Kundi la Ndondole na Muntsali likaja kuhamia panapoitwa Panunu
karibu na lilipo kanisa Katoliki la Malangali, na kundi la Mwigiha na Nyilowa
likaenda kuweka maskani yake Uhafiwa. Kuna uwezekano mkubwa kuwa makundi haya
yalikuwa na chanzo kimoja kwani mwiko wa kundi la Mwigiha na Nyilowa, ulikuwa
ni ule ule wa kundi la Muntsali na Ndondole , mwiko wao ulikuwa ng’anga au Kanga. Pia hata mwidikiso wao wote ulikuwa
Nyamahuvi. Baadae Nyilowa aliongoza
kundi lake na kwenda kufanya maskani yao Lutemi na kule Makungu. Kati ya watoto
wote wa Nyilowa, aliyekuja kuwa maarufu zaidi ni Nyakunga. Watoto wa Mwigiha walikuja kuwa watawala.,
mtoto wake wa kwanza aliitwa Lyelu, huyu alitawala kuanzia Welu hadi Pawaga, na mtoto
wake mwingine aliitwa Mwano, huyu alitawala kuanzia kilima cha Utinde, kaskazini
mwa Kalenga, sehemu ya ilipo Iringa sasa na mpaka sehemu za Nduli, na sehemu kadhaa za Pawaga mpaka Manyile juu ya
Ndewela. Kuna akina Nyakunga mpaka
karibuni wamekuwa wakizaliwa na kuwa na nywele nyekundu au zenye rangi ya
dhahabu. Na kuna wajukuu wa akina Mwano walio na nywele za singa laini za
kahawia, za kukaribiana na rangi za nywele za wazungu.
Muntsali alikuja kuongoza wafuasi wake wakahamia Wanging’ombe, huko akawa
mtawala. Mwanamke mmoja kutoka ukoo wake alikuja kuolewa Uwanji na mwanae ndie
akaja kuwa Chifu Merere wa kwanza aliyetawala, huyu aliwatawala Wasangu na
Wasafwa.
Jina la awali la Ndondole lilikuwa Benna, siku hizi wajukuu wanaume wa ukoo
huitwa kwa mwidikiso wa Benaa na wanawake Nyatende. Ndondole pia alikuwa na
watoto wengi lakini waliokuja kujitokeza zaidi katika historia ya Wahehe ni
Chavala na Kimamu.
Chavala alikuja kuhamia Mufindi, na ukoo uliokuwa unatawala kule, ukoo wa
Kavindikadodi, ukamuachia nchi atawale. Akapata mke Sekiduku, ambaye alipata
mimba lakini wakati wakati wa kuzaa mtoto akawa hatoki, hivyo wakalazimika
kufanya kile ambacho ni cha kawaida siku hizi, nacho ni kutanua njia kwa kumchana,
na mtoto akazaliwa salama. Kuchana kwa Kihehe ni kudemula, hivyo mtoto huyo
akaitwa Mdemu.
Watu wa ukoo wa Chavala, hasa akina Mdemu, huwa na si weusi huwa na rangi
nyepesi na nywele nyekundu. Wanawake wa ukoo huu huitika kwa mwidikiso wa Gogo. Sifa moja ya ukoo wa Chavala ni uganga
wa kiasili.
Huyu mtoto mwingine wa Ndondole, yaani Kimamu, alizaa watoto wengi , lakini
historia ya Uhehe inawakumbuka sana wawili Chota na Kindole . Hawa walijulikana sana kwa uganga wa
kuzindika nyumba, mashamba na hata nchi nzima. Kwa sababu hiyo waliitwa na
watawala huku na kule kwenda kuwa zindika, hata Wakilwa waliokuwa wakitawala
sehemu mbalimbali za Uheheni, waliwaita
ili wazindike nchi yao ili kusitokee tena kuingiliwa na maadui kama wale
waliokuwa wakiteka watumwa au kushambuliwa tena na Vanyangologo.
Wakati mmoja Chota na Kindole
waliitwa Lungemba ili wakatawale, ili watu wawe na uhakika wa usalama. Chota
aliyekuwa mkubwa akamwambia mdogo wake achukue ng’ombe na yeye achukue nchi.
Kindole alikuja juu na kuanza kuchoma mikuki hovyo ng’ombe aliokuwa kakusanyiwa,
huku akuisema ‘Sitaki ng’ombe nataka nchi’. Watu waliweza kuwatuliza na
kumuomba Chota amuache mdogo wake atawale Lungemba na yeye akatawale Iwawa, nchi
iliyokuwa na rutuba na wenyeji wake walikuwa tayari kumpokea awe mkuu wao.
Chota akaafiki wazo lile.
Iwawa wakati huo ilikuwa ikitawaliwa na Munyaluwaho, mjukuu wa Mdongwe na Mkilwa
wa ukoo wa Kavindikadodi. Mnyaluwaho aliposikia Chota anakuja akamuandalia
karamu na kumpokea vizuri sana. Walipokula na kushiba na watu wakiendelea na
sherehe ya kumpokea mkuu mpya, Chota, ambaye inasemekana alikuwamtu mwenye
miraba minne, na alikuwa na ndevu ndefu za singa, alikuwa mweupe kiasi cha watu
kumuita mwelu, alichukua mkuki na kumchoma nao Mnyaluwaho moyoni na kumuua
palepale. Wenyeji walitimka mbio
hovyo, ndugu wa Mnyaluwaho, akina
Kavindikadodi wakakimbia kabisa nchi na kuhamia Udzungwa. Hivyo Chota akaanza kutawala akiwa na uhakika
hatapata upinzani kutoka kwa ndugu wa marehemu. Himaya ya Chota ilianzia Iwawa
mpaka ilipo Iringa, na hata sehemu za Udongwe. Makao yake yakawa Luhota iliyokuwa
katikati ya Udongwe. Kuanzia wakati huo
Wahehe walipata msemo ‘lusungu lwa
Munyaluhwao’…yaani ukarimu wa Mnyaluhwao ulivyomponza….ili kuonya hatari za
ukarimu kwa usiemjua vizuri….. Wahusika toeni maoni
Tuesday, August 2, 2022
JE UNAJUA CHANZO CHA USEMI 'LUSUNGU LWA MNYALUHWAHO'?
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment