Pages

Thursday, August 4, 2022

WAHABESHI , WAZIGUA NA WAJUKUU ZAO WAHEHE

 


Kipindi kilekile ambacho Vanyangologo walikuwa wakitoka ilipo Kenya na kuelekea kusini hadi kufika Uheheni, Mhabeshi mmoja alianza safari kwa kutumia punda, safari yake ilikuwa  kuelekea kusini mwa Uhabeshi. Alishuka chini mpaka kufika Ukambani ambapo alipata mke wa Kikamba na kuzaa nae watoto wakiwemo wanaume watatu.
Hawa watoto walipofika umri wa utu uzima, nao wakaondoka kwao nakusafiri kuelekea kusini zaidi kama alivyofanya baba yao, hatimae wakaingia  nchi ya Uzigua ambako wakaoa na kisha kuendelea na safari kuelekea kusini zaidi wakifuata njia ile ile waliopita Vanyagologo miaka kadhaa nyuma,
Hatimae waliingia Usagala na kufanya makazi yao mahala palipoitwa Ikombagulu, kule kwenye michoro ya kale ya kwenye mapango. Hapo wakaanzisha ukoo uliokuja kuitwa Mombe. Kuna wanaosema jina hili linauhusiano na Mombo iliyoko karibu na Lushoto. Kuna Wazigua wengine walikuja kuwafuata baadae nao hatimae walikuja kuwa Wahehe ambao hujulikana kwa 'mwidikiso' wa Vanyamsigula.
Katika wale watoto watatu wa yule Mhabeshi aliyeoa Mkamba, akina Mombe hukumbuka  jina la mtoto mmoja tu nalo ni Mubunsugulo. Akina Mombe husisitiza kuwa Mubunsugulo alikuwa mweupe, pengine weupe uliotokana na muingiliano wa Wareno na Wahabeshi, miaka mingi nyuma. Kwenye mwaka 1520 Wahabeshi waliomba msaada wa Wareno katika vita ya kidini iliyokuwa inaendelea, kikosi cha askari 400 wa Kireno waliweka makazi yao kwa miaka kadhaa katika nchi ya Uhabeshi.
Inasemekana Mubunsugulo alikuwa na watoto watatu. Wa kwanza Nguluchawangi,  huyu pia aliitwa Manga na alihamia Masagati, wa pili alikuja itwa Mufwimi yaani muwinaji, na wa tatu ni Ngwila ambaye alikuja kurithi kwa baba yake utawala wa  nchi kutoka Ikombagulu hadi Ifakara. Taarifa hii hupingwa na wazee wengine ambao husema Manga alikuwa kaka yake Kilonge, babu yake Mkwava na Ngwila alikuwa Mkamba aliyekuwa binamu yake Mubunsugulo. Hata hivyo kundi la wajukuu wa Ngwila lilihamia iliko Pawaga siku hizi. Vanyamsigula wengine walikwenda kuishi Wota kaskazini mwa Lyambanngali na wengine walikuja kuhamia Ugogo wakiwa na makundi makubwa ya ng’ombe.
Kuna hadithi moja ya ajabu sana kuhusu hawa waliohamia Ugogo. Kiongozi wao alipata ugonjwa wa  ndui, hivyo watu wake wakamtenga na kuhama na kumuacha peke yake. Siku moja radi kubwa ilipiga na kuwatisha  ng’ombe ambao walikimbia na kurudi makazi yao ya zamani alikoachwa yule kiongozi mwenye ndui. Yule kiongozi mwenye ndui aliweza kuanza kuishi kwa kunywa maziwa na kumuomba mizimu ya kwao hadi akapona ndui. Baada ya mkasa huu wa ajabu, Wamasai waliokuwa wakiishi jirani na maeneo hayo walimchagua awe Laibon wao.na kumpa jina la Arheringisho maana yake Ng’ombe mweusi mwenye nyota nyeupe kichwani.
Hadithi hii inaeleza kwa sababu gani Wamasai wa Ugogoni hujitapa kuwa asili ya mkuu wao ni moja na ile ya Mkwawa.
Siku moja Mufwimi mtoto wa Mubunsugulo, aliondoka Ikombagulu  kwenda kuwinda, akapitia Usagala, akapanda milima ya Udzungwa na kutokea Ng’uluhe, nchi ya udongo mwekundu. Wakati huo Nguluhe ilikuwa inatawaliwa na Mduda, huyu alikuwa Msagala aliyetokana na wale watu weupe  waliofukuzwa na Vanyangologo kama nilivyohadithia huko nyuma. Asili yake hiyo inathibitishwa na mwiko wa ukoo huo iliyokuwa  boga lililoitwa lilangala, ambalo huwa na rangi nyekundu ya kung’aa inayokumbusha asili ya ngozi yao.
Hata jina la ukoo huu huitwa pia Ginga yaani fuga nywele, ikimaananisha watoto wao walikuwa wakikumbushwa kufuga nywele zao ambazo zilikuwa  kama za kizungu au za kiarabu. Watoto wa Mduda walioa katika koo za Mveyange na Wategeta, walizaliwa watoto shupavu ambao hawakukubali kutawaliwa, wakaja kuitwa Vatemikwila, pengine kutokana na swali walilopenda kuuliza mtu yoyote aliyejifanya mtawala, Mtemi kwiya? Maana yake  We Mtemi wa wapi?

