Pages

Monday, August 8, 2022

WASANGU WALITAFUNA MATETE KWA NJAA

 

Migagi

Leo tunaendelea na sehemu ya 11 ya simulizi ya historia ya Wahehe. Nitashukuru sana kama ukiwa mmoja wa atakae kuwa anafuatilia maandiko haya kwa kuwa mmoja wa followers na ikiwezekana kutoa maoni yako kuhusu unachojua kuhusu historia ya Wahehe ili tuboreshe historia hii.

Katika maelezo niliyoyatoa katika awali nilielezea mkasa wa Kindole na nduguye Chota kugombania kutawala Rugemba na hatimae Chota kuhamia Iwawa ambako pamoja na kukaribishwa kwa ukarimu mwingi aliishia kumchoma mkuki na kumuua mwenyeji wake ambaye alikuwa tayari kumuachia utawala. Sehemu iliyokuja kutawaliwa na Chota iliitwa Udongwe. Jina la Udongwe lilitokana na jina la babu yake Mnyaluwaho, akiyefahamika kama Mkilwa Mudongwe. Munyaluwaho ndie aliyekuwa mtawala aliyeuwawa na Chota, sasa kutokana na jina la babu yake, ni wazi asili yao ilikuwa Kilwa. Wajukuu wa Wadongwe wamekuwa wakijitapa kuwa wao ndio Wahehe wa asili, lakini hili lina utata kwani wengi wao walikuwa wa asili ya Wahumya (Wahamitic) ambao  hawakuwa Wabantu. Kuna wadongwe wengine asili yao Vakilwa yaani waliotoka Kilwa, wengine asili yao Vanyalyagi, wengine Vanyamahuvi, kuna Vanyandembwe ( hawa walikuwa wakidai kuwa asili ya ukoo wao ni Tembo- Ndembwe).
Lakini ni ukweli kuwa Wadongwe walistahili kuitwa kiini cha kuanzishwa kwa kabila la Wahehe. Mtu wa awali kabisa katika kujenga misingi ya Uheheni aliitwa Mihwela alikuwa mjukuu wa Chota. Miwhela alikuwa akijulikana kwa majina tofauti matatu. Aliitwa Mihwela kwakuwa alipokuwa mtoto mchanga nchi ya Udongwe ilibarikia kuwa na mvua nyingi za usiku kucha, jina lake la pili lilikuwa la Lwangwi lwa ndembwe,hii ilikuwa kwa sababu ya sauti yake kubwa iliyofika mbali alipocheka au kuongea,hivyo tafsiri ya jina lake ni kicheko cha tembo, na mwisho alijulikana kwa jina la Gingilifwili, alikuwa anafuga nywele zake nyingi na kuzifunga kisogoni!!!.
Mihwela ndie alikuwa kiongozi wa kwanza kuanza kuwakusanya askari na kuwafundisha maarifa na ujanja wa vita, jambo lililofanya Udongwe isihinde vita nyingi.
Hebu tuangalie mambo mengine makubwa aliyoyafanya Miwhela.  Wahafiwa na  Vanyamahuvi walikuwa wakiishi katika sehemu ya makutano ya mito Lyambangali na Luvaha, hawakuwa na amani kwa kuwa jirani zao Wahuma walikuwa mara kwa mara wanawashambulia. Watu hawa wakamuomba Mihwela aje kuwasaidia kumukomesha adui yao huyu.  Jeshi la Mihwela lilikuja na kuwashambulia Wahuma na kuwafukuza mpaka ng’ambo ya mto Kizigo, na pia wakanyang’anywa mifugo yao yote, tangu wakati ule Wahumma hawakuvuka tena Kizigo na Lyambangali kusumbua Uheheni. Koo mbalimbali zilikubali kumkaribisha Mihwela awatawale kwani hilo lilihakikisha amani na usalama wao toka kwa maadui.
Kuna wakati Wasangu waliingia na kuanza kuenea sehemu za Uhehe, waliingia kupitia Ilongo na kukaribishwa na Wasawila ambao walikuwa na ndoto za kumpinga Miwhela. Mihwela alishuku kuwa Wasangu wataingiliwa Uhafiwa ili kufika Udongwe kumshambulia. Kwanza akakusanya mifugo yote, ilia dui watakapofika wakose chakula, na kweli kama alivyotabiri Wasangu walipoingia uheheni wakaweka kambi mahala palipoitwa Ipagala, katikati ya Tosamaganga na Kalenga, mahala hapo palikuwa na majani ya  matete mengi, njaa zilipowazidia Wasangu walianza kuyatafuna matete kama miwa. Mihwela aliizunguka kambi ya Wasangu na kuwavamia, Wasangu wengi walikufa pale, waliotekwa wakafanywa watumwa na wachache sana waliweza kutoroka na kukimbia. Tangu ushindi ule bwawa la Kipagala likapewa jina la Idete kukumbusha jinsi Wasangu walivyofyonza matete kwa njaa.

