Pages

Wednesday, August 4, 2010

Prefect wangu


Abbas Kandoro alikuwas prefect wangu Aga Khan Secondary, siku hizi Lugalo Secondary Iringa. Namfahamu toka enzi hizo . Nina uhakika atafaa sana kuwa Mbunge wa Kalenga. Kalenga mtakuwa mmelamba dume mkimchagua Kandoro

Sunday, April 11, 2010

Aga Khan 3

Niligusia hapo awali kuwa nilipoingia Form One nilikuta wanafunzi wengi kutoka Mwanza wakiwa Form Two, ni karibuni tu ndio nilikuja fahamu sababu. Usitishwaji wa darasa la nane ulianza kwa awamu tofauti katika Kanda mbalimbali, kuna kanda ambazo zilianza kufuta darasa la nane tangu 1965, wakati Kanda ambayo Iringa ipo walifuta darasa la saba 1967. Hivyo basi wale wanafunzi waliolazimika kuingia Form One kutoka mikoa ya kaskazini walipelekwa mikoa ya kusini kama Iringa ambako kulionekana kuna nafasi, tatizo ni kuwa nafasi hii haikupatikana kwa wanafunzi wa ziada waliomaliza darasa la saba na la nanewaliotoka kusini, hivyo wengi kukosa nafasi ya kuendelea iliyokuwa imechukuliwa 1966. Pamoja na kuonekana ni jambo la kawaida lakini matokeo ya nafsi hizo kukosekana kwa wanafunzi wa kusini yanaonekana mpaka leo.

Friday, April 9, 2010

Aga Kha Secondary 2


(Picha ya juu Hostel ya wanafunzi wa Kihindi, chini madarasa Aga khan)
Chini ya Headmaster Mr Sheikh, ambaye baadae alitoka na kwenda kuanzisha Highland Secondary School, tulianza masomo. Mi nadhani nina bahati na herufi B. Darasa la kwanza na la pili nilisoma Government Primary Std IB na IIB, nikahama shule na kuingia Consolata Primary na kusoma IIIB na IVB, nilipofika Aga Khan Secondary nikasoma Form 1B na Form 2B.
Form 1B lilikuwa darasa lenye watu wa kukumbuka maana walikuwa na mengi waliyoyafanya katika kipindi chote cha O level. Namkumbuka Andrew 'Kojo' au 'The artfull dodger', alijipa jina hili baada ya kusoma kitabu cha Oliver Twist, na kujikuta ana uwezo wa kutoroka darasani wakati mwalimu anaandika ubaoni. Walikuweko Frank na Japhet vijana wawili wa Kichaga waliokuwa mabingwa wa draft, hao waliweza kucheza draft hata katikati ya kipindi wakati mwalimu anafundisha. Eberhard, bingwa wa kusoma. Abasi alieacha shule baada ya miezi michache akisema haelewi kitu kinachoendelea . Tulikuwa na waalimu wahindi , waswahili, Mu Irish, Mrusi, Wamarikani, Mnorwegian. Kazi kubwa ilikuwa. Kati ya waalimu wa kukumbukwa alikuweko Mr Dhanani, huyu alikuwa mwangalizi wa Hostel ambayo kwa wakati huo ilikuwa ya Wahindi watupu, na pia alikuwa mwalimu wa Book keeping. Utamu wa mwalimu huyu ni Kiingereza chake cha kihindi na jinsi alivyokuwa anashindwa kabisa kutamka majina ya waswahili, rafiki yangu Mbembati aliishia kuitwa Mabemabati kila siku, Mr Dhanani alikuwa na mwandiko mzuri sana, mpaka wengi tukawa tunajitahidi kuuiga.
Katika kipindi hiki kukaanzishwa gwaride la Kimapinduzi, wataalam wa gwaride hili walikuja kutoka Zanzibar. Amri za gwaride hili zote ziliishia neno z,..Nyumaz geuka, kushotoz geuka, kuliaz geuka. Lilikuwa gwaride la mapozi na silaukakamavu kama lile la jeshi. Kuna mambo ya kuchekesha lakini kila mara ilikuwa huruma kuangalia watoto wa kihindi wakijaribu kutembea katika paredi, kila wakijaribu walijikuta mkono wa kushoto na mguu wa kushoto vinaenda pamoja na mguu wa kulia na mkono wake vinaenda pamoja.

