Pages

Tuesday, April 6, 2010

Aga Khan 2


Siku za sikukuu za Kitaifa hazikuwa nzuri kwa watoto wa Kihindi, maana ndio siku za kukutana na wanafunzi wa shule nyingine siku hiyo watavutwa nywele watataniwa,jamaa zangu wa Kisingasinga watavuliwa vilemba, basi ikikaribia siku ya sikukuu kama vile Muungano au Sabasaba, utaona waswahili tunaanza kukaribishwa kile chakula cha saa nne wakati wa kupumzika, na sentensi zinazokuwepo ni, "John you r my friend no? You vill stay with me during mandomando?" Hapo unakubali au unamuuliza atakulipa shilingi ngapi, mara nyingi malipo yalikuwa uhakika wa kuletewa Comics mwezi au kupewa pesa za kwenda sinema kwa kazi hiyo ya ubodigad. Urafiki huo ulikuwa wa muda tu. Pamoja na kuwa katika shule za wahindi kwa miaka mingi nina rafiki wawili tu wa kipindi hicho. Ni ukweli usiopingika kuwa shule nilizotoka zilikuwa na nidhamu ya juu kuliko hizi za Aga Khan, japo huku mambo mengi yalikuwa bora, vitabu, madaftari, maktaba ya shule vilikuweko, kazi kama za kusafisha vyoo huku zilikuwa na mtu maalumu, si zamu za wanafunzi kama nilikotoka. Adhabu zake zilikuwa laini laini, ukikorofisha sana unapumzishwa shule wiki, au adhabu iliyoonekana kali ilikuwa kuandika kosa lako mara nyingi. Ukikutwa unakula Bazooka , basi utaambiwa uandike 'Sitakula bazooka darasani,' mara mia mbili. Unajikuta sentensi hiyo umejaza daftari nzima.
Mambo mengine yalikuwa sawa ngumi za siku ya kufunga shule zilikuweko, na watemi walikuweko, alikuweko kijana moja anaitwa Moez K, yeye ndo alikuwa mtemi mpaka kaka zake walikuwa wanamfwata akawatetee kukiwa na ngumi. Peke yake alikuwa na jeuri ya kutandikana ngumi na waswahili.
Kila asubuhi kabla ya kuingia darasani kulikuwa nakusali, kihindi kwenye foleni haikuchukua muda mrefu wote tulikuwa tunasali kihindi, na hata kuongea kihindi.

1 comment:

  1. Kaka Kitime hivi utani wa jadi kati ya Highlands Sec School na Lugalo (Aga Khan), ulikuwa kama ambao tulioukuta kizazi cha sasa?

    ReplyDelete

STAT COUNTER