Pages

Saturday, July 30, 2022

WANYAKYUSA WALITOKA UHEHENI

 


Vanu velu au watu weupe waliotoka Kilwa waliingia nchi ya Uheheni kwa amani na wakaendelea kuishi kwa amani na hatimae kuwa sehemu ya wenyeji, mfano nilioutoa ni wakina Kiwhele. 

Lakini kuna kundi jingine la watu weupe hawa waliingia kutoka kaskazini na kuingia katika eneo lililoitwa Ugunda, wenyeji wa Ugunda walikuwa ni Wategeta, habari zao nilikwisha zizungumzia awali. Jina la Ugunda lilitokana na babu yao mmoja aliyeitwa Mugunda.  Eneno la Ugunda kwa sasa linaitwa Image na tutaelezana chanzo cha jina hilo baadae. Kama mnakumbuka, niliwaeleza kuwa Wategeta walikuwa wafua chuma wazuri sana na walikuwa watu walioishi kwa mpangilio mzuri katika kazi yao hiyo, pia niliwaambia kuwa walikuwa ni watu wenye maungo makubwa yenye afya hawakuwa watu wa mchezo. Kuna kundi moja la Wahumma kutokea aidha Pawaga au Izazi, liliwashambulia Wategeta hawa ili kuwanyang’anya ng’ombe. Pamoja na Wahuma kuwa na silaha za kutisha ,Wategeta waliwakamata adui zao hao kwa mikono  na kuanza kuwachanachana vipande. Walimbakiza Muhumba mmoja tu nae walikata masikio wakamwachia aende kwao akahadithie. Baada ya hapo Wategeta wakawa mara kwa mara wanawashambulia Wahuma na kuwanyang’anya ng’ombe bila upinzani mkubwa. 
 
Lakini hili kundi la watu weupe kutoka kaskazini liliwazidi sana nguvu Wategeta. Wenyeji wengi wakalazimika kukimbia nchi yao na kukimbilia upande wa iliko Pawaga sasa, wale maadui waliwafwata mpaka huko na kuwamaliza na waliobaki kuwachukua watumwa na kwenda kuwauza Pwani. Mahala palipokamilisha vita hiyo palikuja kuitwa Malikilo maana yake pa kumalizia. Siku hizi panaitwa Kidali.

Wategeta wengine walikimbia kaskazini na kufika mpaka ulipo sasa mpaka wa Kenya na Uganda. Huko wakalikuta kabila la Wasamia na kuwashinda na kuwa watawala wao. Hata siku hizi wajukuu zao hujiita Bahehe na kusema kuwa babu zao walitokea Uheheni. Kundi jingine la Wategeta lilikimbilia Mahenge na baadae kuanza kufuata bonde la  Kilombelo kisha kuingia Ubena na kuendelea na safari hadi Kaskazini mwa Ziwa Nyasa, wakaanza kuishi sehemu waliyoiita Kavala, maana yake  peupe penye kuwaka jua, wakaendelea na kazi yao ya asili ya uhunzi. Wengi wao walikuwa wa ukoo wa kina Chusi na wakawa watawala, jina lao likageuka kuwa Chusa,  Wagonde wakaligeuza jina hilo kuwa Wanyachusa, au Wanyakyusa. Kuna Wanyakyusa ambao hatimae walirudi Uheheni kwa mfano ukoo wa akina Kalinga, hawa walitumia majina kama Kwilengilyova, yaani maji yangurumayo, wakikumbuka  maporomoko ya maji katika sehemu walizopita wakati wakisafiri wakifuata bonde la Kilombelo. Wengine wakijiita Magalamatitu, wakikumbuka sehemu ambapo kulikuwa tambarare  ya  ndege wengi weusi ambayo ipo mpaka leo. Hawa watu weupe waliowafukuza Wategeta waliacha uzao wao katika nchi ya Usagala. Wajukuu hawa wa Wasagala wa zamani, ambao hujulikana kama Vanyikami, huwa na madai tofauti, wengine wakidai kuwa asili yao ni waarabu, wengine wakidai asili yao ni wazungu. Wanahistoria wengi huona hiyo si rahisi kwani wangekuwa Waarabu, lazima wangeanzisha dini ya Kiislamu na hali kadhalika wangekuwa wazungu kungeletwa pia ukristu. Kinachodhaniwa ni kuwa Vanu velu hawa walikuwa ni machotara au watu tu wenye ngozi angavu.

2 comments:

  1. Twiga kwa Kihehe ni Nundulu au Singomlanzi kwa mujibu wa sisi Wana Image.

    ReplyDelete

STAT COUNTER