Jina Iringa lilitokana na neno la Kihehe Lilinga ambalo tafsiri yake kwa Kiingereza ni Observation Post. Wahehe walianzisha lilinga sehemu hii ilipo Iringa ya sasa, ilikuweza kuwaona maadui kwa urahisi na kuweza kutoa taarifa za kulinda Ikulu iliyokuweko Kalenga. Wajerumani walijenga Boma juu ya kilima hicho hicho baada ya ushindi uliopatikana baada ya kupigana na Wahehe kwa mara ya pili. Katika pambano la kwanza Wajerumani chini ya Von Zelewiski waliuwawa wote akabakizwa mmoja akatoe taarifa kuwa Uheheni kuna wanaume. Vita hiyo ilipigwa eneo la Lugalo mpaka Lundamatwe Kaburi la Zelewiski liko pale Lugalo. Kuboma ni jina walilotumia Wahehe kupaita pale ambapo Wajerumani walijenga Boma lao. Blog hii ni sehemu ya kukutania kuelezana matamu na machungu ya Iringa kwa wakazi wa Iringa walioko na ambao waliwahi kuweko hapa. Blog hii itatupa nafasi ya kukutana kuelezana na kukumbushana yaliyotukuta katika kukutana na mji huu uliopo juu ya kilima . Karibuni.

Sunday, April 4, 2010

Hapo zamani za kale

Nimezaliwa Iringa, wazazi wangu wote walikuwa waalimu. Baba alikuwa akifundisha Iringa Middle School, (iliyoitwa baadae Mshindo Primary School), ambayo wenye akili fulani katika miaka ya sabini, waliamua ivunjwe ili ujengwe uwanja wa Samora. Ilikuwa ndio shule inayofuata baada ya mwanafunzi kumaliza Government Primary School, inayoitwa sasa Mlandege Primary School. Goverment iliishia darasa la nne, na Middle School ilianza darasa la tano hadi la nane. Mama alikuwa mama mendeleo na baadae akafundisha Aga Khan primary,(Shabaha Primary ambayo nayo haipo tena majengo yake yamechukuliwa na Lugalo sekondari). Na pia alifundisha St Mary's secondary , ambayo sasa ni Iringa Girls.
Nakumbuka kuanza shule Mlandege darasa la kwanza ambapo madarasa yalikuwa na makundi mawili 1A, na 1B. Nilikuwa 1B mwalimu wetu alikuwa Mwalimu Chitigo, wakati 1A walikuwa wanafundishwa na Mwalimu Mary. Mwalimu Mkuu alikuwa mwalimu George Nyakunga, ambaye bahati mbaya alifariki mapema miaka hiyo hiyo. Namkumbuka Mwalim George akituita na kutugawia uniform zetu ambazo siku hizo zilikuwa zinashonwa na fundi maalumu wa shule. Kisha nikahamia Consolata Primary ambayo leo inaitwa Chemchem, nikakutana na mwalimu Daudi Luhanga, Mwalimu Kalinga, Mwalimu Filangali, Mwalimu Mkuu akiwa Mwalimu Mwinuka. Kwa kipindi cha mwaka baba alihamia Mbeya nikasoma Aga Khan Mbeya, kisha kurudi Iringa ambapo nilisoma Aga Khan Primary wakiwemo waalim kama Mrs Saleh ambaye hadi sasa anaendesha mgahawa unaitwa Hasty Tasty, mwalim Daya, mwalimu Pabani, mwalimu mkuu akiwa Mr Thakore, kisha nilijiunga Aga Khan Secondary chini ya mwalimu Mkuu Mr Sheikh na baadae Mr Ntemo, na Mr Hassan, mwisho Iringa Teachers training Centre- Klerruu College of National Education., hapa Principal alikuwa Mzee Basimaki, ambae baadae alifuatiwa na Mr Kilimuhana. Wakufunzi wengi wa hapa walipanda sana katika serikali kuu. Mr Halinga aliwahi kuwa Mbunge Mbozi, Mr Mwanga alikuja kuwa Waziri wa Utumishi, Mh Ngw’andu waziri wa Sayansi na Technolojia.


1 comment:

  1. Nimefurahi sana kuiona picha ya bweni nililokuwa naishi. Mimi nilisoma Lugalo nikitokea Ilala primary school na nilikuwa nakaa Mkwawa(Makanyagio). Nakumbuka tulikuwa tunapita mlimani kila siku kabla sijahamishiwa bording baba yangu alivyohamia Mbeya kikazi. Sijasoma siku nyingi, wababe wetu hapi Iringa walikuwa akina Cool nine (Najua Kaka John unamjua vilivyo), pamoja na wadogo zake.
    Kweli "Sa nzusa miluka kukaye"

    ReplyDelete