Sunday, August 7, 2022

MAELEZO YA ZIADA KUTOKA KWA MZEE MKOCHA KUHUSU MUFWIMI

 



Simulizi kuhusu Mufwimi ni simulizi nzuri na ina uhalisia fulani. Kwa mujibu wa akina Mwamuyinga wa Image, Avanyidaha wote walikuwa wawindaji; tofauti kubwa aliyoleta Mfwimi ilikuwa ushujaa wake wa kuua mnyama mkubwa, nyati, kwa mara ya kwanza na umaarufu wa Mfwimi wa pili, alikuja na chumvi, ambayo haikuwepo. Chumvi iliwawezesha jamii ile kula nyama nyingi. Na hasa ndiyo ilikuwa kivutio cha Mfwimi kwa Mwamduda na kwa muda mfupi watu hawa wakanawiri wakawa na nguvu. Hata huyu kijana aliyezaliwa na Se Mduda licha ya uwindaji, alikuwa mtundu na jeuri kupindukia.
Wakati wa utoto wangu mwanzoni mwa miaka ya 1950, kule kwetu Image kulikuwa na utaratibu wa kupimana nguvu kwa kupigana. Kila Kijiji kulikuwa na kijogoo wa ngumi, na kulikuwa na utaratibu wa kijogoo mmoja kutawala sehemu kubwa.
Wanaume walikuwa wanapigana bila kuwa wamegombana ila tu kuonyeshana ubabe. Mwamba mmoja alikuwa anasimama mbele ya watu kwenye mkusanyika hata kama ni kilabuni au hata kusanyiko la msibani, na kujitangaza kuwa anaeona kuwa ni kijogoo ajitokeze atetee heshima yake. Na kweli ilikuwa inatokea vurugu hapo mpaka kijogoo mmoja anapatikana.
Mimi nimeanza kwenda shule 1957, kijogoo wa Image wakati huo alikuwa Mwamadate. Akikasirika mishipa ya damu ya mikononi inatokeza mithili ya mkono wa mtoto mchanga. Ngumi yake ni kifo ikimpata mpinzani kichwani. Mwamba wa kujengea nyumba ya liking'a ya vyumba 3,  anatoka nao milimani amebeba kama unyasi wakati wenzie hata kuusimamisha huo mwamba, wanasaidiana watu kadhaa!
Kwa hiyo hata majeshi ya watu hawa walioshiba nyama, maziwa na ugali wa ulezi yalikuwa na afya kweli kweli. W
aandishi wengi wa historia ya Waafrika wanasahau kuelezea jinsi lishe bora ilivyowafanya watu wa zamani wawe wakakamavu walioweza kufanya mambo mengi ya ajabu.

Saturday, August 6, 2022

MUFWIMI ALILAZIMIKA KUKIMBIA UHEHENI KUTOROKA KESI

 