 

 


Wednesday, August 3, 2022

UNAJUA CHANZO CHA JINA MTAGE?

 


Kamwene vanyalukolo, leo naomba niendelee kutaja makundi mengine makubwa ya watu walioingia Uheheni. Kundi la kwanza ni lile lililotokea  Ukimbu, hili kundi linadhaniwa liliingia wakati mmoja na Wakilwa. Kundi hili lilikuwa likijiita Vanyandembwe, ndembwe ni tembo, na Vanyandembwe walikuwa wakidai asili yao ni tembo.
Kwa nyakati hizi ni ukoo wa akina Ugulumu na Ifweni ndio wajukuu wa kundi hili la Vanyandembwe. Baadae sana liliingia kundi jingine kutoka Ukimbu hili liliongozwa na  Mufilinge aliyekuwa mtoto wa Musawila aliyekuwa mtawala wa Ukimbu wakati huo. Na kwa sababu hiyo ukoo wa Mfilinge huitwa Vasawila, wao walikuja kuishi sehemu za kutoka  Makungu mpaka jirani ya Wasa na eneo hilo lilikuja julikana kama Usawila.
 Inawezekana walikuwa na uhusiano na Vanyamahuvi kwani , walipofika Uheheni walikaribishwa na Vanyamahuvi na kupewa eneo la  Makungu watawale, lakini baada ya muda mfupi waliongezeka na kutawala kuanzia Kiponzelo mpaka Malangali, jambo lililowaletea uadui na ukoo wa Nyilowa na Nyakunga ambao hatimae walihamia Uhafiwa na Udongwe.
Hawa Wasawila walipoingia uheheni walikuwa wakivaa aina ya nguo iliyotengenezwa kwa magamba ya miti yaliyotwangwa,  wenyeji wakawaita Vanyamwenda.
Pia walikuwa waganga wazuri hivyo wanawake zao wakapewa mwidiko ( muitikio) wa Ganga, wakati wanaume zao waliitika kwa Mikwile au Nyasite.
Wasawila waliendelea kukumbusha kuwa wao ni Wakimbu. Makundi mengine yalichukua lugha ya wenyeji na hakika Kihehe kilipata mchango wa maneno kutoka lugha nyingi za wageni walioingia.
Kwa mfano Wakimbu ndio walioleta neno Mtemi,  ambalo walilikopa ktoka kwa jirani zao Wanyamwezi. Wahehe wakaanza kutumia neno Wutemaa kumaananisha utawala, kabla ya hapo walikuwa wakitumia neno Wumutwa ambalo lilitoka kwa Wabena.
Kwa Wahehe jina Mtemi hutumika likiwa na maana mkata shauri au hakimu, kutema ni kukata. Wahehe waliamini mtunga sheria asiyehukumu na kuadhibu hawezi kuheshimiwa.
Lugha ya Kihehe imebadilika sana, kwa mfano ,nakumbuka wimbo ambao babu yangu alinifundisha na kunambia kuwa ulikuwa wimbo wa askari wa Kihehe walipotoka vitani, wacha niuimbe mwenye kuweza kuutafsiri tafadhali fanya hivyo kwenye sanduku la Comment hapo chini;
 Mitela kimalimali na manyile mtalavande
Oh Likalikasela 
Oh likoko ngomba mitela

Ukoo wa Ndondole hasa akina Kindole walisifika kupenda kujikweza kuwa wao ni ukoo wenye hadhi,  wanaume walijiita Mulugu Mutavangu, maana yake kiongozi wa wapiganaji na wanawake wakajiita Vanyatage yaani waliotupwa, hii ilikuwa kukumbusha kitendo cha Kindole kung’ang’ania kutawala Lungemba, na kumtupa kaka yake Chota aliyekwenda kutawala kwa Mnyaluhwao.
Baadae Wahehe waliendeleza utamaduni huu kwa kumuita mwanaume  mwenye hadhi Mulugu na mwanamke mwenye hadhi Mtage.

