Mihwela
alipofariki, wale watoto wake wawili wa
kiume, Muyoviligombo au Myovela na Mwengamagoha, wakaamua kugawana nchi ya baba
yao na kumpa binamu yao Munyigumba mali. Munyigumba akakataa na kudai apewe
eneo la kutawala. Ndugu zake wakampuuza, na yeye akajifanya kama pia hana shida
kumbe alianza kupanga mipango ya chinichini ya kupata alichokuwa anakitaka.
Kwanza akaanza kuonyesha ukaribu mkubwa na
Mwengamagoha, kwa kuwa huyu alikuwa na hasira za harakaharaka akawa
anamtumia kumchokoza kaka yake kwa hila moja au nyingine. Alipoona hila zake
hazimtii hasira Myovela akaona abadili utaratibu, siku moja akamualika Myovela
amtembelee Ng’uluhe, baadhi ya Wadongwe mashuhuri waliompenda Myovela akina
Luvanga, Mulala, Nyakunga, wakamkataza asiende, tena wakamshauri kuwa ni heri
aondoke na watu wake na mifugo yake na kuhamia nchi nyingine, kwani ni lazima
Munyigumba takuja kupiga. Myovela na watu wake wakaondoka na kutembea mpaka
Izazi wakataka kuweka masikani pale, lakini wakapata habari kuwa Munyigumba na
jeshi lake wanawasaka, wakalazimika kuondoka na kuvuka mto Lyambangali mpaka
Ilolo, kule kulikuwa na mtawala aliyeitwa Msane, Msane aliwakaribisha Myovela
na watu wake, lakini Myovela hakukaa sana hakutaka wenyeji wake aliyemkaribisha
vizuri aje apewe adhabu na Munyigumba kwa ajili yake. Aliendelea na safri hadi
Nyamasitu, akapumzika na watu wake pale, lakini tena akaambiwa kuwa adui bado
anamfuata. Myovela aliendelea na msafara mpaka jirani na ulipo mji wa Kibakwe
siku hizi, eneo hilo lilikuwa likitawaliwa na Mdemu mtoto wa Manyile, huyu
aliposikia jeshi la Wadongwe lililoongozwa na Myovela linamkaribia hakungoja,
aliondoka na watu wake na kukimbilia Ugogo. Wanyandewela wa Mudemu walikuwa
wana haki ya kuliogopa jeshi la Myovela maana habari za ukali wa Wadongwe
zilifahamika sana. Lakini bahati haikuwa ya Mudemu, jeshi lake lilipofika karibu na ilipo Mvumi, likashambuliwa na Wagogo na Wamasai na
kuangamizwa karibu lote, mahala pale pakaitwa Makang’wa, na wajukuu wa
waliosalimika katika maangamizi yale mpaka leo hutumia kiapo cha Kumakang’wa
kukumbuka ilikolala mizimu yao.
Muyovela
alitulia kwa miaka kadhaa katika makao yake mapya, watu wake wakaanza kusambaa
na kuishi bila woga kwani wenyeji waliwaogopa sana hawa wageni, waliendelea
kuishi na hadi leo wakazi wa maeneo ya Wota waliotokana na msafara huo wa
Myovela hujitambua kuwa ni Wahehe na hufuata mila zote za Kihehe.
Myovela aliondoka tena na watu wake wengine na kuelekea Nondwa iliyokuwa katika himaya ya Ugogo, kwenye tambarare kusini mwa bwawa la Kinyambwa, aliafikiana na wenyeji kule na akaishi kwa raha ukiachia mapigano ya hapa na pale na Wamasai aidha kwa kuwaibia ng’ombe au walipokuwa wakiibiwa ng’ombe.
Huku nyuma Mnyigumba na Mwengamagoha wakaamua kugawana nchi. Munyigumba akamshauri Mwengamagoha akajenge ikulu yake Nzihi, wakati yeye akaendaa kujenga ikulu yake Lungemba. Myovela alipopata habari ya kinachoendelea akatuma ujumbe kwa nduguye na kumsihi akajenge ikulu yake Luhota kwani ndiko ilikokuwa chanzo cha himaya ya baba yake, angekuwa kati ya watu wake, Nzihi ilikuwa ni kama ugenini. Mwengamagoha akampuuza kaka yake. Na kuanza kujenga ikulu yake Nzihi. Munyigumba akatuma kikosi cha siri kikaenda kushambulia Nzihi, mke na watoto wote wa Mwengamagoha waliuwawa, na yeye alinusurika tu kwa kujificha kwenye shimo lililokuwa linachimbwa udongo wa kujengea ikulu yake.
Mwengamagoha
alipopata nafasi akatoroka na kuelekea alikokuwa kaka yake Ugogoni. Alipofika
kaka yake alimpokea vizuri lakini alimkaripia sana kwa upumbavu wake wa
kutokutambua kuwa Munyigumba alikuwa adui yao wote. Mwengamagoha aliyapokea
makaripio ya kaka yake vizuri lakini wake na watoto wa Muyovela waliendelea
kumtania na hata kumtungia nyimbo za kejeli, hakuweza kuvumilia akahama na
kuelekea Usangu na baadae Ukosikamba
hatimae akafia Udonya akiwa hana nchi,
No comments:
Post a Comment