Thursday, April 8, 2010

Aga Kha Secondary 1


Mwaka 1967 ndipo darasa la nane lilipofutwa Mkoani Iringa, hivyo waliokuwa std VIII walifanya mtihani na std VII tayari kwa pamoja kusubiri kuchaguliwa kuingia Form One. Kati ya wanafunzi wanane tuliochaguliwa kuingia sekondari, waswahili tulikuwa wawili, Mheshimiwa aliyekuwa Mbunge Kisyeri Chambiri na mimi. Wengine sita walikuwa wahindi. Na wote tukachaguliwa kuingia Aga Khan Secondary Iringa. Kuingia sekondari ni experience nyingine. Nilikutana na rafiki zangu niliyoachana nao Consolata, kama Emmanuel 'Katuluta', Chesus, Naboth, Nuhu, na hata wale waliotutangulia kama Gerald, John Mzungu, Kandoro, na wengine wengi. Siku ya kwanza nakumbuka kabisa tulipewa mafyekeo na kuanza kufyeka majani,kila mtu akijihisi kuwa katika hatua mpya ya maisha. Mwaka 1966 ulikuwa umeanzishwa mpango ambao uliweza kufuta kabisa ukabila, kwa kuchanganya watu toka mkoa mmoja kwenda mwingine hivyo form 2 tulioikuta ilikuwa na wanafunzi wengi sana kutoka Mwanza hususan Wasukuma. Mchanganyiko huu ulifanya maisha ya shule ile kuwa na kumbukumbu nyingi sana za furaha. Rafiki yangu Kisyeri ambaye alikuwa na bongo inacheka sana hasa kwenye mahesabu aliamua kuhamia shule ya Ufundi Ifunda, mwenyewe akiwa na picha kamili kuwa anataka kuwa engineer. Nakumbuka barua zake za kwanza kwangu akiniandikia wanaproject ya kutengeneza Hoovercraft. Hiki ni chombo kinachoweza kutembea hewani majini na kwenye nchi kavu. Nasi tukaanza maisha ya form one tukiwa na waalimu wa Kimarekani waliokuwepo kutokana na mpango wa Peace Corps. Kasheshe ndipo lilipoanza, kufundishwa Kiingereza na Mmarekani, anamaliza kipindi hata akiwauliza 'Did ya understand?' Hamjui anasema nini, wala alikuwa anasema nini kipindi kizima. Maliwato

Tuesday, April 6, 2010

Aga Khan 2


Siku za sikukuu za Kitaifa hazikuwa nzuri kwa watoto wa Kihindi, maana ndio siku za kukutana na wanafunzi wa shule nyingine siku hiyo watavutwa nywele watataniwa,jamaa zangu wa Kisingasinga watavuliwa vilemba, basi ikikaribia siku ya sikukuu kama vile Muungano au Sabasaba, utaona waswahili tunaanza kukaribishwa kile chakula cha saa nne wakati wa kupumzika, na sentensi zinazokuwepo ni, "John you r my friend no? You vill stay with me during mandomando?" Hapo unakubali au unamuuliza atakulipa shilingi ngapi, mara nyingi malipo yalikuwa uhakika wa kuletewa Comics mwezi au kupewa pesa za kwenda sinema kwa kazi hiyo ya ubodigad. Urafiki huo ulikuwa wa muda tu. Pamoja na kuwa katika shule za wahindi kwa miaka mingi nina rafiki wawili tu wa kipindi hicho. Ni ukweli usiopingika kuwa shule nilizotoka zilikuwa na nidhamu ya juu kuliko hizi za Aga Khan, japo huku mambo mengi yalikuwa bora, vitabu, madaftari, maktaba ya shule vilikuweko, kazi kama za kusafisha vyoo huku zilikuwa na mtu maalumu, si zamu za wanafunzi kama nilikotoka. Adhabu zake zilikuwa laini laini, ukikorofisha sana unapumzishwa shule wiki, au adhabu iliyoonekana kali ilikuwa kuandika kosa lako mara nyingi. Ukikutwa unakula Bazooka , basi utaambiwa uandike 'Sitakula bazooka darasani,' mara mia mbili. Unajikuta sentensi hiyo umejaza daftari nzima.
Mambo mengine yalikuwa sawa ngumi za siku ya kufunga shule zilikuweko, na watemi walikuweko, alikuweko kijana moja anaitwa Moez K, yeye ndo alikuwa mtemi mpaka kaka zake walikuwa wanamfwata akawatetee kukiwa na ngumi. Peke yake alikuwa na jeuri ya kutandikana ngumi na waswahili.
Kila asubuhi kabla ya kuingia darasani kulikuwa nakusali, kihindi kwenye foleni haikuchukua muda mrefu wote tulikuwa tunasali kihindi, na hata kuongea kihindi.