Tuesday, August 2, 2022

JE UNAJUA CHANZO CHA USEMI 'LUSUNGU LWA MNYALUHWAHO'?



Baada ya vurugu ya Vanyangologo kwisha, nchi ya Uhehe ikatulia kwa muda na ikaendelea kupata wageni kutoka sehemu nyingine mbalimbali, waliokuja kuhamia Uheheni.  Kutoka Ukimbu yalikuja makundi mawili, moja likiongozwa na Ndondole na Muntsali na la pili liliongozwa na Mwigiha na Nyilowa. Kutokana na maelezo ya wahenga, watu hawa hawakuwa weusi,  walikuwa weupe japokuwa weupe wao si ule wa wazungu.

Kundi la Ndondole na Muntsali likaja kuhamia panapoitwa Panunu karibu na lilipo kanisa Katoliki la Malangali, na kundi la Mwigiha na Nyilowa likaenda kuweka maskani yake Uhafiwa. Kuna uwezekano mkubwa kuwa makundi haya yalikuwa na chanzo kimoja kwani mwiko wa kundi la Mwigiha na Nyilowa, ulikuwa ni ule ule wa kundi la Muntsali na Ndondole , mwiko wao ulikuwa ng’anga au  Kanga. Pia hata mwidikiso wao wote ulikuwa Nyamahuvi. Baadae Nyilowa  aliongoza kundi lake na kwenda kufanya maskani yao Lutemi na kule Makungu. Kati ya watoto wote wa Nyilowa, aliyekuja kuwa maarufu zaidi ni Nyakunga.  Watoto wa Mwigiha walikuja kuwa watawala., mtoto wake wa kwanza aliitwa Lyelu, huyu  alitawala kuanzia Welu hadi Pawaga, na mtoto wake  mwingine aliitwa  Mwano, huyu  alitawala kuanzia kilima cha Utinde, kaskazini mwa Kalenga, sehemu ya ilipo Iringa sasa na mpaka  sehemu za Nduli, na  sehemu kadhaa za Pawaga mpaka Manyile juu ya Ndewela.  Kuna akina Nyakunga mpaka karibuni wamekuwa wakizaliwa na kuwa na nywele nyekundu au zenye rangi ya dhahabu. Na kuna wajukuu wa akina Mwano walio na nywele za singa laini za kahawia, za kukaribiana na rangi za nywele za wazungu.
Muntsali alikuja kuongoza wafuasi wake wakahamia Wanging’ombe, huko akawa mtawala. Mwanamke mmoja kutoka ukoo wake alikuja kuolewa Uwanji na mwanae ndie akaja kuwa Chifu Merere wa kwanza aliyetawala, huyu aliwatawala Wasangu na Wasafwa.
Jina la awali la Ndondole lilikuwa Benna, siku hizi wajukuu wanaume wa ukoo huitwa kwa mwidikiso wa Benaa na wanawake Nyatende. Ndondole pia alikuwa na watoto wengi lakini waliokuja kujitokeza zaidi katika historia ya Wahehe ni Chavala na Kimamu.
Chavala alikuja kuhamia Mufindi, na ukoo uliokuwa unatawala kule, ukoo wa Kavindikadodi, ukamuachia nchi atawale. Akapata mke Sekiduku, ambaye alipata mimba lakini wakati wakati wa kuzaa mtoto akawa hatoki, hivyo wakalazimika kufanya kile ambacho ni cha kawaida siku hizi, nacho ni kutanua njia kwa kumchana, na mtoto akazaliwa salama. Kuchana kwa Kihehe ni kudemula, hivyo mtoto huyo akaitwa Mdemu.
