Mihwela azuia utumwa
Katika mfululizo wa historia hii nimeongelea mambo makubwa aliyofanya Mihwela mjukuu wa Chota. Lakini mtu huyu bahati mbaya jina lake huwa halitajwi sana katika watu muhimu Uheheni, licha ya makubwa aliyowafanyia watu wa Uheheni. Tuliona jinsi alivyokuwa wa kwanza kuanza kuanzisha mpangilio wa mafunzo ya kijeshi kwa askari na alivyoweza kushinda vita kadhaa kiasi cha koo na kabila ndogondogo mbalimbali kuanza kumuita awatawale ili wapate ulinzi wa askari wake. Leo tutazungumzia jambo moja kubwa sana alilolifanywa Mihwela.
Kati ya
mwaka 1820 na 1830, Waarabu walianza kuingia bara kutoka pwani na kuanza kuteka
watu ili wakauzwe na kuwa watumwa kwenye mashamba ya Karafuu huko Unguja.
Kikosi
kimoja cha waarabu kikaingia sehemu za Pawaga na kuteka watu wengi na kuwaweka
katika makambi tayari kwa safari ya kwenda pwani kuuzwa Pwani, baadhi ya
watu walioweza kutoroka walikimbia na kwenda kumtaarifu Mihwela ambaye alikusanya
jeshi lake na kuweza kusafiri na hatimae kufika usiku karibu na kambi hiyo ya
Waarabu. Jeshi la Mihwela lilijipanga na kuizunguka kambi ile, mapema alfajiri jeshi lile lilifanya mashambulizi na kuteketeza Waarabu wote, wakamuachia mmoja tu aliambiwa akatoe taarifa kuwa Wadongwe wamepiga marufuku biashara ya utumwa eneo lile.
Na tangu
wakati ule biashara ya utumwa uheheni ilikufa, Wahehe wachache walioingia
utumwani ni wale waliorubuniwa kuondoka mipaka ya Uheheni na huko kujikuta
wakitekwa na kuuzwa. Wanyamwezi wanasemekana
walikuwa maarufu kwa ujanja huu wa kuwa rubuni Wahehe kuondoka katika usalama wa nchi yao.
Waarabu walikuja baadae kufanya
biashara Uheheni lakini si biashara ya utumwa, Ila ieleweke kuwa Wahehe wenyewe walikuwa na
watumwa waliofanya kazi mashambani, majumbani na kwenye shughuli za uchungaji.
Kiukweli kwa
hili Mihwela alistahili kuwa shujaa si wa Uheheh tu bali wa nchi yetu ya
Tanzania.
Kama
mnakumbuka babu yake Mihwela, Chota, alimuua Mnyaluhwao siku ya kwanza ya kukutana nae
hivyo kuzuia kuja kupingwa baadae, na Mihwela alitumia akili hiyohiyo kuzuia
upinzani pale alipohisi unaweza kuja kutokea, himaya yake ikaanza kukua.
Kama
tulivyoona awali alimaliza uasi wa Wasawila kwa kuwapiga wasaidizi wao Wasangu,
akawaweka chini ya utawala wake Vanyandevelwa waliokuwa chini ya mtawala wao
Mdemu mtoto wa Manyile ambaye baada ya mapigano kadhaa alikimbilia Wota.
![]() |
Wahehe |
Jeshi la Mihwela lilikuwa na vikosi
Jeshi la Mihwela lilikuwa na vikosi vyenye watu 200 kila kikosi. Taratibu hii ya kuwa na askari 200 kila kikosi inaonekana ilikuwa ya kawaida katika Afrika, kwani miaka mingi kabla ya hapo Vanyangologo walipoingia Uheheni walikuwa wakitembea kwa vikosi vya watu mia mbili mia mbili, hata Shaka wa Wazulu jeshi lake pia lilikuwa na mfumo huo, na hata Mkwawa baadae alikuwa na jeshi lenye vikosi vya idadi hiyohiyo.Wadongwe
walipenda sana mtindo wa kuwazunguka adui usiku na kisha kuwashambulia alfajiri
mapema, kila askari wa Wadongwe alikuwa na ngao iliyotengenezwa kwa ngozi ya
ng’ombe iliyokuwa na urefu wa kwenda juu kimo cha askari na upana wake kiasi cha upana wa binadamu. Pia kila askari alikuwa na mikuki miwili, mmoja
mwembamba alioutupa na mwingine wenye bapa nene, ulioitwa lisala, ulitumika
kuchoma adui na kuchomoa kama kisu.
Mdongwe
alikuwa akipigana na adui mwenye mkuki alisimamisha ngao yake, na kama ni adui
waliotumia visu na mapanga kama Wahuma ngao aliishika kwa kuilaza upande kusudi
kisu kisichane ngao ile kutoka juu mpaka chini. Kuna hadithi kuwa
Wahehe walianza kutumia ngao baada ya kupigana na Wangoni, hii si kweli
Wategeta walianza kutumia ngao baada ya mapigano yao na Wahumma na kuona
Wahumma walivyofaidika na kinga hiyo
No comments:
Post a Comment