Wawindaji walithaminiwa sana Uheheni kwani walikuwa chanzo cha mlo safi kwa jamii, hivyo sifa za Mufwimi zilitangulia kabla hajaingia Ng’uluhe. Alipofika Nguluhe akapokelewa vizuri na Mduda aliyekuwa mtawala wa eneo lile na kuwa mgeni rasmi wa Mutwa. Kila baada ya siku chache alikuwa akienda kuwinda na kurudi na nyama nyingi, Wahehe huita nyama hizi za porini  'mbelembo'. Kuna wakati alikuwa akipotea kwa siku kadhaa lakini hatimae akarudi tena, wenyeji wakampa jina la utani wakampa jina la Kayinguye.
Siku alizokuwa ametulia aliwafurahisha wenyeji kwa kupiga chombo chake cha muziki unachoweza kulinganisha na gitaa kilichokuwa kinaitwa Kimandinda, kilikuwa ni chombo cha muziki maarufu katika nchi ya Usagala wakati huo, nacho kama lilivyo gitaa kilikuwa na nyuzi sita.
Binti mkubwa wa Mduda alianza kumpenda Mufwimi, walianza kushinda pamoja jioni mpaka usiku mzito wakati watu wengine wamekwenda kulala, Mufwimi akimhadithia binti  yule habari zake  mbalimbali za kusisimua za maisha yake ya uwindaji. Haikuchukua muda mrefu ukaribu huo ukaanzisha mapenzi, siku moja Semduda, yaani binti ya Mduda akamwambia Muyinga kuwa anajihisi ana mimba. Mufwimi alijua kabisa kuwa kutakuwa na janga kubwa litakalomkumba pale  Mtemi Mduda atakapopata taarifa za mimba ya binti yake,  hivyo Mufwimi  akamwambia mpenzi wake kuwa kama atazaa mtoto wa kiume amfundishe kuwa mwiko wa ukoo wa Mombe ni Funo. Kisha akatoroka kuelekea kwao Ikombagulu.
Hakuna habari tena zinazosimuliwa kuhusu Mufwimi baada ya hapo, japo kuna habari zingine husema akina Mduda walimtafuta na kumuua Mufwimi kwa kosa la kumpa mimba dada yao bila ndoa,pengine hii ni hadithi tu kwani haijulikani kulikuwa na taratibu gani za kuishi  mtu na mzazi mwenzie zama hizo,
Mduda alimpa mjukuu wake jina la Mwamuyinga, yaani mtoto wa yule anayetangatanga. Mwamuyinga nae alikuwa na kuja kuwa muwindaji hodari kama baba yake, na pia alikuwa na busara sana, inaonekana alikuja kuwa kipenzi cha babu yake, hivyo alikuja kurithi sehemu ya utawala wa Babu yake, baada ya kifo cha Mduda.

Kuna hadithi za mapokeo kuhusu watawala waliokuja kumrithi Muyinga huyu wa kwanza, lakini nyingine ni wazi ni za kubuni, na pengine nyingine zimebadilika kutoka na kuwa zimekuwa zikirithiwa kwa kuhadithiana. Kilicho wazi ni kuwa kwa vyovyote Muyinga hakuweko kabla ya mwaka 1760, hivyo kutaja majina mengi ya warithi wa Muyinga wa kwanza na kudai kuwa wengine walitawala mpaka uzee sana  kunakosa mashiko kutokana ma  muda. 
Huwa majina kama Kitova, Lalika,  Mdegela, Kilonge hutajwa katika orodha ya watawala warithi wa Muyinga, lakini kuna wenye kudhani kuwa Kitowa ni jina jingine tu la Muyinga wa kwanza, na Lalika ni jina la mdogo wake Mdegela aliyekuwa babu mzazi wa Mkwava. Kuna wanaosema Kitoa na Mdegela ni jina lamtu huyohuyo mmoja, wengine husema Mdegela alikuwa mtoto wa Kilonge, na wengine husema Kilonge alikuwa mtoto wa Mdegela, na huo ndio mchanganyiko wenyewe. Kwa kuendeleza historia tukubali kuwa Kilonge alikuwa mtoto wa Mdegela.
Inasemekana kuwa akina Muyinga walikuwa wakioa katika ukoo wa  Mveyange, Kindole na Vanyamahuvi. Mpango huu ulikuwa tofali moja katika ujenzi wa kabila moja la Wahehe..
Kilonge alimuoa binti mmoja wa Kindole, ukumbuke kuwa Kindole alikuwa mtawala wa Lungemba baada ya msuguano na kaka yake Chota, hivyo baada ya Kilonge kumuoa Sekindole, binti huyo alipewa na baba yake askari 200 wa kumsindikiza na kumlinda na hatimae wawe walinzi wa sehemu aliyotawala Kilonge. Labda niongeze neno hapa, Wahehe walikuwa na utaratibu wa kuwa na vikosi vya askari mia mbili mia mbili. Baada ya kukabidhiwa  jeshi hili na mkwewe,  Kilonge akaanza kutamani  kutawala Nguluhe yote kama ilivyokuwa enzi za Mduda, hivyo akamtimua kaka yake aliyeitwa  Manga, ambae akalazimika  kukimbia na wafuasi wake ambamo pia walikuweko Watemikwila.
Kundi hili lilikimbia mpaka nyanda za juu za Ubena, sehemu ambayo sasa inaitwa Masagati. Jina hili lilitokana Mwarabu mmoja aliyeanzisha shamba la miti ya mpira na kuamua kupaita mahala hapo Muscat akikumbuka nchi aliyotoka, ugumu wa matamshi  ya jina hilo ukapafanya hapo paitwe MASAGATI. .   