Watu wa ukoo wa Chavala, hasa akina Mdemu, huwa na si weusi huwa na rangi nyepesi na nywele nyekundu. Wanawake wa ukoo huu huitika kwa mwidikiso wa  Gogo. Sifa moja ya ukoo wa Chavala ni uganga wa kiasili.
Huyu mtoto mwingine wa Ndondole, yaani Kimamu, alizaa watoto wengi , lakini historia ya Uhehe  inawakumbuka sana  wawili Chota na Kindole .  Hawa walijulikana sana kwa uganga wa kuzindika nyumba, mashamba na hata nchi nzima. Kwa sababu hiyo waliitwa na watawala huku na kule kwenda kuwa zindika, hata Wakilwa waliokuwa wakitawala sehemu mbalimbali za Uheheni,  waliwaita ili wazindike nchi yao ili kusitokee tena kuingiliwa na maadui kama wale waliokuwa wakiteka watumwa au kushambuliwa tena na Vanyangologo.
Wakati mmoja  Chota na Kindole waliitwa  Lungemba ili wakatawale,  ili watu wawe na uhakika wa usalama. Chota aliyekuwa mkubwa akamwambia mdogo wake achukue ng’ombe na yeye achukue nchi. Kindole alikuja juu na kuanza kuchoma mikuki hovyo ng’ombe aliokuwa kakusanyiwa, huku akuisema ‘Sitaki ng’ombe nataka nchi’. Watu waliweza kuwatuliza na kumuomba Chota amuache mdogo wake atawale Lungemba na yeye akatawale Iwawa, nchi iliyokuwa na rutuba na wenyeji wake walikuwa tayari kumpokea awe mkuu wao. Chota akaafiki wazo lile.
Iwawa wakati huo ilikuwa ikitawaliwa na Munyaluwaho, mjukuu wa Mdongwe na Mkilwa wa ukoo wa Kavindikadodi. Mnyaluwaho aliposikia Chota anakuja akamuandalia karamu na kumpokea vizuri sana. Walipokula na kushiba na watu wakiendelea na sherehe ya kumpokea mkuu mpya, Chota, ambaye inasemekana alikuwamtu mwenye miraba minne, na alikuwa na ndevu ndefu za singa, alikuwa mweupe kiasi cha watu kumuita mwelu, alichukua mkuki na kumchoma nao Mnyaluwaho moyoni na kumuua palepale.  Wenyeji walitimka mbio hovyo,  ndugu wa Mnyaluwaho, akina Kavindikadodi wakakimbia kabisa nchi na kuhamia Udzungwa.  Hivyo Chota akaanza kutawala akiwa na uhakika hatapata upinzani kutoka kwa ndugu wa marehemu. Himaya ya Chota ilianzia Iwawa mpaka ilipo Iringa, na hata sehemu za Udongwe. Makao yake yakawa Luhota iliyokuwa katikati ya Udongwe.  Kuanzia wakati huo Wahehe walipata msemo ‘lusungu lwa Munyaluhwao’…yaani ukarimu wa Mnyaluhwao ulivyomponza….ili kuonya hatari za ukarimu kwa usiemjua vizuri….. Wahusika toeni maoni

