WAZEE wa zamani wa
Kisambaa walikuwa wakihadithia kuwa kuna wakati kundi kubwa la Wahumba lilipita
nchini kwao likielekea Kusini, ilikuwa ni wakati Waarabu wa Oman chini ya
Mfalme wao Said Bin Sultan walipokuwa wakiwashambulia Wareno katika ngome yao Fort
Jesus kule Mombasa. Kwa tarehe hizo ina maana Wahumba hao walipita Usambaa kati
ya tarehe 13 March 1696 na 13 March1698. Wahumba hao walikuwa wakiongozwa na Wahabeshi.
Wahumba hawa walikuwaa wametoboa masikio
yao na kuyarefusha hadi kufikia karibu na mabega na hivyo masikio yalifanana na
aina ya pembe za ng’ombe ambazo hupinda
na kuangalia chini, pembe za aina hiyo
hiyo huitwa Ngologo, hivyo Vahumba hawa walipoingia Uheheni walikuja julikana
kama Vanyangologo.
Vahumba hawa waliingia Uheheni kupitia Wota kisha wakavuka Lyambangali na kuingia Ugunda. Kama
nilivyokuhadithia katika masimulizi huko nyuma, Ugunda ilikaliwa na watu weupe
ambao wenyeji waliwaita Valangi.
Wahumba hawa waliwashambulia Valangi na kukawa na mapigano makali watu wengi
pande zote wakapoteza maisha na Valangi wakalazimika kukimbia na ndipo
wakahamia Singida kama nilivyokuhadithia hapo awali.
Pale Ugunda kulitapakaa sime za Vahumba waliouwawa, na kwa kuwa wahehe huita
sime Mage, mahala pale pakaitwa Image mpaka hivi leo.
Vanyangologo waliendelea na safari yao ya kusaka watu weupe huku wakiacha ndugu
zao wengine kuwaangalia majeruhi pale Image. Safari hiyo ya kuwaska na kuwauwa
watu weupe iliendelea mpaka Ilongo, Ubena, na hata Ukimbu.
Kitu cha ajabu ni kuwa Vahumba hawa hawakushughulika na Vakilwa, hivyo Vakilwa
walikuja kuanza kutawala sehemu nyingi ambazo hawakuguswa.
Wale Vanyangologo waliobaki Image walianza mahusiano na wanawake wa Usagala,
Hivyo katika sehemu za Image na Ilole kukawa na koo za wahehe ambao wanafanana
na Wamasai kwa umbo, na sura zao za kuchongoka.
Wengi hukataa kuwa asili ya kizazi chao ni
Vahumba lakini wanadai asili yao ni Hamitic. Lakini Humma maana yake ni
Hamitic. Akina Ngimba wa Ilole asili yao ni Vahumba. Itakumbukwa kuwa mama mzazi wa Mutwa Mkwava alikuwa Sengimba.
Ukoo wa akina Sambala asili yao ni Wahamitic, hata mwitiko au mwidikiso wao ni
Mugonanzi , maana yake mwenye kulala sehemu mbalimbali au mhamaji, kwa
Kiingereza tungesema nomad na hiyo ndiyo ilikuwa sifa ya Vahuma.
Wale wasagala weupe hawakukwepa kusakwa na Wahumba, wengine wao walikimbilia
Wota kwa kuvuka Lyambangali,hawa wakaja kujiita
Mlowoka. Kuna walowoka wengine walikuja kurudi Uheheni kama ukoo wa Fivawo na Makombe wa Tanangozi
na Iwawa. Mliotajwa mnasemaje?