Thursday, August 4, 2022

WAHABESHI , WAZIGUA NA WAJUKUU ZAO WAHEHE

 


Kipindi kilekile ambacho Vanyangologo walikuwa wakitoka ilipo Kenya na kuelekea kusini hadi kufika Uheheni, Mhabeshi mmoja alianza safari kwa kutumia punda, safari yake ilikuwa  kuelekea kusini mwa Uhabeshi. Alishuka chini mpaka kufika Ukambani ambapo alipata mke wa Kikamba na kuzaa nae watoto wakiwemo wanaume watatu.
Hawa watoto walipofika umri wa utu uzima, nao wakaondoka kwao nakusafiri kuelekea kusini zaidi kama alivyofanya baba yao, hatimae wakaingia  nchi ya Uzigua ambako wakaoa na kisha kuendelea na safari kuelekea kusini zaidi wakifuata njia ile ile waliopita Vanyagologo miaka kadhaa nyuma,
Hatimae waliingia Usagala na kufanya makazi yao mahala palipoitwa Ikombagulu, kule kwenye michoro ya kale ya kwenye mapango. Hapo wakaanzisha ukoo uliokuja kuitwa Mombe. Kuna wanaosema jina hili linauhusiano na Mombo iliyoko karibu na Lushoto. Kuna Wazigua wengine walikuja kuwafuata baadae nao hatimae walikuja kuwa Wahehe ambao hujulikana kwa 'mwidikiso' wa Vanyamsigula.
Katika wale watoto watatu wa yule Mhabeshi aliyeoa Mkamba, akina Mombe hukumbuka  jina la mtoto mmoja tu nalo ni Mubunsugulo. Akina Mombe husisitiza kuwa Mubunsugulo alikuwa mweupe, pengine weupe uliotokana na muingiliano wa Wareno na Wahabeshi, miaka mingi nyuma. Kwenye mwaka 1520 Wahabeshi waliomba msaada wa Wareno katika vita ya kidini iliyokuwa inaendelea, kikosi cha askari 400 wa Kireno waliweka makazi yao kwa miaka kadhaa katika nchi ya Uhabeshi.
Inasemekana Mubunsugulo alikuwa na watoto watatu. Wa kwanza Nguluchawangi,  huyu pia aliitwa Manga na alihamia Masagati, wa pili alikuja itwa Mufwimi yaani muwinaji, na wa tatu ni Ngwila ambaye alikuja kurithi kwa baba yake utawala wa  nchi kutoka Ikombagulu hadi Ifakara. Taarifa hii hupingwa na wazee wengine ambao husema Manga alikuwa kaka yake Kilonge, babu yake Mkwava na Ngwila alikuwa Mkamba aliyekuwa binamu yake Mubunsugulo. Hata hivyo kundi la wajukuu wa Ngwila lilihamia iliko Pawaga siku hizi. Vanyamsigula wengine walikwenda kuishi Wota kaskazini mwa Lyambanngali na wengine walikuja kuhamia Ugogo wakiwa na makundi makubwa ya ng’ombe.
Kuna hadithi moja ya ajabu sana kuhusu hawa waliohamia Ugogo. Kiongozi wao alipata ugonjwa wa  ndui, hivyo watu wake wakamtenga na kuhama na kumuacha peke yake. Siku moja radi kubwa ilipiga na kuwatisha  ng’ombe ambao walikimbia na kurudi makazi yao ya zamani alikoachwa yule kiongozi mwenye ndui. Yule kiongozi mwenye ndui aliweza kuanza kuishi kwa kunywa maziwa na kumuomba mizimu ya kwao hadi akapona ndui. Baada ya mkasa huu wa ajabu, Wamasai waliokuwa wakiishi jirani na maeneo hayo walimchagua awe Laibon wao.na kumpa jina la Arheringisho maana yake Ng’ombe mweusi mwenye nyota nyeupe kichwani.
Hadithi hii inaeleza kwa sababu gani Wamasai wa Ugogoni hujitapa kuwa asili ya mkuu wao ni moja na ile ya Mkwawa.
Siku moja Mufwimi mtoto wa Mubunsugulo, aliondoka Ikombagulu  kwenda kuwinda, akapitia Usagala, akapanda milima ya Udzungwa na kutokea Ng’uluhe, nchi ya udongo mwekundu. Wakati huo Nguluhe ilikuwa inatawaliwa na Mduda, huyu alikuwa Msagala aliyetokana na wale watu weupe  waliofukuzwa na Vanyangologo kama nilivyohadithia huko nyuma. Asili yake hiyo inathibitishwa na mwiko wa ukoo huo iliyokuwa  boga lililoitwa lilangala, ambalo huwa na rangi nyekundu ya kung’aa inayokumbusha asili ya ngozi yao.
Hata jina la ukoo huu huitwa pia Ginga yaani fuga nywele, ikimaananisha watoto wao walikuwa wakikumbushwa kufuga nywele zao ambazo zilikuwa  kama za kizungu au za kiarabu. Watoto wa Mduda walioa katika koo za Mveyange na Wategeta, walizaliwa watoto shupavu ambao hawakukubali kutawaliwa, wakaja kuitwa Vatemikwila, pengine kutokana na swali walilopenda kuuliza mtu yoyote aliyejifanya mtawala, Mtemi kwiya? Maana yake  We Mtemi wa wapi?