 

 

Monday, August 1, 2022

JE UNAJUA MWITIKO AU MWIDIKISO WA MGONANZI ULITOKA WAPI? SOMA HAPA

WAZEE  wa zamani wa Kisambaa walikuwa wakihadithia kuwa kuna wakati kundi kubwa la Wahumba lilipita nchini kwao likielekea Kusini, ilikuwa ni wakati Waarabu wa Oman chini ya Mfalme wao Said Bin Sultan walipokuwa wakiwashambulia Wareno katika ngome  yao  Fort Jesus kule Mombasa. Kwa tarehe hizo ina maana Wahumba hao walipita Usambaa kati ya tarehe 13 March 1696 na 13 March1698.  Wahumba hao walikuwa wakiongozwa na Wahabeshi.  Wahumba hawa walikuwaa wametoboa masikio yao na kuyarefusha hadi kufikia karibu na mabega na hivyo masikio yalifanana na aina ya pembe za  ng’ombe ambazo hupinda na  kuangalia chini, pembe za aina hiyo hiyo huitwa Ngologo, hivyo Vahumba hawa walipoingia Uheheni walikuja julikana kama  Vanyangologo.
Vahumba hawa waliingia Uheheni kupitia Wota kisha wakavuka  Lyambangali na kuingia Ugunda. Kama nilivyokuhadithia katika masimulizi huko nyuma, Ugunda ilikaliwa na watu weupe ambao wenyeji waliwaita Valangi.
Wahumba hawa waliwashambulia Valangi na kukawa na mapigano makali watu wengi pande zote wakapoteza maisha na Valangi wakalazimika kukimbia na ndipo wakahamia Singida kama nilivyokuhadithia hapo awali.
Pale Ugunda kulitapakaa sime za Vahumba waliouwawa, na kwa kuwa wahehe huita sime Mage, mahala pale pakaitwa Image mpaka hivi leo.
Vanyangologo waliendelea na safari yao ya kusaka watu weupe huku wakiacha ndugu zao wengine kuwaangalia majeruhi pale Image. Safari hiyo ya kuwaska na kuwauwa watu weupe iliendelea mpaka Ilongo, Ubena, na hata Ukimbu.
Kitu cha ajabu ni kuwa Vahumba hawa hawakushughulika na Vakilwa, hivyo Vakilwa walikuja kuanza kutawala sehemu nyingi ambazo hawakuguswa.
Wale Vanyangologo waliobaki Image walianza mahusiano na wanawake wa Usagala, Hivyo katika sehemu za Image na Ilole kukawa na koo za wahehe ambao wanafanana na Wamasai kwa umbo, na sura zao za kuchongoka.
Wengi hukataa kuwa asili ya kizazi chao ni  Vahumba lakini wanadai asili yao ni Hamitic. Lakini Humma maana yake ni Hamitic. Akina Ngimba wa Ilole asili yao ni Vahumba. Itakumbukwa kuwa  mama mzazi wa Mutwa Mkwava alikuwa Sengimba.
Ukoo wa akina Sambala asili yao ni Wahamitic, hata mwitiko au mwidikiso wao ni Mugonanzi , maana yake mwenye kulala sehemu mbalimbali au mhamaji, kwa Kiingereza tungesema nomad na hiyo ndiyo ilikuwa sifa ya Vahuma.
Wale wasagala weupe hawakukwepa kusakwa na Wahumba, wengine wao walikimbilia Wota kwa kuvuka Lyambangali,hawa wakaja kujiita  Mlowoka. Kuna walowoka wengine walikuja kurudi Uheheni  kama ukoo wa Fivawo na Makombe wa Tanangozi na Iwawa. Mliotajwa mnasemaje?

 

 

 

 


Sunday, July 31, 2022

UNAJUA KUWA ZAMANI MHEHE MWANAUME AKIFA ANAZIKWA NA MKEWE ALIYE HAI?


 