Monday, April 5, 2010

Aga Khan Primary



Kutokana na baba kuhamia Mbeya nilihama kutoka Consolata Iringa na kuendelea na shule Aga Khan primary Mbeya, na baada ya mwaka nilirudi tena Iringa ambapo niliendelea kusoma Aga khan primary Iringa. Kuna mambo mengi yalinikuta wakati huu, kwanza shule hizi zilikuwa na asilimia kubwa ya wanafunzi na waalimu wa kihindi, masomo yote yalikuwa ya kiingereza na mimi nilitoka shule ya kiswahili full time. Kiingereza chenyewe cha kihindi. Kwa miezi ya kwanza nadhani nilikuwa nahudhuria tu darasani. Lakini nakumbuka kitu cha kwanza nilichoshangaa ni jinsi watot wa kihindi walivyopenda kula, kila mmoja alikuwa anakuja shuleni na kopo la chakula, wakati wa mapumziko ilikuwa wakati wa kukaa vikundi kila mtu anatoa chakula chake na kajipati kanaendelea. Kila mtu alionekana anakuja shuleni na pesa. Hapa ndio nikakutana na magazeti yanaitwa comics. Beano, Dandy, Beezer, Xmen, Superman, Batman na kadhalika. Kila jumanne Beano na Dandy jipya lilitoka, na kila alhamisi Beezer. Ujio wa magazeti ya Film na Boom yaliongeza utamu na kila Jumanne watu tuliwahi Bookshop kununua Film ili tujue mkasa gani mpya umemkuta Rabon Zoro kwenye mikono ya Lance Spearman. Na Fearless Fang na mikasa yake porini. Kila saa sita magari kibao yalikuwa yanakuja shuleni kuwachukua wanafunzi kuwarudisha nyumbani kwa chakula cha mchana. Vijana wawili walikuwa wanabishana kuhusu uwezo wa Spear kuruka kutoka kwenye magari yanayokimbia kama walivyokuwa wakimwona kwenye picha za magazeti. Mmoja akasema anaweza, na wakati wako karibu na msikiti wa Miyomboni mtoto wa kihindi akajitosa toka kwenye gari, hakupata nafasi ya kuanguka kama Spear, aliangukia uso kwenye lami na kukaa hospitali mwezi mzima

Consolata Primary School 4

Kila shule yenye hadhi enzi hizo ililazimika kuwa na bendi ya shule. Bendi ilipiga kila asubuhi wakati wa ukaguzi. Wanafunzi walikaguliwa kuanzia nywele, kucha nguo meno kama wamepiga mswaki, na siku nyingine kila mtu alilazimika kuja na mswaki kuuonyesha , ole wako uje na mswaki wa kisasa ni viboko tu, ilikuwa lazima utumie mswaki wa mti tena mti maalumu, sababu ilikuwa miswaki ya miti ina utomvu unaotunza meno, miswaki ya plastic lazima uweke dawa. Sweta ilikuwa marufuku, viatu vya ngozi vilikuwa ni nadra sana na anaevaa kulikuwa naina maalumu ya viatu. Bata shoes. Mwenye nywele ndefu alikuwa ananyolewa alama ya msalaba kichwani hivyo mwenyewe anaenda malizia zilizobaki. Wakati wa inspection ulipigwa wimbo wa Baba Paka, au Tanganyika Tanganyika. Kisha nyimbo kama Ngo ngo ngo twaingilia zilikuwa ni za kuingilia darasani. Siku za sherehe ndipo kila shule ilitanguliwa na bendi yake wanafunzi wakienda kwa gwaride safi kuliko mgambo wa siku hizi. Sijisifu lakini bendi yetu chini ya Mwalimu Daudi Luhanga ilikuwa the best wakati huo. Mbwembwe za mshika fimbo ilikuwa ni kivutio tosha huku akiwa kavishwa vitambaa vyenye rangi mbalimbali......loh

STAT COUNTER