 

 


Wednesday, August 3, 2022

UNAJUA CHANZO CHA JINA MTAGE?

 


Kamwene vanyalukolo, leo naomba niendelee kutaja makundi mengine makubwa ya watu walioingia Uheheni. Kundi la kwanza ni lile lililotokea  Ukimbu, hili kundi linadhaniwa liliingia wakati mmoja na Wakilwa. Kundi hili lilikuwa likijiita Vanyandembwe, ndembwe ni tembo, na Vanyandembwe walikuwa wakidai asili yao ni tembo.
Kwa nyakati hizi ni ukoo wa akina Ugulumu na Ifweni ndio wajukuu wa kundi hili la Vanyandembwe. Baadae sana liliingia kundi jingine kutoka Ukimbu hili liliongozwa na  Mufilinge aliyekuwa mtoto wa Musawila aliyekuwa mtawala wa Ukimbu wakati huo. Na kwa sababu hiyo ukoo wa Mfilinge huitwa Vasawila, wao walikuja kuishi sehemu za kutoka  Makungu mpaka jirani ya Wasa na eneo hilo lilikuja julikana kama Usawila.
 Inawezekana walikuwa na uhusiano na Vanyamahuvi kwani , walipofika Uheheni walikaribishwa na Vanyamahuvi na kupewa eneo la  Makungu watawale, lakini baada ya muda mfupi waliongezeka na kutawala kuanzia Kiponzelo mpaka Malangali, jambo lililowaletea uadui na ukoo wa Nyilowa na Nyakunga ambao hatimae walihamia Uhafiwa na Udongwe.
Hawa Wasawila walipoingia uheheni walikuwa wakivaa aina ya nguo iliyotengenezwa kwa magamba ya miti yaliyotwangwa,  wenyeji wakawaita Vanyamwenda.
Pia walikuwa waganga wazuri hivyo wanawake zao wakapewa mwidiko ( muitikio) wa Ganga, wakati wanaume zao waliitika kwa Mikwile au Nyasite.
Wasawila waliendelea kukumbusha kuwa wao ni Wakimbu. Makundi mengine yalichukua lugha ya wenyeji na hakika Kihehe kilipata mchango wa maneno kutoka lugha nyingi za wageni walioingia.
Kwa mfano Wakimbu ndio walioleta neno Mtemi,  ambalo walilikopa ktoka kwa jirani zao Wanyamwezi. Wahehe wakaanza kutumia neno Wutemaa kumaananisha utawala, kabla ya hapo walikuwa wakitumia neno Wumutwa ambalo lilitoka kwa Wabena.
Kwa Wahehe jina Mtemi hutumika likiwa na maana mkata shauri au hakimu, kutema ni kukata. Wahehe waliamini mtunga sheria asiyehukumu na kuadhibu hawezi kuheshimiwa.
Lugha ya Kihehe imebadilika sana, kwa mfano ,nakumbuka wimbo ambao babu yangu alinifundisha na kunambia kuwa ulikuwa wimbo wa askari wa Kihehe walipotoka vitani, wacha niuimbe mwenye kuweza kuutafsiri tafadhali fanya hivyo kwenye sanduku la Comment hapo chini;
 Mitela kimalimali na manyile mtalavande
Oh Likalikasela 
Oh likoko ngomba mitela

