Baada ya
Shaka ka Senzangakhona, au kwa jina maarufu Shaka Zulu,kurithi utawala wa
Wazulu baada ya kifo cha baba yake, kati ya
mwaka 1818 na 1828 alianzisha utawala wa kikatili wa kuua na kuteka
tawala zilizokuwa jirani yake. Kipindi hiki kigumu kwa Wazulu kilipewa jina Mfecane, viongozi wa makabila makubwa kama
Zwangendaba, Mzilikazi, na Shoshangane
wakaanza kuhamisha watu wao na kuelekea kaskazini mwa nchi yao ya awali ili
kukimbia vita hizo za Shaka Zulu, nao katika kusafiri kwao wakapiga na kuteka
mali za makabila walioyakuta njiani mwao bila huruma.
Wavamizi hawa wengine wakaingia eneo sasa linaloitwa Tanzania kupitia iliko Malawi, wengine wakabaki sehemu ulipo mkoa wa Ruvuma hawa wakaja julikana kwa jina la Wangoni, jina lililokuwa kwa asili la ujumla wa makabila mengi yaliyokuwa jirani na
Wazulu. Baada ya kutujila na kujijenga sehemu hii, mwaka 1878 jeshi la Wangoni lilipenya
Ubena toka kusini mpaka kaskazini bila upinzani wowote na hatimae kuingia
katika himaya ya Munyigumba.
Askari wa
jeshi hili la Wangoni, walikuwa hodari wasioogopa kifo. Walitumia bangi kuondoa hofu yoyote, hivyo walifanya walichotaka katika nchi ya Ubena.
Munyigumba alikuwa
hajapata nafasi ya kutayarisha majeshi yake kwa uvamizi wa watu hawa kutoka kusini, hivyo alipojaribu kuwazuia kazi
ilikuwa ngumu sana, majeshi ya Munyigumba yalianza kusukumwa nyuma kwa urahisi kabisa. Munyigumba
alirudishwa nyuma hadi karibu na Image na akalazimika kukimbilia kwenye mapango
ya Nyamulenge na kujificha humo. Wangoni walipomgundua walimzingira na hakika ilionekana kuwa
ndio mwisho wa Mutwa huyo.
Bahati nzuri
sana mwanae Munyigumba, Mukwava
aliyekuwa na umri wa miaka 23 wakati huo alikuwa tayari askari jemadari
aliyekamilika, hivyo alikusanya askari na kutengeneza jeshi imara na kuelekea
Image. Alijipanga vizuri na kuwazunguka Wangoni, kisha kuwashambulia kutoka
mgongoni, Wangoni hawakuwa na namna ila kujiokoa, wakakimbia wakirudi kwao
kupitia Lulanga, kule wakashambuliwa tena na Mutengela aliyekuwa mutwa wa
Wakinamanga, tena yeye akawafukuza mpaka ndani ya nchi yao. Wangoni hawakuamini kipigo hicho kwani katika vita zao
zote walikuwa na kawaida moja tu kushinda vita. Walirudi kwao na kutulia kwa
muda mrefu.
Kiasi
cha mwaka mmoja baada ya mapambano hayo na Wangoni, Mutwa Munyigumba akafariki.
Kikaanza
kipindi chenye mashaka sana, kwani wakati wa uhai wake Munyigumba alikuwa na
msaidizi wake ambaye alikuwa pia mkwewe. Mtu huyu aliyekuwa pande la mtu na
ambaye Munyigumba alimpa mamlaka makubwa, hivyo alikuwa akihofiwa sana. Huyu bwana
alikuwa wa ukoo wa Lunyungu, kwa majina alikuwa akiitwa Mwanakimamule au Pokavilonga.
Mwenyewe alijiita wa ukoo wa Mwamubambe au wengine huita Mwambambe, jina
alilolitoa kutoka jina la baba yake Mubambe.
Wakina pia Muyinga walimhofu sana
mtu huyu na hofu yao haikuwa bure hakuwa mtu wa kawaida. Kutokana na hofu hiyo akina Muyinga wakaacha kumtawaza
Mkwava kwa vile waliona bado kijana mdogo ambaye walihisi asingeweza kushindana na hila za
Mwamubambe. Hivyo wakamteua ndugu yake aliyeitwa Mhalwike awe Mutwa. Haikuchukua muda mrefu woga wa kina Muyinga ukadhihirika, Mwamubambe alimuua
Muhalwike na kumtawaza ndugu yake aliyeitwa Mwamuhenga. Huyu alikuwa mtawala jina tu
kwani mtawala rasmi alikuwa Mwamubambe.
Hapo ikalazimika Mkwawa aikimbie nchi
yake mwenyewe.