Pages

Sunday, April 4, 2010

Consolata Primary School 3

Bado mpaka leo najaribu kupeleleza maneno halisi ya wimbo fulani tuliofundishwa na waalimu wa mazoezi wakati huo nikiwa darasa la nne. Tuliambiwa ni wimbo wa kiingereza tuliuimba hivi
My way, may way is cloudy my way God send ze chelenjez down
zea iz fire in ze east and fire in ze west
fire in ze chelenjez da
For God has sent his chelenjez down, God sent his chelenjez down, my lovely

Siku nikigundua mwalimu alitufundisha nini nitafurahi sana. Jumapili ililazimu kuja misa ya pili na baada ya hapo kuripoti shuleni kuitwa majina na kufundishwa nyimbo mpya, ole wako usije utakumbana na mwalimu Daudi Jumatatu. Kwa hiyo kulikuweko na zamu za kutumikia kanisani, wengine kwenda kuuza magazeti ya Kiongozi na Mwenge nje ya kanisa nk.Siku ya kufunga shule, hasa mwisho wa mwaka ilikuwa na sura nyingi sana. Shule nzima na wazazi wenu mnakusanyika yanaanza kutajwa majina ya wanaopanda darasa. Mwalimu wa darasa anasimama na karatasi na kuanza kusoma, "Hawa ndio wanapanda darasa tutasoma kufuatia maksi zao, wa kwanza Naboth Mbembati(siku hizi Doctor Muhimbili)", watu wote heeeeeeeeeeeeeeeeeeee, "Wa pili Emmanuel Mkusa(Yuko Namibia bingwa wa mahesabu huyo)"...watu wote heeeeeeeeeeeeeeeeeeee. Itaendelea mpaka kufika na hawa ndio walioobunda..haya wasimame wanatajwa majina na kuzomewa yuuuuuuuuuuuuuuuuuu. Hapo sasa bado kipigo cha wazazi kinakungojea na kejelei ya shule nzima kwa likizo nzima na mwaka mzima unaofuatia kwa kuwa darasa la nyuma. Mwalimu Mkuu akitangaza shule imefungwa, kulikuwa nambo mengi yanatokea, kulikuweko na watu wanakimbia haraka toka eneo la shule, siku hii ilikuwa ya malipo, ngumi zilikuwa zinaumuka kila kona, huyu anadaiwa gololi, yule hajalipa mikusu , mwingine alimnyima mwenzie kashata. Basi ukisikia 'Ngumi ngumi" unakimbilia kuona kuna nini na siku hiyo haziamuliwi mpaka atandikwe mtu. Likizo ilikuwa raha sana mambo mengi ya kufanya,kutengeneza baiskeli za miti, magari ya maberingi, kwenda Itamba kuiba maembe, kuwinda vindege na manati, na hii ilikuwa kwanza ukisha tengeneza manati yako unafanya chini juu umpige mbayuwayu, halafu unajichanja kisha unapaka damu yake ilijulikana hiyo inakufanya uwe na shabaha sana. Pamoja na kula matunda mengi ya porini na vindege siku ya bahati mnapata sungura ililazimika uweke nafasi ya kula nyumbani kwa sababu ole wako ufike nyumbani useme umeshiba , ikijulikana ulikula kwa watu ni kipigo tu.