Ukoo wa Ndondole hasa akina Kindole walisifika kupenda kujikweza kuwa wao ni ukoo wenye hadhi,  wanaume walijiita Mulugu Mutavangu, maana yake kiongozi wa wapiganaji na wanawake wakajiita Vanyatage yaani waliotupwa, hii ilikuwa kukumbusha kitendo cha Kindole kung’ang’ania kutawala Lungemba, na kumtupa kaka yake Chota aliyekwenda kutawala kwa Mnyaluhwao.
Baadae Wahehe waliendeleza utamaduni huu kwa kumuita mwanaume  mwenye hadhi Mulugu na mwanamke mwenye hadhi Mtage.

Tuesday, August 2, 2022

JE UNAJUA CHANZO CHA USEMI 'LUSUNGU LWA MNYALUHWAHO'?



Baada ya vurugu ya Vanyangologo kwisha, nchi ya Uhehe ikatulia kwa muda na ikaendelea kupata wageni kutoka sehemu nyingine mbalimbali, waliokuja kuhamia Uheheni.  Kutoka Ukimbu yalikuja makundi mawili, moja likiongozwa na Ndondole na Muntsali na la pili liliongozwa na Mwigiha na Nyilowa. Kutokana na maelezo ya wahenga, watu hawa hawakuwa weusi,  walikuwa weupe japokuwa weupe wao si ule wa wazungu.

