![]() |
Wahehe |
Kabla ya Wahehe kuwa kabila moja kama linavyojulikana sasa
kulikuwa na vikabila vidogovidogo karibu 30, na kila kimoja kikiwa chini ya
ukoo kama ndio watawala. Tuanze na ukoo ulioitwa VaMudemu, .hawa walitawala
katikati ya Ubena na Ulanga, maeneo kama
Ifwagi mpaka ilipo Malangali leo yalikuwa maeneo chini ya ya
VaMudemu. Ukoo huu unasemekana
ulianzishwa na muwindaji aliyeitwa
Bugoma aliyetoka Ndweve iliyoko kwenye bonde la Ulanga. Mtiririko wa watawala hao ulianza na Bugoma, akafuata
Silonga, akafuata Nolelo, akafuata Mudemu, akaja Msambila, akafuata Mtamile na
kumalizikia na Jumbe Hassan.
Kulikuwa na ukoo mwingione wenye jina la VaMudemu hawa ni wa Ndevelwa maeneo ya
Isimani, hawa walikuwa ni ukoo tofauti na nilioutaja hapo awali.
Utawala mwingine Uheheni ulikuwa ni wa Ukalinga, huu ulikuweko kwenye milima ya
Udzungwa. Kuna hadithi za mapokeo kuwa machifu hawa wa Kalinga walitoka Unyakyusa, na ndio maana
kuna Wanyakyusa wengi tu ni wa ukoo wa Mwakalinga, lakini pia kuna ile historia
kuwa Wanyakyusa walitokana na ukoo wa Chusi
kama nilivyoeleza katika makala moja hapo nyuma.
Kuna akina Mwakalinga wengine wanasema chanzo cha ukoo wao ni Mufwimi
Mwakalinga, aliyefika Kisanga katika
nchi ya Ukalinga na akampa mimba Sekikungile, na akakimbia na kumuacha binti
huyo mja mzito. Sekikungile akamzaa Mupogole aliyekuja kutawala eneo la
Ukalinga lililokuwa likikaliwa na Vadzungwa ambao hawakuwa na mtawala.
Mlolongo wa utawala huo ulikuwa hivi, kulikuwa na Mpogole aliemuoa Sekatefu,
akafuata Lubida aliyemuoa Sepulamu, akaja
Mumehwa aliyeoa Sekindole,
akafuata Makanya aliyemuoa Semugele, akarithi Mugabe aliyemuoa SeKindole, akarithi Mwanasindava aliyemuoa
Semudalingwa, akafuatia Chotisamba aliyekuja kumzaa Hamisi aliyekuja kuwa sub
chief wa mwisho Ukalinga. Kuna kitu hapa
cha kujihadhari, hadithi ya muwindaji kufika mahali na kumpa mimba mtoto wa Chifu huwa inajirudia
rudia katika simulizi nyingi za Uheheni, hivyo ni ya kuichukua kwa tahadhari
kwa vile ni mapokeo. Lakini ukweli ni kuwa na kulikuwa na Wakalinga wengi
katika eneo lililoitwa Ukalinga. Hii ilikuwa ni eneo mashariki mwa Mdabulo.
Hivyo nyakati za mwanzo za utawala wa Muyugumba, Vakalinga nao walikuwa na
utawala wao, na walikuwa wanaheshimika kiasi hata cha kufika Lugemba na kuoa
akina Sekindole waliokuwa wa koo za kitawala.
Kulikuwa na kabila la Vategeta, hawa walikuwa na kiongozi aliyeitwa Nyembe au
Nyembeke, Vategeta wanasemekana waliishi maeneo jirani na Ilula. Uzazi wao ni
pamoja na wakina Kihwaganise.
Ngoja nizitaje baadhi ya tawala ndogo ndogo na viongozi wao
zilizokuweko kabla ya Uhehe kuwa moja;
1. Igavilo,
mtawala Kindole
2. Savila
mtawala Mandili
3. Hafiwa
mtawala Lyelu
4. Nyandevelwa
mtawala Mudemu
5. Dongwe
mtawala Mudung’u
6. Nyimage
mtawala Maginga
7. Nyilambo
mtawala Kitalika
8. Nyilole
mtawala Kihwaganise
9. Tegeta
mtawala Nyembe
10. Fwagi mtawala
Mudemu
11. Ukalinga mtwala
Kalinga
12. Chalamila
mtawala Chalamila
13. Sagala mtawala
Mukwando
14. Sagala mtawala
Mwigombe
15. Nyaganilwa
mtawala Mugovano
16. Dzungwa mtawala
Kahemela
17. Dzungwa mtawala
Njole
18. Sagala mtawala
Lwafu
19. Sagala mtawala
Mulandali
20. Sagala mtawala
Wutalo
21. Dekwa mtawala
Muhanga
22. Dene mtawala
Mulefi
23. Nyamudenye
mtawala Mandongo
24. Nyamugovelo
(Sagala) mtawala Mutalula
25. Nyang’uluhe
mtawala Mududa
26. Ilongo mtawala
Mduda
27. Ilongo mtawala
Lukungu
28. Kinamuyinga
mtawala Muyinga