Jina Iringa lilitokana na neno la Kihehe Lilinga ambalo tafsiri yake kwa Kiingereza ni Observation Post. Wahehe walianzisha lilinga sehemu hii ilipo Iringa ya sasa, ilikuweza kuwaona maadui kwa urahisi na kuweza kutoa taarifa za kulinda Ikulu iliyokuweko Kalenga. Wajerumani walijenga Boma juu ya kilima hicho hicho baada ya ushindi uliopatikana baada ya kupigana na Wahehe kwa mara ya pili. Katika pambano la kwanza Wajerumani chini ya Von Zelewiski waliuwawa wote akabakizwa mmoja akatoe taarifa kuwa Uheheni kuna wanaume. Vita hiyo ilipigwa eneo la Lugalo mpaka Lundamatwe Kaburi la Zelewiski liko pale Lugalo. Kuboma ni jina walilotumia Wahehe kupaita pale ambapo Wajerumani walijenga Boma lao. Blog hii ni sehemu ya kukutania kuelezana matamu na machungu ya Iringa kwa wakazi wa Iringa walioko na ambao waliwahi kuweko hapa. Blog hii itatupa nafasi ya kukutana kuelezana na kukumbushana yaliyotukuta katika kukutana na mji huu uliopo juu ya kilima . Karibuni.

Friday, April 9, 2010

Aga Kha Secondary 2


(Picha ya juu Hostel ya wanafunzi wa Kihindi, chini madarasa Aga khan)
Chini ya Headmaster Mr Sheikh, ambaye baadae alitoka na kwenda kuanzisha Highland Secondary School, tulianza masomo. Mi nadhani nina bahati na herufi B. Darasa la kwanza na la pili nilisoma Government Primary Std IB na IIB, nikahama shule na kuingia Consolata Primary na kusoma IIIB na IVB, nilipofika Aga Khan Secondary nikasoma Form 1B na Form 2B.
Form 1B lilikuwa darasa lenye watu wa kukumbuka maana walikuwa na mengi waliyoyafanya katika kipindi chote cha O level. Namkumbuka Andrew 'Kojo' au 'The artfull dodger', alijipa jina hili baada ya kusoma kitabu cha Oliver Twist, na kujikuta ana uwezo wa kutoroka darasani wakati mwalimu anaandika ubaoni. Walikuweko Frank na Japhet vijana wawili wa Kichaga waliokuwa mabingwa wa draft, hao waliweza kucheza draft hata katikati ya kipindi wakati mwalimu anafundisha. Eberhard, bingwa wa kusoma. Abasi alieacha shule baada ya miezi michache akisema haelewi kitu kinachoendelea . Tulikuwa na waalimu wahindi , waswahili, Mu Irish, Mrusi, Wamarikani, Mnorwegian. Kazi kubwa ilikuwa. Kati ya waalimu wa kukumbukwa alikuweko Mr Dhanani, huyu alikuwa mwangalizi wa Hostel ambayo kwa wakati huo ilikuwa ya Wahindi watupu, na pia alikuwa mwalimu wa Book keeping. Utamu wa mwalimu huyu ni Kiingereza chake cha kihindi na jinsi alivyokuwa anashindwa kabisa kutamka majina ya waswahili, rafiki yangu Mbembati aliishia kuitwa Mabemabati kila siku, Mr Dhanani alikuwa na mwandiko mzuri sana, mpaka wengi tukawa tunajitahidi kuuiga.
Katika kipindi hiki kukaanzishwa gwaride la Kimapinduzi, wataalam wa gwaride hili walikuja kutoka Zanzibar. Amri za gwaride hili zote ziliishia neno z,..Nyumaz geuka, kushotoz geuka, kuliaz geuka. Lilikuwa gwaride la mapozi na silaukakamavu kama lile la jeshi. Kuna mambo ya kuchekesha lakini kila mara ilikuwa huruma kuangalia watoto wa kihindi wakijaribu kutembea katika paredi, kila wakijaribu walijikuta mkono wa kushoto na mguu wa kushoto vinaenda pamoja na mguu wa kulia na mkono wake vinaenda pamoja.

1 comment:

  1. Mzee Kitime kweli nyie ndo mliifaidi sana Lugalo sekondari. Nasi pia kwa ile miaka yetu tulikuta chakula cha mchana shuleni nikitokea Kihesa shule ya Msingi. Tuliona kama ajabu tukipata ndizi, mikate tena bila kugombania. Mchanganyiko uliendelea kwani kuna wanafunzi walikuwa wakitoka Mbeya na sehemu nyingine kila mwaka. Hii ilileta umoja wa kitaifa na kuondoa ukabila. Kwa sasa jambo hili halipo bali limebaki la vyuo vikuu tu kwani sekondari ya Lugalo ni high school inayotakiw kupokea wanafunzi wote wa shule za kata toka pale Iringa mjini.

    ReplyDelete