Kundi la Ndondole na Muntsali likaja kuhamia panapoitwa Panunu karibu na lilipo kanisa Katoliki la Malangali, na kundi la Mwigiha na Nyilowa likaenda kuweka maskani yake Uhafiwa. Kuna uwezekano mkubwa kuwa makundi haya yalikuwa na chanzo kimoja kwani mwiko wa kundi la Mwigiha na Nyilowa, ulikuwa ni ule ule wa kundi la Muntsali na Ndondole , mwiko wao ulikuwa ng’anga au  Kanga. Pia hata mwidikiso wao wote ulikuwa Nyamahuvi. Baadae Nyilowa  aliongoza kundi lake na kwenda kufanya maskani yao Lutemi na kule Makungu. Kati ya watoto wote wa Nyilowa, aliyekuja kuwa maarufu zaidi ni Nyakunga.  Watoto wa Mwigiha walikuja kuwa watawala., mtoto wake wa kwanza aliitwa Lyelu, huyu  alitawala kuanzia Welu hadi Pawaga, na mtoto wake  mwingine aliitwa  Mwano, huyu  alitawala kuanzia kilima cha Utinde, kaskazini mwa Kalenga, sehemu ya ilipo Iringa sasa na mpaka  sehemu za Nduli, na  sehemu kadhaa za Pawaga mpaka Manyile juu ya Ndewela.  Kuna akina Nyakunga mpaka karibuni wamekuwa wakizaliwa na kuwa na nywele nyekundu au zenye rangi ya dhahabu. Na kuna wajukuu wa akina Mwano walio na nywele za singa laini za kahawia, za kukaribiana na rangi za nywele za wazungu.
Muntsali alikuja kuongoza wafuasi wake wakahamia Wanging’ombe, huko akawa mtawala. Mwanamke mmoja kutoka ukoo wake alikuja kuolewa Uwanji na mwanae ndie akaja kuwa Chifu Merere wa kwanza aliyetawala, huyu aliwatawala Wasangu na Wasafwa.
Jina la awali la Ndondole lilikuwa Benna, siku hizi wajukuu wanaume wa ukoo huitwa kwa mwidikiso wa Benaa na wanawake Nyatende. Ndondole pia alikuwa na watoto wengi lakini waliokuja kujitokeza zaidi katika historia ya Wahehe ni Chavala na Kimamu.
Chavala alikuja kuhamia Mufindi, na ukoo uliokuwa unatawala kule, ukoo wa Kavindikadodi, ukamuachia nchi atawale. Akapata mke Sekiduku, ambaye alipata mimba lakini wakati wakati wa kuzaa mtoto akawa hatoki, hivyo wakalazimika kufanya kile ambacho ni cha kawaida siku hizi, nacho ni kutanua njia kwa kumchana, na mtoto akazaliwa salama. Kuchana kwa Kihehe ni kudemula, hivyo mtoto huyo akaitwa Mdemu.
Watu wa ukoo wa Chavala, hasa akina Mdemu, huwa na si weusi huwa na rangi nyepesi na nywele nyekundu. Wanawake wa ukoo huu huitika kwa mwidikiso wa  Gogo. Sifa moja ya ukoo wa Chavala ni uganga wa kiasili.
Huyu mtoto mwingine wa Ndondole, yaani Kimamu, alizaa watoto wengi , lakini historia ya Uhehe  inawakumbuka sana  wawili Chota na Kindole .  Hawa walijulikana sana kwa uganga wa kuzindika nyumba, mashamba na hata nchi nzima. Kwa sababu hiyo waliitwa na watawala huku na kule kwenda kuwa zindika, hata Wakilwa waliokuwa wakitawala sehemu mbalimbali za Uheheni,  waliwaita ili wazindike nchi yao ili kusitokee tena kuingiliwa na maadui kama wale waliokuwa wakiteka watumwa au kushambuliwa tena na Vanyangologo.
Wakati mmoja  Chota na Kindole waliitwa  Lungemba ili wakatawale,  ili watu wawe na uhakika wa usalama. Chota aliyekuwa mkubwa akamwambia mdogo wake achukue ng’ombe na yeye achukue nchi. Kindole alikuja juu na kuanza kuchoma mikuki hovyo ng’ombe aliokuwa kakusanyiwa, huku akuisema ‘Sitaki ng’ombe nataka nchi’. Watu waliweza kuwatuliza na kumuomba Chota amuache mdogo wake atawale Lungemba na yeye akatawale Iwawa, nchi iliyokuwa na rutuba na wenyeji wake walikuwa tayari kumpokea awe mkuu wao. Chota akaafiki wazo lile.
Iwawa wakati huo ilikuwa ikitawaliwa na Munyaluwaho, mjukuu wa Mdongwe na Mkilwa wa ukoo wa Kavindikadodi. Mnyaluwaho aliposikia Chota anakuja akamuandalia karamu na kumpokea vizuri sana. Walipokula na kushiba na watu wakiendelea na sherehe ya kumpokea mkuu mpya, Chota, ambaye inasemekana alikuwamtu mwenye miraba minne, na alikuwa na ndevu ndefu za singa, alikuwa mweupe kiasi cha watu kumuita mwelu, alichukua mkuki na kumchoma nao Mnyaluwaho moyoni na kumuua palepale.  Wenyeji walitimka mbio hovyo,  ndugu wa Mnyaluwaho, akina Kavindikadodi wakakimbia kabisa nchi na kuhamia Udzungwa.  Hivyo Chota akaanza kutawala akiwa na uhakika hatapata upinzani kutoka kwa ndugu wa marehemu. Himaya ya Chota ilianzia Iwawa mpaka ilipo Iringa, na hata sehemu za Udongwe. Makao yake yakawa Luhota iliyokuwa katikati ya Udongwe.  Kuanzia wakati huo Wahehe walipata msemo ‘lusungu lwa Munyaluhwao’…yaani ukarimu wa Mnyaluhwao ulivyomponza….ili kuonya hatari za ukarimu kwa usiemjua vizuri….. Wahusika toeni maoni

