Kama
nilivyoeleza katika makala zilizopita, wale
watu weupe waliowatimua Wategeta walikuwa pia wakifanya biashara ya
kuuza watumwa. Koo nyingi
za Kihehe hazikukubali kuuuzwa hivyo wengine waliona heri wauwawe, wengine
waligoma kula hivyo kufa wakiwa katika masafara wa kuelekea pwani, na wengine
walikimbia mbali kutoka maeneo yao ya asili.
Tuliona jinsi kabila la Wanyakyusa lilivyopatikana kutokana na
kusambaratika huko. Wagogo pia ni kabila lilitokana na fujo hizo. Koo
mbalimbali za Wahehe walikimbilia kaskazini na kufika mpaka sehemu inaitwa
Mkofa kando ya mto Lyambangali, wakawa
wanatafuta namna ya kuvuka kwenda upande wa pili, sehemu moja
wakakuta gogo kubwa limeanguka na kulala juu ya mto na kutengeneza aina ya
daraja, hivyo wakaweza kuvuka kumkimbia adui, kwa kukumbuka kuvuka huko, wahehe
wale walijiita Vanyagogo, jina ambalo baadae likafupishwa kuwa Wagogo.
Wagogo wengi
kwa kukumbuka walikotoka huwaita Wahehe wajomba zao.
Kuna
simulizi za kale kuwa Warangi walitokana na watu watu weupe waliohamia
Uheheni kutoka Usambara.
Wakati ule
koo kadhaa zilizokuwa zikiishi karibu na bahari ya Hindi zilijikuta zikiwa na
machotara wengi wa Kiarabu na baadae waKireno. Watu hawa weupe toka Usambara
walikuja kuishi sehemu ya Ugunda iliyokuwa ikiitwa Ilamba na wengine kuhamia
Usagala.
Kuna Wasagala wa zamani walikuwa weupe na
wanaume wakawa na nywele nyingi mikononi na kifuani na walikuja kuwa na muitiko
au mwidikiso wa Mnyakami, inawezekana walikuwa na uhusiano na Wakami wa Ulugulu. Hawa watu
weupe walienea sehemu nyingi za Uhehe, Ubena
na Ukimbu. Wale waliobaki Ugunda, Wahehe
walianza kuwaita Valangi. Valangi hawa
na ndugu zao Wanyiramba walikuja kuhamia maeneo ilipo Singida sasa. Kuna wakati
wajukuu wa Valangi hawa waliamua kurudi kwao Uheheni, lakini karibu na Dodoma wakakutana
na ukoo wa Wadongwe waliokuwa chini ya Kiongozi wao Muyovela, vita kali
ikaanza wakashindwa na wakalazimika
kukimbilia ilipo Kondoa sasa na huko wakaishi na kuongezeka na kuwa kabila
kubwa.
Makundi
mengine ya watu weupe yalisonga mbele
mpaka Ukimbu, kundi jingine likahamia
sehemu za Ilembula, kundi jingine likahamia kwa muda sehemu za Wasa, kisha
kuelekea Malangali.
Kundi hili
ndilo linalosemekana liliingiza kilimo cha kulima mahala kwenye majani kwa
kugeuza udongo na kutengeneza matuta kwa kufukia majani. Majani yale yaliachwa
kwa muda ili yaoze na kisha ndipo mbegu hupandwa.
Kilimo hiki
kilileta mazao mengi, killimo hiki kiliitwa Malongo, na sehemu ile ya malangali
ikaitwa Ilongo.
Wahehe huita mavuno
mengi kuwa ni Sanga. Katika
sehemu hiyo ya Ilongo kukaweko na kundi fulani la wakulima waliokuwa hodari wa
kulima malongo na hivyo kuwa wanapata mavuno mengi wakaanza kuitwa Vanyasanga, mafanikio ya Vanyasanga yakwaletea maadui na wakaamua
kuhamia sehemu za Ukinga na Uwanji, na ndio chanzo cha koo za Sanga huko Ukinga
na Uwanji.
Ukoo wa Kihaule pia husema walitokea Ilongo,
na hata mwitiko wa binti wa kina Kihaule ni Nyamalongo. Wazee wa Upangwa husema
kina Kihaule wa kwanza kuingia huko walikuwa weupe na walileta kilimo cha
malongo, pia ndio waliokuja kusitisha mila ya kumzika mke akiwa mzima mzima
kama mumewe amefariki, mila hii hata Wahehe awali walikuwa nayo.
Sunday, July 31, 2022
UNAJUA KUWA ZAMANI MHEHE MWANAUME AKIFA ANAZIKWA NA MKEWE ALIYE HAI?
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment