Pages

Monday, September 5, 2022

UHEHENI ILIKUWA MARUFUKU KUMWAGA DAMU YA NDUGU WA MUTWA


 Nchi ambayo sasa inaitwa Uhehe, awali ilikuwa na Vatwa wengi, (mmoja;Mutwa). Nisingependa kutumia neno Chief maana halitoshelezi kutafsiri neno Mutwa.
Kuanzia zama za Mihwela, wale Vatwa wa vikabila mbalimbali vilivyotekwa au vilivyokubali kutawaliwa na Mutwa, wakawa sasa wanaitwa Vansagila. Hii iliendelea mpaka hatimae Mutwa wa Uhehe akaja kuwa mmoja tu Mutwa Mukwava, lakini tufwatilie simulizi hii ili kujua Mkwava alifikiaje nafasi hiyo.

Vatwa waliheshimika mno Uheheni, mtoto wa kiume wa Mutwa aliitwa Mwaluka, wengi waliitwa Valuka. Mtoto wa kike wa Mutwa aliitwa Munumwehe. Mkwe wa Mutwa hasa yule aliyeoa binti wa Mutwa alitambulika kama  Mwanamutwa.

Mutwa alikuwa na salamu yake maalumu, alisalimiwa 'Ase Senga' nae alijibu 'Asee'.
Mwiko mkubwa wa ukoo wa Mutwa ni kumwaga damu ya ndugu. Kuna hadithi za ajabu sana kuhusu imani hii ambayo iliheshimiwa sana. Kuna hadithi moja ilimuhusu Mabohola mtoto wa Munsagila Ngawonalupembe aliyekuwa kiongozi wa jeshi la Vanyamwani kutoka Ubena,  wakati fulani Mkwawa na Mabohola walikuwa wakipigana na Wangoni, Mutwa Mukwawa akaona kuwa vita imekuwa kali mno bora akimbie  atoroke wakati wa usiku. Mabohola akamsihi asifanye hivyo, akamwambia akikimbia usiku, Wangoni wataelewa kuwa kaelemewa na watamfuata, lakini akifanya kama anarudi nyuma wakati wa mchana, adui wangejua anaenda kujipanga mahala pazuri zaidi hivyo adui angesita kumfuata. Wazo lile lilifanikiwa na Mkwava akaweza kurudi Kalenga salama. Lakini Mkwava alianza kuona kuwa Mabohola ana akili mno anaweza kuja kumpindua, na kuna wazee wengine husema kuwa kiutaratibu Mabohola alikuwa na haki sawa kiukoo kuweza kutawala Uheheni kama alivyokuwa nayo Mkwava wakati huo. Mkwava akaona Mabohola ni tishio na hakutakiwa aishi zaidi. Siku moja akamkaribisha Mabohola kwenye Ivaha yake Kalenga, askari wa Mabohola walimuonya kuwa ni hatari kwenda Kalenga.  Mabohola aliamua kwenda, na alipofika kalenga watu wanne waliokuwa wamepangwa wakamkamata na kumnyonga, hawakutumia mkuki ili wakwepe kipengele cha kumwaga damu ya ndugu wa Mutwa. Inasemekana Mkwava alipokuwa akiangalia ndugu yake akinyongwa alisema, 'Wutema wutalamu' yaani 'Ukuu ni mgumu'.

Wakati ule Mwamubambe alipoamua kumuua Muhalwike, aliyepewa Wutwa baada ya kifo cha Munyigumba, askari aliyepewa kazi ya kumchoma mkuki alikataa na kuamua kujiua kwa kujichoma mkuki mwenyewe kuliko kumwaga damu ya Mutwa. 

Hadithi nyingine ilihusu Mpangile , mdogo wake Mukwava, kwa sababu moja au nyingine aliwahi kuchoma mkuki na kuuwa ng'ombe 40 wa kaka yake , Mkwava alikasirika sana lakini hakuweza kumwaga damu ya ndugu yake, badala yake akamchukua mke wa Mpangile aliyekuwa mzuri kuliko wote na kumchuna ngozi ya uso.

Damu ya hawa ndugu wa Mutwa ilikuwa inathaminiwa kiasi cha kwamba hata vitani hawakuruhusiwa kuwa mstari wa mbele.
Hadithi nyingine ilihusu Merere. Munyigumba aliwahi kumuoza Mutwa Merere binti yake mmoja mzuri sana katika makubaliano yao ya kupata amani, bahati mbaya binti yule akapata ugonjwa wa ndui, na kupofoka macho. Merere akamrudisha yule binti Uheheni kwa Muyigumba, jambo hilo lilimuudhi sana Mutwa Muyigumba, akatuma jeshi lake kwenda kumpiga Merere, lakini pamoja na yote akatoa amri, 'Mugonage si senga, sa mulagela mutose migoha, uyo mwanangu' Yaani, tekeni ng'ombe lakini msijaribu kumtupia mikuki huyo ni mwanangu, kwani Merere alikwisha kuwa Mwanamutwa kwa kumuoa binti ya Muyigumba. Hivyo ndivyo ilivyothaminiwa damu ya Vatwa na ndugu zao.

STAT COUNTER