 

 

Monday, August 1, 2022

JE UNAJUA MWITIKO AU MWIDIKISO WA MGONANZI ULITOKA WAPI? SOMA HAPA

WAZEE  wa zamani wa Kisambaa walikuwa wakihadithia kuwa kuna wakati kundi kubwa la Wahumba lilipita nchini kwao likielekea Kusini, ilikuwa ni wakati Waarabu wa Oman chini ya Mfalme wao Said Bin Sultan walipokuwa wakiwashambulia Wareno katika ngome  yao  Fort Jesus kule Mombasa. Kwa tarehe hizo ina maana Wahumba hao walipita Usambaa kati ya tarehe 13 March 1696 na 13 March1698.  Wahumba hao walikuwa wakiongozwa na Wahabeshi.  Wahumba hawa walikuwaa wametoboa masikio yao na kuyarefusha hadi kufikia karibu na mabega na hivyo masikio yalifanana na aina ya pembe za  ng’ombe ambazo hupinda na  kuangalia chini, pembe za aina hiyo hiyo huitwa Ngologo, hivyo Vahumba hawa walipoingia Uheheni walikuja julikana kama  Vanyangologo.
Vahumba hawa waliingia Uheheni kupitia Wota kisha wakavuka  Lyambangali na kuingia Ugunda. Kama nilivyokuhadithia katika masimulizi huko nyuma, Ugunda ilikaliwa na watu weupe ambao wenyeji waliwaita Valangi.
Wahumba hawa waliwashambulia Valangi na kukawa na mapigano makali watu wengi pande zote wakapoteza maisha na Valangi wakalazimika kukimbia na ndipo wakahamia Singida kama nilivyokuhadithia hapo awali.
Pale Ugunda kulitapakaa sime za Vahumba waliouwawa, na kwa kuwa wahehe huita sime Mage, mahala pale pakaitwa Image mpaka hivi leo.
Vanyangologo waliendelea na safari yao ya kusaka watu weupe huku wakiacha ndugu zao wengine kuwaangalia majeruhi pale Image. Safari hiyo ya kuwaska na kuwauwa watu weupe iliendelea mpaka Ilongo, Ubena, na hata Ukimbu.
Kitu cha ajabu ni kuwa Vahumba hawa hawakushughulika na Vakilwa, hivyo Vakilwa walikuja kuanza kutawala sehemu nyingi ambazo hawakuguswa.
Wale Vanyangologo waliobaki Image walianza mahusiano na wanawake wa Usagala, Hivyo katika sehemu za Image na Ilole kukawa na koo za wahehe ambao wanafanana na Wamasai kwa umbo, na sura zao za kuchongoka.
Wengi hukataa kuwa asili ya kizazi chao ni  Vahumba lakini wanadai asili yao ni Hamitic. Lakini Humma maana yake ni Hamitic. Akina Ngimba wa Ilole asili yao ni Vahumba. Itakumbukwa kuwa  mama mzazi wa Mutwa Mkwava alikuwa Sengimba.
Ukoo wa akina Sambala asili yao ni Wahamitic, hata mwitiko au mwidikiso wao ni Mugonanzi , maana yake mwenye kulala sehemu mbalimbali au mhamaji, kwa Kiingereza tungesema nomad na hiyo ndiyo ilikuwa sifa ya Vahuma.
Wale wasagala weupe hawakukwepa kusakwa na Wahumba, wengine wao walikimbilia Wota kwa kuvuka Lyambangali,hawa wakaja kujiita  Mlowoka. Kuna walowoka wengine walikuja kurudi Uheheni  kama ukoo wa Fivawo na Makombe wa Tanangozi na Iwawa. Mliotajwa mnasemaje?

 

 

 

 


STAT COUNTER