Jina Iringa lilitokana na neno la Kihehe Lilinga ambalo tafsiri yake kwa Kiingereza ni Observation Post. Wahehe walianzisha lilinga sehemu hii ilipo Iringa ya sasa, ilikuweza kuwaona maadui kwa urahisi na kuweza kutoa taarifa za kulinda Ikulu iliyokuweko Kalenga. Wajerumani walijenga Boma juu ya kilima hicho hicho baada ya ushindi uliopatikana baada ya kupigana na Wahehe kwa mara ya pili. Katika pambano la kwanza Wajerumani chini ya Von Zelewiski waliuwawa wote akabakizwa mmoja akatoe taarifa kuwa Uheheni kuna wanaume. Vita hiyo ilipigwa eneo la Lugalo mpaka Lundamatwe Kaburi la Zelewiski liko pale Lugalo. Kuboma ni jina walilotumia Wahehe kupaita pale ambapo Wajerumani walijenga Boma lao. Blog hii ni sehemu ya kukutania kuelezana matamu na machungu ya Iringa kwa wakazi wa Iringa walioko na ambao waliwahi kuweko hapa. Blog hii itatupa nafasi ya kukutana kuelezana na kukumbushana yaliyotukuta katika kukutana na mji huu uliopo juu ya kilima . Karibuni.

Monday, April 5, 2010

Consolata Primary School 4

Kila shule yenye hadhi enzi hizo ililazimika kuwa na bendi ya shule. Bendi ilipiga kila asubuhi wakati wa ukaguzi. Wanafunzi walikaguliwa kuanzia nywele, kucha nguo meno kama wamepiga mswaki, na siku nyingine kila mtu alilazimika kuja na mswaki kuuonyesha , ole wako uje na mswaki wa kisasa ni viboko tu, ilikuwa lazima utumie mswaki wa mti tena mti maalumu, sababu ilikuwa miswaki ya miti ina utomvu unaotunza meno, miswaki ya plastic lazima uweke dawa. Sweta ilikuwa marufuku, viatu vya ngozi vilikuwa ni nadra sana na anaevaa kulikuwa naina maalumu ya viatu. Bata shoes. Mwenye nywele ndefu alikuwa ananyolewa alama ya msalaba kichwani hivyo mwenyewe anaenda malizia zilizobaki. Wakati wa inspection ulipigwa wimbo wa Baba Paka, au Tanganyika Tanganyika. Kisha nyimbo kama Ngo ngo ngo twaingilia zilikuwa ni za kuingilia darasani. Siku za sherehe ndipo kila shule ilitanguliwa na bendi yake wanafunzi wakienda kwa gwaride safi kuliko mgambo wa siku hizi. Sijisifu lakini bendi yetu chini ya Mwalimu Daudi Luhanga ilikuwa the best wakati huo. Mbwembwe za mshika fimbo ilikuwa ni kivutio tosha huku akiwa kavishwa vitambaa vyenye rangi mbalimbali......loh

No comments:

Post a Comment