Wabena ndio chanzo cha Wahehe. Inasemekana jina la kabila hili lilitokana na kutofautiana katika mshangao na kabila lao mama la Wabena. Wahehe walikuwa wakishangaa kwa kusema He he, Wabena walikuwa wakishangaa kwa kusema khe khe. Baadaye Wahehe walitumia sauti hiyo hata wakati wakiwa vitani. Kama nilivyosema katika sehemu ya kwanza ya simulizi hii, makundi mawili ya wabena yaliondoka Nyumbanitu na kuelekea Kaskazini mashariki na kuja kuishi kwa muda Magharibi mwa ilipo Malangali sasa. Lakini tena kukaweko na mgawanyiko, kundi moja lilielekea bonde la Lyambangali na kuanzisha kabila la Wasangu , wakati kundi jingine likielekea upande wa pili na hili likaja kuwa chanzo cha Wahehe. Katika kugawanyika huku, sehemu waliyoanzia kugawanyika ikaitwa Igawilo maana yake penye kugawa nchi.
Kama ilivyokuwa katika tabia za Kibantu watu
hawa waliokuja kuitwa Wahehe awali waligawanyika katika koo mbalimbali, japo
inasemekana walikwisha anza kujitambulisha kama Wahehe. Kati ya koo maarufu walikuweko akina;
Vigawilo –
Hawa ni wale waliobaki pale Igawilo, na baadae wengine wakaaza kusambaa katika bonde la
Lyandembela na kuanza kuitwa Vilongo. Mwiko wao hawa ulikuwa bandama, jamaa wa
ukoo huu ni akina Kibodya na Mugandu.
Vahafiwa –
hawa walienea katika sehemu zinazoitwa siku hizi Tanangozi, welu, kalenga
Ntsihi, na maeneo yanayozunguka mji wa Iringa.
Kuna wakati
maeneo haya yalipata uhaba mkubwa wa mvua hivyo kukawa na njaa na hata watu
wengi wakafa kwa njaa, waliosalimika
walikuja kupata mwidikiso wa Vahafiwa
maana yake waliofiwa na wengine walikuwa na mwidikiso wa Mponela yaani
aliyepona njaa.
Wengine
walikuja kuitwa Vanyalugome kwa sababu ya desturi yao ya kutengeneza mitego ya
wanyama kwa kuchimba mahandaki.
Mwiko wao
hawa ilikuwa ni nyopolwa, Yaani mimba ya mnyama yoyote.
Labda niseme
hapa hapa kuwa mwiko maana yake hawaruhusiwi kamwe hata kuonja nyama hiyo.
Kati ya koo
zinazojulikana kutoka kundi hili ni akina Mugovano, Mukemangwa na mutono,
Vanyandevelwa-
maana yake wepesi kuchokozwa, makazi ya kundi hili yalikuwa kati ya barabara
mbili zilizoanzia Iringa, yaani ile ya kwenda
Dar es Salaam na ile ya kwenda Dodoma
.Awali nao
mwiko wao ulikuwa nyopolwa lakini walikuja kunyangwa nchi na kundi lililoitwa
Vanyamahuvi na kuja kutawaliwa nao.
Hawa Wanyamahuvi wakaja kutwaa jina la
Vanyandevela lakini wakaendeleza mwiko wao ambao ni ndege kanga, Ni vigumu siku
hizi kupambanua nani ni Mnyandevela wa awali na nani Mnyamahuvi wa awali
Vategeta
hawa walikuwa na umuhimu sana katika kabila la wahehe kwani walikuwa mafundi wa
kufua chuma.
Wategeta
ndio waliounda mikuki, mundu shoka na kadhalika. Wategeta waliishi karibu na
kila ukoo wa Wahehe na hasa sehemu zenye mchanga uliweza kutoa chuma, wengi
walikuwa warefu wenye maungo yenye afya na hivyo basi waliweza kufikia kutawala
katika sehemu nyingi walizokuwa wakiishi.
Wategeta
waligawana kazi, walikuwa na sifa ya kuwa wana mipangilio katika maisha
yao. Wale waliokuwa mabingwa wakutafuta
kuni kwa ajili ya mkaa wa kuyeyushia chuma waliitwa Vanyantsagala …nzagala ni
kuni, baadae walikuja kufupishwa na kuitwa Wasagala.
Wategeta ambao walikuwa na utaalamu wa
kuchagua mchanga bora kwa chuma waliitwa Vayunga, ambao ndio chanzo cha
Watsungwa. Kutokana majina haya
walipoenea na kuwa wengi sehemu waliyoenea Vayunga ikaitwa Utsungwa na walikoenea
Wasagala ikaitwa Usagala.
Mwiko wa Wategeta ni mato kwa Kiswahili
mbawala na wengine mwiko wao ni dundulu yaani twiga. Inasemekana waliamini kuwa
kwa kula nyama ya wanyama hao wangepata
ukoma ,kwani ngozi ya binadamu huwa na mabaka meupe kama twiga, kama ameambukizwa
ukoma.
Kati ya koo
za Wategeta maarufu ni Chusi na kina Mveyange
Wakilwa,,,
hawa waliitwa hivi kwa kuwa walitokewa Kilwa na kuingia sehemu inayoitwa siku
hizi Mufindi kwenye robo ya kwanza ya
karne ya 16. Yaani mwaka 1500. Hawa hawakutokana na Wabena kama Wahehe wengine.
Hawa
walikuwa na ngozi ya maji ya kunde na walikuwa na nywele nyingi mikononi na
kifuani. Nywele ambazo Wahehe huziita
Lyagi,hivyo Wakilwa pia wakaaitwa Vanyalyagi. Dalili hizi ziliwatofautisha na
wabantu wengine. Inasemekana walipokuwa badi Kilwa, walichanganyika na Wareno na Washirazi waliokuwa
tayari wametua Kilwa wakati huo.
Kati ya Wakilwa wa Uheheni ni akina Kihwele ambao walipoenea Uheheni walionyesha
kutengeneza vifaa vya chuma bora kuliko Wategeta. Huko Katanga Kongo kuna ukoo unaitwa Kiwele,
na kuna uwezekano kuwa ni ndugu wa Kihwele wa Uheheni kwani wote walikuwa
wakizika wafu wao kichwa kikielekea mashariki, kwa kukumbuka kwao Kilwa, ambayo iko mashariki mwa
Katanga na Uhehe pia,
No comments:
Post a Comment