![]() |
Isimila |
Tukirudi nyuma kama miaka 11,000 iliyopita tuna ushahidi kuwa walikuweko binadamu ambao walitumia silaha za kuchonga mawe, kihistoria zama hizo hujulikana kama zama za mawe au stone age era.
Kilomita chache
kutoka mji wa Iringa, ukiwa unaelekea na
barabara kuu iendayo Mbeya, kuna sehemu inaitwa Isimila,
hapa katika bonde moja kubwa kunapatikana ushahidi wa
vipande vya mawe vilivyochongwa kwa ajili ya kazi mbalimbali hasa za uwindaji
katika zama hizo.
Wahehe walipopafahamu hapa ndipo wakapaita Isimila, jina
linalotokana na neno la Kihehe ‘simo’, maana yake fumbo. Kwani kuweko kwa
silaha zile za mawe kwa wahehe lilikuwa fumbo.
Ukiingia sehemu za Usagala kuna mlima uitwao Ikombagulu,
huku kuna pango ambako iko michoro ya zamani sana, kuonyesha kuwa pia kulikuwa
na watu waliokuwa na utamaduni wa michoro ya mapangoni.
Katika bhonde la mto Lya Ndembela kuna ushahidi wa kuishi
watu ambao Wahehe katika simulizi zao waliwaitwa Vanyidaha,
watu hawa waliacha
ushahidi wa utamaduni uliofanana sana na utamaduni wa Wairaki wa huko Mbulu,
kuna watafiti wanasema wakazi hao walikuwa Wairaki wa zamani.
Baadhi ya utamaduni
waliouacha Wairak hawa ni kulima kando ya mito maarufu kwa jina la finyungu, na
kutumia mawe ya kutoka mtoni kusagia nafaka.
Wahehe waliendeleza utamaduni huu na huita mawe hayo nunulilo.
Pia walikuwa na utamaduni wa kujenga majengo ya mviringo
kutumia mawe,mpaka miaka ya mwanzoni ya 60 kulikuwa na mabaki ya jengo la namna
hiyo kule Kiwiluka, ambalo lilikuja fumuliwa taratibu na watoto. Kule Engaruka,
Monduli kulikuwa na mabaki ya majengo ya aina hiyohiyo.
Katika bonde hilo la Lyambangali kulikuwa na masalia ya
majengo mengine, yaliyojengwa kwa matofali ya kuchomwa. Wahehe katika simulizi
zao za kale walisema waliojenga nyumba hizo walikuwa Waiyenzele,
Ugogoni kulikuwa na
masalia ya majengo kama hayo na Wagogo walisimulia kuwa wajenzi wa magofu yale
walikuwa Wamankala, lakini hakuna maelezo zaidi kuhusu watu hawa kuwa
Waiyenzele au Wamankala walikuwa wa aina gani , walitoka wapi, na walienda
wapi.
Watu wengine waliokuweko katika nchi hii walikuwa ni
Mbilikimo. Kuna hadithi za kale za Wahehe kuwa hawa Mbilikimo walikuwa hodari
kwa mishale, kwa vile walikuwa wafupi walikuwa wanawaona watu wengine mapema na
kupiga kelele ‘Ngulenge’ yaani
nimekwisha kulenga.
Kama mtu alimuona Mbilikimo kwanza alimwambia ,
Nguwene’ maana yake nimekuona, na hawa
mbilikimo, walikuwa wakiuliza umbonie kwi? Kwa sababu hiyo mpaka zama hizi
Mbilikimo au watu wafupi Uheheni, hujulikana kwa jina la utani, Mwanangulenge
au Wambonie kwi
Kundi jingine la watu waliokuweko katika uwanda huu wa
Wahehe kabla ya ujio wa Wahehe walikuwa Wahamya au kwa Kiingereza huitwa
Bushmen, hawa ni wafupi lakini si wafupi kama mbilikimo na pia huwa ni weupe
kiasi.
Hawa walifika mpaka sehemu za Manyoni na kuanza
kuchanganyika na wenyeji, wajukuu za Wahamya hawa waliobakia Uheheni huitwa kwa
mwidikiso wa Mkemwa na mwiko wao (msilo), ni nyama ya pundamilia.
Ukoo wa kina Mwisaka chanzo chao ni Wahamya hawa.
Kundi la mwisho ni Vahumma, Wahehe hutamka Vahumba, ni kundi
ambalo kwa Kiingereza hujulikana kama
Hamitic.
Hawa nao walienda kuweka maskani yao katika bonde la
Lyambangali .
No comments:
Post a Comment