Pages

Monday, April 5, 2010

Aga Khan Primary



Kutokana na baba kuhamia Mbeya nilihama kutoka Consolata Iringa na kuendelea na shule Aga Khan primary Mbeya, na baada ya mwaka nilirudi tena Iringa ambapo niliendelea kusoma Aga khan primary Iringa. Kuna mambo mengi yalinikuta wakati huu, kwanza shule hizi zilikuwa na asilimia kubwa ya wanafunzi na waalimu wa kihindi, masomo yote yalikuwa ya kiingereza na mimi nilitoka shule ya kiswahili full time. Kiingereza chenyewe cha kihindi. Kwa miezi ya kwanza nadhani nilikuwa nahudhuria tu darasani. Lakini nakumbuka kitu cha kwanza nilichoshangaa ni jinsi watot wa kihindi walivyopenda kula, kila mmoja alikuwa anakuja shuleni na kopo la chakula, wakati wa mapumziko ilikuwa wakati wa kukaa vikundi kila mtu anatoa chakula chake na kajipati kanaendelea. Kila mtu alionekana anakuja shuleni na pesa. Hapa ndio nikakutana na magazeti yanaitwa comics. Beano, Dandy, Beezer, Xmen, Superman, Batman na kadhalika. Kila jumanne Beano na Dandy jipya lilitoka, na kila alhamisi Beezer. Ujio wa magazeti ya Film na Boom yaliongeza utamu na kila Jumanne watu tuliwahi Bookshop kununua Film ili tujue mkasa gani mpya umemkuta Rabon Zoro kwenye mikono ya Lance Spearman. Na Fearless Fang na mikasa yake porini. Kila saa sita magari kibao yalikuwa yanakuja shuleni kuwachukua wanafunzi kuwarudisha nyumbani kwa chakula cha mchana. Vijana wawili walikuwa wanabishana kuhusu uwezo wa Spear kuruka kutoka kwenye magari yanayokimbia kama walivyokuwa wakimwona kwenye picha za magazeti. Mmoja akasema anaweza, na wakati wako karibu na msikiti wa Miyomboni mtoto wa kihindi akajitosa toka kwenye gari, hakupata nafasi ya kuanguka kama Spear, aliangukia uso kwenye lami na kukaa hospitali mwezi mzima

No comments:

Post a Comment

STAT COUNTER