Consolata Primary School 2

Waalimu kipindi hicho walihakikisha sheria zinafuatwa haswa, na kiboko kilitembea haraka sana kwa wakorofi. Mwanafunzi aliyekuwa na nguvu kuliko wote hapo shuleni aliitwa Odongo, na huyo ndiye aliyekuwa na kazi ya kuwafukuza wale ambao walikuwa wakikimbia adhabu. Siku moja kundi la wanafunzi walipanga kumuua mwalimu mmoja aliyekuwa na sifa ya ukali sana. Mmoja wa wanafunzi alikuwa ametuhadithia kuwa bibi yake kamwambia kuwa ukikaanga mchanga wa unyao wa mtu anakufa. Msako wa mchanga wa unyao wa mwalimu ulianza. Wakati huo eneo lote la shule mpaka kanisani palikuwa pamemwagwa kokoto hivyo ikawa ngumu kupata unyayo wa mwalimu. Bahati mbaya zaid mwanafunzi mmoja akapata uwoga akamtaarifu mwalimu kuhusu mpango huo wa 'muder'. Loh wakati tuko katikati ya kipindi kengele ikalia shule nzima tukaambiwa foleeeeni. Tukiwa mbele ya shule wakaanza kuitwa majina wote walioshiriki katika kupanga hiyo masta plani. Wote wakatandikwa viboko halafu mwalimu akawapa mchanga wenye unyayo wake akawambia sasa wakakaange vizuri.
Kila alhamisi mchana ililazimu kutoroka shule na kwenda stendi ya mabasi ambayo wakati huo iliwa eneo lilipo soko. Soko lilikuweko ule upande unaoangaliana na kanisa la Kilutheli. Hili la huku juu limejengwa ilipokuwa stendi. Siku ya alhamisi mchana kulikuwa na basi la DMT lililokuwa linatoka Malawi, wakati huo kukiitwa Nyasaland. Huko kulikuwa na mganga aliyekuwa akiogopwa sana jina lake Chikanga, yeye alikuwa na sifa ya kuwatoa uchawi wachawi na kisha kuwanyoa. Kazi yetu ilikuwa kuangalia abiria mwenye kipara hapo ni mawe makopo tu, na wengi walikuwa wakikimbilia kituo cha polisi ambacho kipo hapo toka enzi za ukoloni.

Consolata Primary School

Barabara Mbili
Jiwe la adhabu nje ya shule ya Chemchem
Katika kipindi nilipokuwa nasoma, Consolata aka Chemchem, eneo lote linaloitwa Frelimo lilikuwa pori tu, palikuwa na njia ya mkato toka hapo shuleni mpaka Makorongoni. Nilikuwa nikiishi Barabara Mbili kwenye nyumba ambayo kwa sasa ni kilabu cha pombe. Wakati huo kulikuwa na wenzetu wanakaa Nduli ambao nao walikuwa wanawahi kila siku kuja shule asubuhi saa moja na nusu.Ukichelewa prefect alikuwa anaandika majina, prefect mmoja ambaye sasa ni mkuu fulani, alikuwa bingwa wa kupokea hongo yamatunda kama mitoo, misasati, na mifudu na mahindi ya kuchoma ili asikuandike jina ikiwa umechelewa. Moja ya adhabu mbaya ilikuwa ni kupewa nyundo na kuligonga jiwe lililopo kwenye uwanja wa shule, mwalimu alitakiwa awe anasikia akiwa darasani, kwa kawaida baada ya kugonga dakika kumi ilikuwa kama unajigonga ndani ya kichwa. Kati ya starehe za wakati huo ilikuwa ni kuogelea katika kisima kilichokuwa kwenye makutano ya barabara itokayo stendi na ile iendayo Ilala, wakati huo hapo ilipo stendi palikuwa ni makaburi tu. Starehe nyingine ilikuwa ni kutengeza bunduki zilizoitwa Nyongamembe, au kuteremka Ruaha kwa ajili ya kuchuma mitoo,misasati na mifudu na kuogelea kuvua samaki na kutengeneza kamba za katani kwa kuzileta shule kwenye kipindi cha Maarifa ya Nyumbani. Adhabu ya kufungiwa darasa zima kutokwenda kula mchana nayo ilikuwa maarufu sana.
Nakumbuka hapo mtaani barabara mbili tulianzisha bendi kama zile za shule kwa kuwamba ngoma sisi wenyewe. Ila tuliwahi kuibiwa ngozi na mwalimu mmoja wa shule ya chini ya mti ambaye wote tulikuwa tunamuogopa kwani aliwahi kujaribu kujinyonga chooni kamba ikakatika akawa kama zezeta fulani lakini hiyo shule ya chini ya mti imekuwa shule maarufu mpaka leo.

