano na kaka yake Chota, hivyo baada
ya Kilonge kumuoa Sekindole, binti huyo alipewa na baba yake askari 200 wa
kumsindikiza na kumlinda na hatimae wawe walinzi wa sehemu aliyotawala Kilonge. Labda niongeze neno hapa, Wahehe walikuwa na utaratibu wa kuwa na vikosi vya askari mia mbili mia mbili. Baada ya kukabidhiwa jeshi hili na mkwewe, Kilonge akaanza kutamani kutawala
Nguluhe yote kama ilivyokuwa enzi za Mduda, hivyo akamtimua kaka yake aliyeitwa Manga, ambae akalazimika kukimbia na wafuasi
wake ambamo pia walikuweko Watemikwila.
Kundi hili lilikimbia mpaka nyanda za juu za Ubena, sehemu
ambayo sasa inaitwa Masagati. Jina hili lilitokana Mwarabu mmoja aliyeanzisha
shamba la miti ya mpira na kuamua kupaita mahala hapo Muscat akikumbuka nchi
aliyotoka, ugumu wa matamshi ya jina
hilo ukapafanya hapo paitwe MASAGATI. .
No comments:
Post a Comment