Mtoto wa kwanza wa Kilonge na Sekindole aliitwa
Mugavanalupembe. Huyu ndie aliyerithi utawala wa Ng’uluhe, lakini hakutawala
muda mrefu kwani aliuwawa na Muhingile Mwangwenga kwenye ugomvi wakati wa
kunywa pombe. Muhingile alitoroka na kujificha kwa muda mrefu lakini
alipojitokeza kitu cha ajabu, hakuna aliyemkamata au kumhukumu.
Mtoto wa pili wa Kilonge na Sekindole aliitwa Binini. Jina
hili halikupendwa sana na kwani lilikuwa likitambulisha umbo la mtoto
huyu kuwa alikuwa na aina ya kibyongo. Alikuja kujulikana zaidi kwa jina la
Munyigumba au Mugohang’amwa yaani Mkuki unakamulika, kwani kwa kutumia mikuki
alipata mali kama mtu mwenye ng’ombe anavyokamua maziwa.
Wakati kaka yake Mugavanalupembe alipokuwa akitawala
Ng’uluhe, Binini alipelekwa kukulia kwa mjomba wake shujaa Mihwela. Mihwela
alikuwa binamu ya Sekindole mama wa Binini hivyo alikuwa mjomba wake. Huko
akajifunza mbinu za vita na utawala. Akaanza nae kuwa na hamu ya kutawala.
Mihwela alikuwa na watoto wa kiume wawili, Muyoveligombo na Mwengamagoha. Huyu Muyoveligombo alikuwa mwanamuziki aliyependa kupiga ‘ligombo’, aina ya gitaa la asili ya Uheheni, na pia kuimba. Na ndivyo alivyopata jina la Muyoveligombo ambalo baadae likafupishwa na kuwa Muyovela.
Huyu Mwengamagoha alikuwa mtu wa
kukasirika kasirika na mwenye jeuri.
Mihwela aliwahi kumkemea mara kadhaa mwanae huyu kutokana kuwa na jeuri. Kuna
wakati aliwateka watu wawili, Mwisaka mmoja na Mwachusi mmoja, akawatesa sana
na hatimae akamuua yule Mwisaka, Mihwela alikasirika sana na kumwambia mwanae
kuwa anafumua misingi ya kuunganisha koo
mbalimbali na hivyo kuwa na nguvu za pamoja na pia kwa kuwa watu hawa walikuwa
mashujaa katika mapambano kadhaa aliyofanya Mihwela. Lakini Mihwela alifahamu
pia kuwa Binini ndie aliyekuwa akichochea hayo ili apunguze nguvu za kumpinga
wakati atakapoanza mbinu zake za kuchukua utawala.
Mihwela alimwambia mwanae Myovela kuwa apigane na
Mwengamagoha na Binini wakati akiwa bado na uwezo kwani alikuwa ameota ndoto
kuwa Muyovela alikimbilia nchi ya mbali,
kavu na yenye joto nje ya Uhehe. Lakini wajukuu zake watarudi Uhehe ila wakati
huo watu weupe watakuwa wamefika na kuchimba ardhi na kujenga vichuguu vikubwa
vyeupe. Myovela alikuwa mtu wa amani hakutaka kupigana na ndugu zake, hivyo akapuuza maagizo ya baba yake, lakini miaka
mingi baadae ndoto ya baba yake ilitokea kama alivyoiota, kama tutakavyoona hapo
baadae.
Wakati Binini yupo Luhota akaoa mke kutoka ukoo wa mwa Ngimba wa Ilole. Akina NGimba asili yao ni Hamitiki hivyo mpaka leo hutokeza wajukuu
warefu wenye vidole virefu, masalia ya DNA ya Wahamitiki..
Binini alipoitwa kweda kwenye msiba wa kaka yake
Mugavanalupembe alikataa na kusema kuwa angetaka kwanza aende kuwapiga Wasangu,
kwani aliamini baada ya hapo angerudi na mali nyingi na utukufu hivyo kuchukua
kirahisi himaya iliyokuwa ya kaka yake. Alikusanya vikosi vya Wadongwe wa
Luhota na akapata vikosi vingine kutoka kwao Ng’uluhe, na askari wote walitakiwa kukutana
Lungemba, Binini mwenyewe alipofika Lungemba, ndugu zake akina Kindole wakamuongezea askari, akawa
na jeshi kubwa. Aliingia Usangu na kuwashambulia ghafla Wasangu na kuteka mali nyingi na
wanawake. Binini mwenyewe akamuua kiongozi wa Wasangu aliyeitwa Munyigumba na
akatwaa jina lake kama kumbukumbu ya vita hiyo. Baada ya ushindi huo akaanza
kurudi Ng’uluhe akapitia Mufindi iliyokuwa chini ya binamu yake Musambila
Mwamdemu mtoto wa Chawala. Huyu alitawala Ifwagi, Mufindi na hata sehemu za
Malangali. Munyigumba alipokelewa kwa shangwe na ngoma, lakini katikati ya
sherehe akamchoma mkuki mwenyeji wake na kumuua na kujitangaza mtawala. Na nia yake ya kupitia Mufindi ikadhihirika
kwani alikuwa kapita ili kulipa kisasi kwani Musambila hakumpa askari wakati
anaenda kupigana na Wasangu, na pia kuanza kutimiza ndoto yake ya kutawala eneo kubwa.
No comments:
Post a Comment