Hapo zamani za kale 2

Madirisha matatu ya kwanza ni darasa la 1A na 1B

Raha ya shule enzi hizo kwanza ni hadithi za kutisha kama zile za mazimwi, mbwa mwitu, na ujanja wa sungura. Hakuna kusahau jinsi Wagagagigikoko walivyoweza kunitokea ndotoni. Muda wa kupumzika ,ambao pale Chechem ulijulikana kama pausi (pause????) ulitawaliwa na kila aina ya michezo kama vile 'mbinga, gololi, kiboleni, mdako... huku biashara ya misasati, mifudu, mafulusadi zikiendelea.
kulikuwa natatizo moja pale Mlandege, kile choo cha wasichana tuliambiwa kina jini, na ilikuwa lazima uvuke hapo kwenda choo cha wavulana, na kumbuka wakati huo nyuma ya choo cha wavulana kulikuwa na pori kubwa si leo ambapo kumezungukwa na nyumba. Dawa ilikuwa kujitahidi usilazimike kwenda chooni wakati wa vipindi maana utakuwa nje peke yako na jini. Choo cha mbele ni cha wasichana na nyuma ni cha wavulana
Watu wengi waliamua kukojoa darasani kuliko kukutana na jini

Hapo zamani za kale

Nimezaliwa Iringa, wazazi wangu wote walikuwa waalimu. Baba alikuwa akifundisha Iringa Middle School, (iliyoitwa baadae Mshindo Primary School), ambayo wenye akili fulani katika miaka ya sabini, waliamua ivunjwe ili ujengwe uwanja wa Samora. Ilikuwa ndio shule inayofuata baada ya mwanafunzi kumaliza Government Primary School, inayoitwa sasa Mlandege Primary School. Goverment iliishia darasa la nne, na Middle School ilianza darasa la tano hadi la nane. Mama alikuwa mama mendeleo na baadae akafundisha Aga Khan primary,(Shabaha Primary ambayo nayo haipo tena majengo yake yamechukuliwa na Lugalo sekondari). Na pia alifundisha St Mary's secondary , ambayo sasa ni Iringa Girls.
Nakumbuka kuanza shule Mlandege darasa la kwanza ambapo madarasa yalikuwa na makundi mawili 1A, na 1B. Nilikuwa 1B mwalimu wetu alikuwa Mwalimu Chitigo, wakati 1A walikuwa wanafundishwa na Mwalimu Mary. Mwalimu Mkuu alikuwa mwalimu George Nyakunga, ambaye bahati mbaya alifariki mapema miaka hiyo hiyo. Namkumbuka Mwalim George akituita na kutugawia uniform zetu ambazo siku hizo zilikuwa zinashonwa na fundi maalumu wa shule. Kisha nikahamia Consolata Primary ambayo leo inaitwa Chemchem, nikakutana na mwalimu Daudi Luhanga, Mwalimu Kalinga, Mwalimu Filangali, Mwalimu Mkuu akiwa Mwalimu Mwinuka. Kwa kipindi cha mwaka baba alihamia Mbeya nikasoma Aga Khan Mbeya, kisha kurudi Iringa ambapo nilisoma Aga Khan Primary wakiwemo waalim kama Mrs Saleh ambaye hadi sasa anaendesha mgahawa unaitwa Hasty Tasty, mwalim Daya, mwalimu Pabani, mwalimu mkuu akiwa Mr Thakore, kisha nilijiunga Aga Khan Secondary chini ya mwalimu Mkuu Mr Sheikh na baadae Mr Ntemo, na Mr Hassan, mwisho Iringa Teachers training Centre- Klerruu College of National Education., hapa Principal alikuwa Mzee Basimaki, ambae baadae alifuatiwa na Mr Kilimuhana. Wakufunzi wengi wa hapa walipanda sana katika serikali kuu. Mr Halinga aliwahi kuwa Mbunge Mbozi, Mr Mwanga alikuja kuwa Waziri wa Utumishi, Mh Ngw’andu waziri wa Sayansi na Technolojia.


STAT COUNTER