Pages

Thursday, August 4, 2022

WAHABESHI , WAZIGUA NA WAJUKUU ZAO WAHEHE

 


Kipindi kilekile ambacho Vanyangologo walikuwa wakitoka ilipo Kenya na kuelekea kusini hadi kufika Uheheni, Mhabeshi mmoja alianza safari kwa kutumia punda, safari yake ilikuwa  kuelekea kusini mwa Uhabeshi. Alishuka chini mpaka kufika Ukambani ambapo alipata mke wa Kikamba na kuzaa nae watoto wakiwemo wanaume watatu.
Hawa watoto walipofika umri wa utu uzima, nao wakaondoka kwao nakusafiri kuelekea kusini zaidi kama alivyofanya baba yao, hatimae wakaingia  nchi ya Uzigua ambako wakaoa na kisha kuendelea na safari kuelekea kusini zaidi wakifuata njia ile ile waliopita Vanyagologo miaka kadhaa nyuma,
Hatimae waliingia Usagala na kufanya makazi yao mahala palipoitwa Ikombagulu, kule kwenye michoro ya kale ya kwenye mapango. Hapo wakaanzisha ukoo uliokuja kuitwa Mombe. Kuna wanaosema jina hili linauhusiano na Mombo iliyoko karibu na Lushoto. Kuna Wazigua wengine walikuja kuwafuata baadae nao hatimae walikuja kuwa Wahehe ambao hujulikana kwa 'mwidikiso' wa Vanyamsigula.
Katika wale watoto watatu wa yule Mhabeshi aliyeoa Mkamba, akina Mombe hukumbuka  jina la mtoto mmoja tu nalo ni Mubunsugulo. Akina Mombe husisitiza kuwa Mubunsugulo alikuwa mweupe, pengine weupe uliotokana na muingiliano wa Wareno na Wahabeshi, miaka mingi nyuma. Kwenye mwaka 1520 Wahabeshi waliomba msaada wa Wareno katika vita ya kidini iliyokuwa inaendelea, kikosi cha askari 400 wa Kireno waliweka makazi yao kwa miaka kadhaa katika nchi ya Uhabeshi.
Inasemekana Mubunsugulo alikuwa na watoto watatu. Wa kwanza Nguluchawangi,  huyu pia aliitwa Manga na alihamia Masagati, wa pili alikuja itwa Mufwimi yaani muwinaji, na wa tatu ni Ngwila ambaye alikuja kurithi kwa baba yake utawala wa  nchi kutoka Ikombagulu hadi Ifakara. Taarifa hii hupingwa na wazee wengine ambao husema Manga alikuwa kaka yake Kilonge, babu yake Mkwava na Ngwila alikuwa Mkamba aliyekuwa binamu yake Mubunsugulo. Hata hivyo kundi la wajukuu wa Ngwila lilihamia iliko Pawaga siku hizi. Vanyamsigula wengine walikwenda kuishi Wota kaskazini mwa Lyambanngali na wengine walikuja kuhamia Ugogo wakiwa na makundi makubwa ya ng’ombe.
Kuna hadithi moja ya ajabu sana kuhusu hawa waliohamia Ugogo. Kiongozi wao alipata ugonjwa wa  ndui, hivyo watu wake wakamtenga na kuhama na kumuacha peke yake. Siku moja radi kubwa ilipiga na kuwatisha  ng’ombe ambao walikimbia na kurudi makazi yao ya zamani alikoachwa yule kiongozi mwenye ndui. Yule kiongozi mwenye ndui aliweza kuanza kuishi kwa kunywa maziwa na kumuomba mizimu ya kwao hadi akapona ndui. Baada ya mkasa huu wa ajabu, Wamasai waliokuwa wakiishi jirani na maeneo hayo walimchagua awe Laibon wao.na kumpa jina la Arheringisho maana yake Ng’ombe mweusi mwenye nyota nyeupe kichwani.
Hadithi hii inaeleza kwa sababu gani Wamasai wa Ugogoni hujitapa kuwa asili ya mkuu wao ni moja na ile ya Mkwawa.
Siku moja Mufwimi mtoto wa Mubunsugulo, aliondoka Ikombagulu  kwenda kuwinda, akapitia Usagala, akapanda milima ya Udzungwa na kutokea Ng’uluhe, nchi ya udongo mwekundu. Wakati huo Nguluhe ilikuwa inatawaliwa na Mduda, huyu alikuwa Msagala aliyetokana na wale watu weupe  waliofukuzwa na Vanyangologo kama nilivyohadithia huko nyuma. Asili yake hiyo inathibitishwa na mwiko wa ukoo huo iliyokuwa  boga lililoitwa lilangala, ambalo huwa na rangi nyekundu ya kung’aa inayokumbusha asili ya ngozi yao.
Hata jina la ukoo huu huitwa pia Ginga yaani fuga nywele, ikimaananisha watoto wao walikuwa wakikumbushwa kufuga nywele zao ambazo zilikuwa  kama za kizungu au za kiarabu. Watoto wa Mduda walioa katika koo za Mveyange na Wategeta, walizaliwa watoto shupavu ambao hawakukubali kutawaliwa, wakaja kuitwa Vatemikwila, pengine kutokana na swali walilopenda kuuliza mtu yoyote aliyejifanya mtawala, Mtemi kwiya? Maana yake  We Mtemi wa wapi?

 

 


No comments:

Post a Comment

STAT COUNTER