Kamwene vanyalukolo, leo naomba niendelee kutaja makundi
mengine makubwa ya watu walioingia Uheheni. Kundi la kwanza ni lile
lililotokea Ukimbu, hili kundi
linadhaniwa liliingia wakati mmoja na Wakilwa. Kundi hili lilikuwa likijiita
Vanyandembwe, ndembwe ni tembo, na Vanyandembwe walikuwa wakidai asili yao ni
tembo.
Kwa nyakati hizi ni ukoo wa akina Ugulumu na Ifweni ndio wajukuu wa kundi hili
la Vanyandembwe. Baadae sana liliingia kundi jingine kutoka Ukimbu hili
liliongozwa na Mufilinge aliyekuwa mtoto
wa Musawila aliyekuwa mtawala wa Ukimbu wakati huo. Na kwa sababu hiyo ukoo wa
Mfilinge huitwa Vasawila, wao walikuja kuishi sehemu za kutoka Makungu mpaka jirani ya Wasa na eneo hilo lilikuja
julikana kama Usawila.
Inawezekana walikuwa na uhusiano na Vanyamahuvi
kwani , walipofika Uheheni walikaribishwa na Vanyamahuvi na kupewa eneo la Makungu watawale, lakini baada ya muda mfupi
waliongezeka na kutawala kuanzia Kiponzelo mpaka Malangali, jambo lililowaletea
uadui na ukoo wa Nyilowa na Nyakunga ambao hatimae walihamia Uhafiwa na
Udongwe.
Hawa Wasawila walipoingia uheheni walikuwa wakivaa aina ya nguo iliyotengenezwa
kwa magamba ya miti yaliyotwangwa,
wenyeji wakawaita Vanyamwenda.
Pia walikuwa waganga wazuri hivyo wanawake zao wakapewa mwidiko ( muitikio) wa
Ganga, wakati wanaume zao waliitika kwa Mikwile au Nyasite.
Wasawila waliendelea kukumbusha kuwa wao ni Wakimbu. Makundi mengine yalichukua
lugha ya wenyeji na hakika Kihehe kilipata mchango wa maneno kutoka lugha
nyingi za wageni walioingia.
Kwa mfano Wakimbu ndio walioleta neno Mtemi,
ambalo walilikopa ktoka kwa jirani zao Wanyamwezi. Wahehe wakaanza
kutumia neno Wutemaa kumaananisha utawala, kabla ya hapo walikuwa wakitumia
neno Wumutwa ambalo lilitoka kwa Wabena.
Kwa Wahehe jina Mtemi hutumika likiwa na maana mkata shauri au hakimu, kutema
ni kukata. Wahehe waliamini mtunga sheria asiyehukumu na kuadhibu hawezi
kuheshimiwa.
Lugha ya Kihehe imebadilika sana, kwa mfano ,nakumbuka wimbo ambao babu yangu
alinifundisha na kunambia kuwa ulikuwa wimbo wa askari wa Kihehe walipotoka
vitani, wacha niuimbe mwenye kuweza kuutafsiri tafadhali fanya hivyo kwenye
sanduku la Comment hapo chini;
Mitela
kimalimali na manyile mtalavande
Oh Likalikasela
Oh likoko ngomba mitela
Ukoo wa Ndondole hasa akina Kindole walisifika kupenda kujikweza kuwa wao ni
ukoo wenye hadhi, wanaume walijiita
Mulugu Mutavangu, maana yake kiongozi wa wapiganaji na wanawake wakajiita
Vanyatage yaani waliotupwa, hii ilikuwa kukumbusha kitendo cha Kindole
kung’ang’ania kutawala Lungemba, na kumtupa kaka yake Chota aliyekwenda
kutawala kwa Mnyaluhwao.
Baadae Wahehe waliendeleza utamaduni huu kwa kumuita mwanaume mwenye hadhi Mulugu na mwanamke mwenye hadhi
Mtage.
ino ya mtage ulonzile pi mtwa vangu ve
ReplyDeleteNyee nahangaika kupata historia nakuandikia na kukusomea nikusomee?
ReplyDelete