Kama nilivyoeleza katika makala zilizopita, wale  watu weupe waliowatimua Wategeta walikuwa pia wakifanya biashara ya kuuza watumwa. Koo nyingi za Kihehe hazikukubali kuuuzwa hivyo wengine waliona heri wauwawe, wengine waligoma kula hivyo kufa wakiwa katika masafara wa kuelekea pwani, na wengine walikimbia mbali kutoka maeneo yao ya asili.
Tuliona jinsi kabila la  Wanyakyusa lilivyopatikana kutokana na kusambaratika huko. Wagogo pia ni kabila lilitokana na fujo hizo. Koo mbalimbali za Wahehe walikimbilia kaskazini na kufika mpaka sehemu inaitwa Mkofa kando ya mto Lyambangali,  wakawa wanatafuta namna ya kuvuka kwenda upande wa pili, sehemu moja wakakuta gogo kubwa limeanguka na kulala juu ya mto na kutengeneza aina ya daraja, hivyo wakaweza kuvuka kumkimbia adui, kwa kukumbuka kuvuka huko, wahehe wale walijiita Vanyagogo, jina ambalo baadae likafupishwa kuwa Wagogo.
Wagogo wengi kwa kukumbuka walikotoka huwaita Wahehe wajomba zao. 
Kuna simulizi za kale kuwa Warangi walitokana na watu watu weupe waliohamia Uheheni  kutoka Usambara.
Wakati ule koo kadhaa zilizokuwa zikiishi karibu na bahari ya Hindi zilijikuta zikiwa na machotara wengi wa Kiarabu na baadae waKireno. Watu hawa weupe toka Usambara walikuja kuishi sehemu ya Ugunda iliyokuwa ikiitwa Ilamba na wengine kuhamia Usagala.
 Kuna Wasagala wa zamani walikuwa weupe na wanaume wakawa na nywele nyingi mikononi na kifuani na walikuja kuwa na muitiko au mwidikiso wa Mnyakami, inawezekana walikuwa na  uhusiano na Wakami wa Ulugulu. Hawa watu weupe walienea  sehemu nyingi za Uhehe, Ubena na Ukimbu.  Wale waliobaki Ugunda, Wahehe walianza kuwaita Valangi. Valangi  hawa na ndugu zao Wanyiramba walikuja kuhamia maeneo ilipo Singida sasa. Kuna wakati wajukuu wa Valangi hawa waliamua kurudi kwao Uheheni, lakini karibu na Dodoma wakakutana na ukoo wa Wadongwe waliokuwa chini ya Kiongozi wao Muyovela, vita kali ikaanza  wakashindwa na wakalazimika kukimbilia ilipo Kondoa sasa na huko wakaishi na kuongezeka na kuwa kabila kubwa.
Makundi mengine ya watu weupe  yalisonga mbele mpaka Ukimbu,  kundi jingine likahamia sehemu za Ilembula, kundi jingine likahamia kwa muda sehemu za Wasa, kisha kuelekea Malangali.
Kundi hili ndilo linalosemekana liliingiza kilimo cha kulima mahala kwenye majani kwa kugeuza udongo na kutengeneza matuta kwa kufukia majani. Majani yale yaliachwa kwa muda ili yaoze na kisha ndipo mbegu hupandwa.
Kilimo hiki kilileta mazao mengi, killimo hiki kiliitwa Malongo, na sehemu ile ya malangali ikaitwa Ilongo.  
Wahehe huita mavuno mengi kuwa ni Sanga. Katika sehemu hiyo ya Ilongo kukaweko na kundi fulani la wakulima waliokuwa hodari wa kulima malongo na hivyo kuwa wanapata mavuno mengi wakaanza kuitwa Vanyasanga, mafanikio ya Vanyasanga yakwaletea maadui na wakaamua kuhamia sehemu za Ukinga na Uwanji, na ndio chanzo cha koo za Sanga huko Ukinga na Uwanji.
Ukoo wa Kihaule pia husema walitokea Ilongo, na hata mwitiko wa binti wa kina Kihaule ni Nyamalongo. Wazee wa Upangwa husema kina Kihaule wa kwanza kuingia huko walikuwa weupe na walileta kilimo cha malongo, pia ndio waliokuja kusitisha mila ya kumzika mke akiwa mzima mzima kama mumewe amefariki, mila hii hata Wahehe awali  walikuwa nayo. 

Saturday, July 30, 2022

WANYAKYUSA WALITOKA UHEHENI

 


Vanu velu au watu weupe waliotoka Kilwa waliingia nchi ya Uheheni kwa amani na wakaendelea kuishi kwa amani na hatimae kuwa sehemu ya wenyeji, mfano nilioutoa ni wakina Kiwhele. 

Lakini kuna kundi jingine la watu weupe hawa waliingia kutoka kaskazini na kuingia katika eneo lililoitwa Ugunda, wenyeji wa Ugunda walikuwa ni Wategeta, habari zao nilikwisha zizungumzia awali. Jina la Ugunda lilitokana na babu yao mmoja aliyeitwa Mugunda.  Eneno la Ugunda kwa sasa linaitwa Image na tutaelezana chanzo cha jina hilo baadae. Kama mnakumbuka, niliwaeleza kuwa Wategeta walikuwa wafua chuma wazuri sana na walikuwa watu walioishi kwa mpangilio mzuri katika kazi yao hiyo, pia niliwaambia kuwa walikuwa ni watu wenye maungo makubwa yenye afya hawakuwa watu wa mchezo. Kuna kundi moja la Wahumma kutokea aidha Pawaga au Izazi, liliwashambulia Wategeta hawa ili kuwanyang’anya ng’ombe. Pamoja na Wahuma kuwa na silaha za kutisha ,Wategeta waliwakamata adui zao hao kwa mikono  na kuanza kuwachanachana vipande. Walimbakiza Muhumba mmoja tu nae walikata masikio wakamwachia aende kwao akahadithie. Baada ya hapo Wategeta wakawa mara kwa mara wanawashambulia Wahuma na kuwanyang’anya ng’ombe bila upinzani mkubwa. 
 
Lakini hili kundi la watu weupe kutoka kaskazini liliwazidi sana nguvu Wategeta. Wenyeji wengi wakalazimika kukimbia nchi yao na kukimbilia upande wa iliko Pawaga sasa, wale maadui waliwafwata mpaka huko na kuwamaliza na waliobaki kuwachukua watumwa na kwenda kuwauza Pwani. Mahala palipokamilisha vita hiyo palikuja kuitwa Malikilo maana yake pa kumalizia. Siku hizi panaitwa Kidali.

