Jina Iringa lilitokana na neno la Kihehe Lilinga ambalo tafsiri yake kwa Kiingereza ni Observation Post. Wahehe walianzisha lilinga sehemu hii ilipo Iringa ya sasa, ilikuweza kuwaona maadui kwa urahisi na kuweza kutoa taarifa za kulinda Ikulu iliyokuweko Kalenga. Wajerumani walijenga Boma juu ya kilima hicho hicho baada ya ushindi uliopatikana baada ya kupigana na Wahehe kwa mara ya pili. Katika pambano la kwanza Wajerumani chini ya Von Zelewiski waliuwawa wote akabakizwa mmoja akatoe taarifa kuwa Uheheni kuna wanaume. Vita hiyo ilipigwa eneo la Lugalo mpaka Lundamatwe Kaburi la Zelewiski liko pale Lugalo. Kuboma ni jina walilotumia Wahehe kupaita pale ambapo Wajerumani walijenga Boma lao. Blog hii ni sehemu ya kukutania kuelezana matamu na machungu ya Iringa kwa wakazi wa Iringa walioko na ambao waliwahi kuweko hapa. Blog hii itatupa nafasi ya kukutana kuelezana na kukumbushana yaliyotukuta katika kukutana na mji huu uliopo juu ya kilima . Karibuni.

Sunday, October 7, 2012

WAZEE WA KIHESA -1-MZEE PHILIPO SAWANI

Mzee huyu wa kabila la Kikinga ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa Kihesa alikuwa mkulima eneo la Ngano Isimani. Huku akiendesha biashara ya duka na bar hapo KIHESA katika nyumba yake ya kisasa kabisa. Wazee matajiri wa mji wa Iringa mfano Mzee Mwaitebele, Mzee Idd Mwangubi, Mzee Zabron Mwanyato pamoja na wafanya kazi maofisa kama Mzee Asam Sajio Kaduma walipenda kunywa kwenye bar ya Mzee Sawani. Lakini pia alipokuwa Mwenyekiti wa Tanganyika African Parents Association (TAPA) wa wilaya na alinunua jengo kwa pesa zake na kulifanya shule ya TAPA ambayo kwa sasa inaitwa Shule ya Msingi Mtwivila. Na mwalimu wa shule hiyo wa kwanza alikuwa Mwalimu Edward Chaula ( Baba Kichupa ) na Joseph Msandi ambao mishahara yao ililipwa na mzee Philipo Sawani. Jully Sawani ni mtoto wa Mzee Sawani ambaye alikuwa diwani wa kwanza Kihesa. Mzee Sawani alikuwa  mtu nadhifu sana akipendelea kuvaa English suit. Ama kwa hakika Mzee Philipo Sawani ana mambo mengi sana aliyochangia kwa Kihesa na maisha ya wengi tukisema tuyaandike yote hapatoshi.

No comments:

Post a Comment