Wategeta wengine walikimbia kaskazini na kufika mpaka ulipo sasa mpaka wa Kenya na Uganda. Huko wakalikuta kabila la Wasamia na kuwashinda na kuwa watawala wao. Hata siku hizi wajukuu zao hujiita Bahehe na kusema kuwa babu zao walitokea Uheheni. Kundi jingine la Wategeta lilikimbilia Mahenge na baadae kuanza kufuata bonde la  Kilombelo kisha kuingia Ubena na kuendelea na safari hadi Kaskazini mwa Ziwa Nyasa, wakaanza kuishi sehemu waliyoiita Kavala, maana yake  peupe penye kuwaka jua, wakaendelea na kazi yao ya asili ya uhunzi. Wengi wao walikuwa wa ukoo wa kina Chusi na wakawa watawala, jina lao likageuka kuwa Chusa,  Wagonde wakaligeuza jina hilo kuwa Wanyachusa, au Wanyakyusa. Kuna Wanyakyusa ambao hatimae walirudi Uheheni kwa mfano ukoo wa akina Kalinga, hawa walitumia majina kama Kwilengilyova, yaani maji yangurumayo, wakikumbuka  maporomoko ya maji katika sehemu walizopita wakati wakisafiri wakifuata bonde la Kilombelo. Wengine wakijiita Magalamatitu, wakikumbuka sehemu ambapo kulikuwa tambarare  ya  ndege wengi weusi ambayo ipo mpaka leo. Hawa watu weupe waliowafukuza Wategeta waliacha uzao wao katika nchi ya Usagala. Wajukuu hawa wa Wasagala wa zamani, ambao hujulikana kama Vanyikami, huwa na madai tofauti, wengine wakidai kuwa asili yao ni waarabu, wengine wakidai asili yao ni wazungu. Wanahistoria wengi huona hiyo si rahisi kwani wangekuwa Waarabu, lazima wangeanzisha dini ya Kiislamu na hali kadhalika wangekuwa wazungu kungeletwa pia ukristu. Kinachodhaniwa ni kuwa Vanu velu hawa walikuwa ni machotara au watu tu wenye ngozi angavu.

UNAJUA WAHEHE WALITOKEA WAPI 2 ? marekebisho

 


Wabena ndio chanzo cha Wahehe. Inasemekana jina la kabila hili lilitokana na kutofautiana katika mshangao na kabila lao mama la Wabena. Wahehe walikuwa wakishangaa kwa kusema He he, Wabena walikuwa wakishangaa kwa kusema khe khe. Baadaye Wahehe walitumia sauti hiyo hata wakati wakiwa vitani. Kama nilivyosema katika sehemu ya kwanza ya simulizi hii, makundi mawili ya wabena yaliondoka Nyumbanitu na kuelekea Kaskazini mashariki na kuja  kuishi kwa muda Magharibi mwa ilipo Malangali sasa.  Lakini tena kukaweko na mgawanyiko, kundi moja lilielekea  bonde la Lyambangali na kuanzisha  kabila la Wasangu , wakati kundi jingine likielekea upande wa pili na hili likaja kuwa chanzo cha Wahehe. Katika kugawanyika huku, sehemu waliyoanzia kugawanyika ikaitwa  Igawilo maana yake penye kugawa nchi. 

Kama ilivyokuwa katika tabia za Kibantu watu hawa waliokuja kuitwa Wahehe awali waligawanyika katika koo mbalimbali, japo inasemekana walikwisha anza kujitambulisha kama Wahehe.  Kati ya  koo  maarufu walikuweko  akina;  
Vigawilo – Hawa ni wale waliobaki pale Igawilo,   na baadae wengine wakaaza kusambaa katika bonde la Lyandembela na kuanza kuitwa Vilongo. Mwiko wao hawa ulikuwa bandama, jamaa wa ukoo huu ni akina Kibodya na Mugandu.
Vahafiwa – hawa walienea katika sehemu zinazoitwa siku hizi Tanangozi, welu, kalenga Ntsihi, na maeneo yanayozunguka mji wa Iringa.

Kuna wakati maeneo haya yalipata uhaba mkubwa wa mvua hivyo kukawa na njaa na hata watu wengi  wakafa kwa njaa, waliosalimika walikuja kupata mwidikiso wa  Vahafiwa maana yake waliofiwa na wengine walikuwa na mwidikiso wa Mponela yaani aliyepona njaa. 

Wengine walikuja kuitwa Vanyalugome kwa sababu ya desturi yao ya kutengeneza mitego ya wanyama kwa  kuchimba mahandaki.

Mwiko wao hawa ilikuwa ni nyopolwa, Yaani mimba ya mnyama yoyote.

Labda niseme hapa hapa kuwa mwiko maana yake hawaruhusiwi kamwe hata kuonja nyama hiyo.

Kati ya koo zinazojulikana kutoka kundi hili ni akina Mugovano, Mukemangwa na mutono,

Vanyandevelwa- maana yake wepesi kuchokozwa, makazi ya kundi hili yalikuwa kati ya barabara mbili zilizoanzia Iringa, yaani ile ya kwenda  Dar es Salaam na ile ya kwenda Dodoma

.Awali nao mwiko wao ulikuwa nyopolwa lakini walikuja kunyangwa nchi na kundi lililoitwa Vanyamahuvi na kuja kutawaliwa nao.

 Hawa Wanyamahuvi wakaja kutwaa jina la Vanyandevela lakini wakaendeleza mwiko wao ambao ni ndege kanga, Ni vigumu siku hizi kupambanua nani ni Mnyandevela wa awali na nani Mnyamahuvi wa awali

Vategeta hawa walikuwa na umuhimu sana katika kabila la wahehe kwani walikuwa mafundi wa kufua chuma.

Wategeta ndio waliounda mikuki, mundu shoka na kadhalika. Wategeta waliishi karibu na kila ukoo wa Wahehe na hasa sehemu zenye mchanga uliweza kutoa chuma, wengi walikuwa warefu wenye maungo yenye afya na hivyo basi waliweza kufikia kutawala katika sehemu nyingi walizokuwa wakiishi.

Wategeta waligawana kazi, walikuwa na sifa ya kuwa wana mipangilio katika maisha yao.  Wale waliokuwa mabingwa wakutafuta kuni kwa ajili ya mkaa wa kuyeyushia chuma waliitwa Vanyantsagala …nzagala ni kuni, baadae walikuja kufupishwa na kuitwa Wasagala.

 Wategeta ambao walikuwa na utaalamu wa kuchagua mchanga bora kwa chuma waliitwa Vayunga, ambao ndio chanzo cha Watsungwa. Kutokana  majina haya walipoenea na kuwa wengi sehemu waliyoenea Vayunga ikaitwa Utsungwa na walikoenea Wasagala ikaitwa Usagala.

 Mwiko wa Wategeta ni mato kwa Kiswahili mbawala na wengine mwiko wao ni dundulu yaani twiga. Inasemekana waliamini kuwa kwa kula nyama ya wanyama hao  wangepata ukoma ,kwani ngozi ya binadamu huwa na mabaka meupe kama twiga, kama ameambukizwa ukoma.

Kati ya koo za Wategeta maarufu ni Chusi na kina Mveyange

Wakilwa,,, hawa waliitwa hivi kwa kuwa walitokewa Kilwa na kuingia sehemu inayoitwa siku hizi Mufindi kwenye robo ya kwanza  ya karne ya 16. Yaani mwaka 1500. Hawa hawakutokana na Wabena kama Wahehe wengine.

Hawa walikuwa na ngozi ya maji ya kunde na walikuwa na nywele nyingi mikononi na kifuani.  Nywele ambazo Wahehe huziita Lyagi,hivyo Wakilwa pia wakaaitwa Vanyalyagi. Dalili hizi ziliwatofautisha na wabantu wengine. Inasemekana walipokuwa badi Kilwa, walichanganyika na Wareno na Washirazi waliokuwa tayari wametua Kilwa wakati huo.

Kati ya Wakilwa wa Uheheni ni akina Kihwele ambao walipoenea Uheheni walionyesha kutengeneza vifaa vya chuma bora kuliko Wategeta.  Huko Katanga Kongo kuna ukoo unaitwa Kiwele, na kuna uwezekano kuwa ni ndugu wa Kihwele wa Uheheni kwani wote walikuwa wakizika wafu wao kichwa kikielekea mashariki, kwa kukumbuka kwao  Kilwa, ambayo iko mashariki mwa Katanga na Uhehe pia,


STAT COUNTER